Kuna watu zaidi ya bilioni nane wapo hai Leo hii. Unaweza kusema kuna sababu zaidi ya bilioni nane za kutafuta hamasa ya maisha. Swali kubwa ambalo halijapata jibu kwa binadamu ni:
Kwanini tupo hai, na kwanini tupo duniani?
Watu wote bilioni nane watakuwa na majibu yao tofauti kwa nyakati tofauti za maisha yao.
Watu wa dini watasema tupo hai hapa duniani kwa ajili ya kumtumikia Mungu a kusifu ukuu wake. Hivyo wanaamini kuwa lengo la maisha ni kuishi kwa kumpendeza Mungu, kufuata neno lake ili twende Mbinguni.
Wanasayansi wametengeneza nadharia kuwa lengo la binadamu ni kusaidia kupanua na kuboresha maisha ya kizazi cha sasa na kinachofuata. Wanaamini dhumuni la kuwa hai ni kugundua teknolojia mpya, kutatua matatizo wanayopitia binadamu na kuboresha maisha.
Kwa ufupi ni kuwa makundi mbalimbali na mtu mmoja mmoja wana mtazamo tofauti wa dhumuni kuu la binadamu kuwa hai duniani. Na majibu yetu yanategemea sana na familia uliyotoka, jamii iliyokuzunguka, marafiki na ndugu na zaidi ni uzoefu kutokana na matukio mbali mbali.
Kama umelelewa kwenye mazingira ya dini ni rahisi kukubali mtazamo wa kuwa dhumuni lako hapa duniani ni kuabudu na kumtukuza Mungu. Kama umezungukwa na jamii yenye muingiliano utaamini ushawishi wa wanasayansi an makundi mengine.
Kama umetokea familia yenye uwezo na mali, dhumuni lako la kuwa duniani litahusisha sana wewe kutunza mali za familia au kuziongeza mara dufu. Na kama umetokea familia ya kimasikini, dhumuni kubwa la maisha yako litakuwa ni kutafuta mali, kupambana kuitoa familia yako kwenye umasikini.
Na kadri tunavyokuwa kwenye maisha ndio dhumuni la kuwepo duniani linabadilika. Miingiliano na jamii tofauti, elimu, uzoefu na matukio ya maisha yetu hupelekea wengi wetu kuwa na malengo tofauti ya kuwa hai duniani.
Kuna muda lengo pekee la kuwa hai ni kumaliza chuo. Kuna muda ni kupata kazi ili uanze kujitegemea. Kuna muda ni kufanikisha biashara au mradi ambao utakupa jina au heshima. Kuna muda ni kupata cheo au nafasi ya juu.
Kuna muda malengo ni kupunguza uzito, au kunenepa kidogo. Kuna muda ni kufunga ndoa na kupata watoto. Kuna muda malengo ni kuwa maarufu au kupata pesa nyingi sana.
Haya yote ni malengo yenye tija katika muda na nafasi tofauti za maisha yako. Na ni malengo hayo ambayo yanaweza kukusogeza karibu au mbali na dhumuni kuu la binadamu kuwa hai hapa duniani.
Dhumuni la mimi kuanza mbali sana kuhusu dhumuni kuu la kwako na binadamu yeyote ni kukukumbusha kitu ambacho huwa unatafuta sababu ya kusahau.
Kitu ambacho kinaumiza, kinatisha na hakina majibu wala maelezo mengi. Hicho kitu ni kifo.
Haijalishi kama utajua dhumuni lako la kuwa hai duniani au hautajua, ukifika muda wako kifo kitakutembelea.
Haijalishi kama unakubali dhumuni la kuwa hai duniani ni kutokana na maelezo ya dini au wanasayansi, ukifika muda wako kifo kitakutembelea.
Sikukumbushi kuhusu kifo ili uogope, nakukumbusha ili uanze kuishi.
Ukiweza kujua kwamba uhai wako unaweza kutoka sekunde yeyote baada ya kumaliza kusoma hii, itabidi ukae chini na kutafakari namna bora ya kuishi maisha yako.
Haujui siku wala saa ya kuondoka sasa kwanini unahairisha kufuata ndoto zako? Kwanini unakuwa na kiburi na dharau? Kwanini unaumia watu wasipoelewa ndoto na malengo yako? Kwanini una mkasirikia mtu ambaye pengine ndo ikawa mara ya mwisho kuwasiliana?
