Ombea Mazuri Lakini Jiandae Mabaya Yakitokea

Ni asili ya binadamu kutafuta furaha, amani na mafanikio kwenye kila kitu. Binadamu atafanya kila analoweza kujikinga na maumivu, changamoto na matatizo. Tunafanya kazi kwa bidii ili kufanikisha furaha na mafanikio.

Tutatumia mbinu yeyote ili kuwa karibu na watu wanaoweza kufanya maisha yetu yawe mazuri na yenye wepesi. Tutaenda kona yeyote ya dunia kufuata amani, furaha na upendo.

Lakini dunia imetengeneza njia za kuhakikisha kuwa mzani unakuwa sawa. Dunia inayoleta furaha inayotafutwa na binadamu imeleta maumivu pia. Dunia yenye amani imeleta chuki na vita pia. Dunia yenye mafanikio na heshima ina kufeli na dharau ndani yake.

Tangu kuumbwa kwa binadamu wa kwanza hakuwahi kupenda uhalisia huu. Binadamu wote wanapenda mazuri ya duniani lakini hawataki kupitia mabaya yake yanayofanya mzani uwe sawa. Wapo tayari kujiombea mazuri wao na kuombea mabaya wengine kama ni lazima mzani uwepo.

Nikupe mfano mmoja, chukulia umeamka asubuhi ukiwa hauna hela kabisa. Haujui utakula nini siku ya leo na hakuna mtu wa kukusaidia. Ukaamua kutoka na kutembea mtaani ukiomba Mungu mtu mwenye moyo wa kutoa atokee na kuokoa siku yako.

Ghafla ukaona kitu chenye rangi ya kijivu karibu na majani. Macho yanakwambia ile ni pochi, lakini moyo unasema mtu hawezi kuangusha pochi mazingira kama yale kwa siku ambayo wewe hauna kitu kwenye mtaa ambao haujawahi kuokota hata mia.

Baada ya kusogea karibu unakuta macho yako hayakudanganya, ni pochi ya kiume ikiwa haina vitambulisho ndani. Lakini kuna kitu cha thamani zaidi kwako, hela ya kukutosha wewe kula wiki nzima.

Kwako wewe hii ni siku bora kabisa kwenye maisha yako, utasema una bahati nzuri au umebarikiwa na kushukuru kwa kila njia. Utashukuru Mungu, babu zako, wazazi wako na pengine hata aliyepoteza hiyo pochi.

Sasa patia picha kuwa miezi imekatika tangu siku hii imetokea. Maisha yako yameendelea lakini siku ya leo hela uliyokuwa nayo mfukoni inakutosha nauli na chalula cha jioni tu. Ukaiweka vizuri hela yako kwenye pochi na kuishindilia chini kabisa kwenye mfuko wako wa koti.

Kila baada ya saa ulikuwa unakagua kama pochi ipo, na ilikuwepo. Ukapata usafiri wa kurudi nyumbani na ukawa unaanza na mipango ya wapi utachukua chakula cha bei rahisi kwa ajili ya usiku na kiporo kibaki kwa ajili ya kesho.

Kondakta akaja na kudai nauli, ukaingiza mkono kwa kujiamini sana kwenye koti lako huku ukitabasamu na kumwangalia kondakta. Ghafla sura yako ikabadilika, pozi lako la kusimama likaisha, ukachuchumaa na kulaani kwa sauti kubwa sana. Pochi yako haionekani.

Sio tu ulipoteza pochi yenye hela ya nauli na kula bali vitambulisho vyako vyote vilikuwa humo pia. Maumivu mbayo utayasikia ni makubwa sana. Na maumivu hayo ni makubwa kiasi kwamba mzani wa furaha uliyopata wakati wewe unaokota pochi hautaweza kuwa sawa kwa maumivu haya.

Ni asili ya binadamu kusikia maumivu zaidi kushinda kusikia furaha na amani mambo yakienda vizuri. Wakati unaokota pochi ulijua kuna mtu kaangusha, na ana maumivu, lakini haukujali sana kwa sababu mzani ulikuwa mzuri kwako. Sasa hivi kuna mtu mwingine kaokota au kaiba pochi yako, mzani wa maumivu upo kwako zaidi.