Steve Jobs, muanzilishi wa kampuni ya Apple, watengenezaji wa simu za iPhone aliongea vizuri sana namna ambavyo kifo kinamsaidia kuishi vizuri, alisema :
“Nilivyokuwa na miaka 17, nilisoma kitu kinachosema “Ukiishi kila siku kama ni siku yako ya mwisho, kuna siku utakuwa sahihi na itakuwa siku ya mwisho.” Ikanivutia sana kwa sababu ni kweli. Kuanzia pale mpaka leo miaka 33 mbele, kila asubuhi nilikuwa najiangalia kwenye kioo na kujiuliza “ kama leo ingekuwa siku yangu ya mwisho kuwa duniani, ningependa kufanya ninachotaka kukifanya? Nikiona jibu ni hapana kwa siku chache mfululizo najua ni muda wa kufanya mabadiliko “
Sasa hive Steve Jobs ni marehemu, lakini aliishi maisha yake na mchango wake kwa dunia hautasahaulika. Mimi naandika ujumbe Hulu kupitia simu ambayo aliitengenezea musings wa kugunduliwa.
Na mimi nimepoteza watu wa karibu wengi sana ndani ya miaka kumi iliyopita. Ukiachana na kifo cha baba yangu, vifo vya marafiki zangu ambao tulikuwa tunalingana umri viliuma zaidi. Na bado vinaniuma sana.
Rafiki yangu wa kwanza alifariki akiwa usingizini. Kwa miaka mingi niliyomfahamu sikuwahi kusikia anaumwa au ana shida za kiafya za kufanya afariki usingizini. Rafiki yangu alikuwa na mtoto mdogo na alikuwa na malengo ya kufunga ndoa, malengo hayakutimia.
Kila nikienda kulala usiku huwa nafikiria kuwa na mimi naweza nisiamke asubuhi.
Rafiki yangu wa pili alikuwa mfanyabiashara anayepambana sana. Alikuwa na ofisi yake maeneo ya chuo kikuu. Siku moja kafika kazini akawa analalamika njaa ina muuma sana ingawa amekula. Watu wakawa wanacheka na kumtania. Akaagiza chakula tena na akashindwa kula, jioni akalalamika zaidi maumivu ya tumbo. Usiku alipelekwa hospitali na mke wake, akafariki asubuhi yake.
Kila nikisikia njaa baada ya kula napata hofu pengine ni shida kubwa ya kupelekea kifo pia kama rafiki yangu.
Mwanzoni nilikuwa naumia, nalia, na kupata hofu kila nikikumbuka kifo. Marafiki zangu tunaolingana umri wamefariki kwa vitu ambavyo hata mimi vingeweza kunitokea muda wowote. Ilinibidi nikae chini na kutafuta funzo kwenye maumivu yangu.
Nikagundua kifo kipo duniani ili kutukumbusha ufupi wa maisha. Kifo ni hamasa kubwa zaidi kwa viumbe hai vyote, kwa kutambua kuwa utakufa itabidi uishi kwa kusudio lako. Haijalishi kusudio lako ni la kidini, kisayansi au kipagani.
Una muda mchache wa kuwa hai, leo au kesho inaweza kuwa siku yako ya mwisho. Swali ni jee, unatumiaje muda mchache uliokuwa nao. Wewe ni kama mimi, umepoteza marafiki na ndugu wenye umri, rangi, afya na mawazo kama yako au bora kushinda wewe.
Kukumbuka kifo isiwe swala la huzuni, inabidi iwe swala la kukuhamasisha uishi maisha yako. Fuata ndoto zako, penda ndugu na marafiki, cheka kwa sauti, jifunze vitu na ishi maisha yako.
Dhumuni kuu la kuwa hai duniani ni kuishi, na kifo ni ukumbusho bora kabisa.
Uwe na furaha.
Uwe na afya.
Uwe huru na mateso
Upate amani.
Kama umejifunza kitu mtumie ndugu au rafiki kumkumbusha dhumuni la kuwa hai
#iThinkSo
Rogers Katuma
Financial Artist, Senior Adventurer, Occasional Storyteller and an Amateur Golfer