Huo ni mfano mmoja tu wa namna maisha yanavyoweza kutufurahisha au kutuumiza bila sisi kujiandaa. Na hiyo inatengeneza tabia ya kuwa hatutaki hata kufikiria uwezekano wa vitu vibaya kutokea kwetu kwa sababu hatutaki vitokee.

Na hiyo hufanya vikitokea, viume zaidi. Kwenye maisha utapoteza watu unaowapenda, vitu unavyovipenda, heshima, faida au hata afya yako. Hata ujiandae na ujifiche vipi vitu vibaya vitakukuta.

Vitu vibaya vinatokea muda wowote kwenye mazingira yeyote na kwa ukubwa au udogo tofauti. Kuna siku utakuwa na haraka ya kufika sehemu na ndio siku itakayo kuwa na foleni kubwa zaidi. Kuna siku utakayo amua kutembea kwa mguu na kuvaa viatu vyako vyeupe na ndio siku mvua ikaamua kunyesha.

Kwahiyo matatizo na majanga ni ya kila mtu, maumivu ni ya kila mtu pia lakini yanapungua ukiamua kutumia njia fulani.

Kuna mtu mmoja aliwahi kusema”kuwa na matumaini ya vitu vizuri kutokea, lakini jiandae kwa vitu vibaya kukukuta.” Mtu Hutu alikuwa ana maanisha kuwa matamanio na mahitaji yetu ya kutaka maisha mazuri, furaha, amani ndio chanzo kikubwa cha kufanya maumivu yawe makubwa pale mambo mabaya yanapotokea.

Tunatengeneza imani ya mambo mazuri kutokea, hivyo tunahisi mambo mabaya hayawezi kutokea. Muda mwingine tunajiambia kuwa hayawezi kutokea kwako na sio kwa muda ambao wewe unataka mambo mazuri yaje.

Mtu ambaye hana sifa nyingi na uzoefu wa kutosha akienda kuomba kazi anakuwa hana imani kubwa sana kuwa atapata, hivyo hata akikosa haimuumizi sana. Atachukua majibu yake mabaya na kwenda kuomba kazi sehemu nyingine.

Mtu mwenye uzoefu na elimu kubwa ana imani na kujiamini sana kupata kazi. Akikosa maumivu yake ni makubwa sana na ni rahisi kwake yeye kukata tamaa kwenda kuomba kazi nyingine.

Njia nzuri ya kuishi maisha ni kutambua na kukubali kuwa mambo mabaya na mazuri hutokea kwa kila mtu na hayatabiriki. Kila ukiamka asubuhi na kutengeneza ratiba yako ya siku usianze kufikiria vitu vizuri tu vitakavyotokea. Anza kufikiria ikiwa leo ndo siku yako mbaya, kitu gani kinaweza kutokea na kukuumiza?

Je, utapoteza pochi? Kuna mtu atakutukana? Kutakuwa na foleni? Utapata hasara? Utakataliwa kitu unachoomba? Au pengine ndo siku yako ya mwisho ya kuwa duniani?

Ukiweza kutumia muda mchache kufikiria uwezekano wa vitu vibaya kutokea utakuwa na amani ya moyo na maumivu hayatakuwa makubwa sana kwa sababu uliweza kutofautisha kitu kilicho chini ya uwezo wako na ambavyo dunia huamua.

Kwenye maisha hauwezi kuchagua kila kitu kitakacho kutokea, lakini una uwezo wa kuchagua kipi kitakuumiza na kipi hakitakuumiza. Kipi kikufurahishe na kipi kisikufurahishe. Na nguvu ya kuchagua inaanza kwa kukubali uwezekano wa mambo mabaya kutokea pia, na sio kutaka tu mazuri.

Kuwa na imani na omba mambo mazuri yatokee, lakini jiandae kisaikolojia kwa mambo mabaya kutokea. Utanishukuru ukiona utofauti.

Uwe na furaha,

Uwe na afya

Uwe huru na maumivu

Upate uhuru na amani

Kama kuna kitu umejifunza, mtumie mtu unayemjali

#iThinkSo

Rogers Katuma

Financial Artist, Senior Adventurer, Occasional Storyteller and an Amateur Golfer


Discover more from iThinkSoo

Subscribe to get the latest posts sent to your email.