Watu Wamekuwa Rahisi Kuwafikia Lakini Ngumu Kuwapata

Mara ya kwanza kutembelea Dubai, kila kampuni ya utalii ilikuwa inashauri nitembelee Mall ya Dubai, ambayo ni Mall kubwa zaidi duniani na pia niende kwenye jengo la Burj Khalifa, ambalo ndo jengo refu kushinda yote ulimwenguni.

Sehemu ambayo hawakuitaja ni matiririko ya maji yenye kufuata ala za muziki. Matiririko hayo yapo katikati ya hiyo mall kubwa kushinda zote duniani na jengo refu zaidi kushinda yote duniani.

Maonyesho hayo ni bure kwa kila mtu, na hufanyika kila baada ya saa moja kuanzia mida ya jioni. Mamia ya watu hutembelea na kufurahia maonesho hayo, mara kadhaa kwa siku. Na mara nyingi watu hutoa simu zao na kurekodi maonesho hayo.

Na mimi nilikuwa kama wengine, mara ya kwanza nilitoa simu na kuanza kurekodi maonesho hayo mwanzo mwisho. Yalipoisha nikaondoka kwenda kuzunguka Dubai Mall.

Baada ya saa moja mimi nilikuwa mbele kabisa tena kwenye maonesho hayo. Baada ya sekunde kadhaa nikajikuta nimetoa simu na naanza kubonyeza camera kutaka kurekodi tena. Nikaangalia pembeni nikaone wengine wote wanafanya hivyo pia.

Tuliacha kufurahia maonesho kwa macho na kupoteza muda na kurekodi. Mara ya kwanza ni sawa kwa sababu ni kitu kipya. Mara ya pili nikagundua sio sawa na kuacha kurekodi. Nikamalizia kuangalia shoo na nilifurahi zaidi.

Tukio hilo ilikuwa ni miaka nane nyuma, na tayari wengi wetu tulikuwa tunarekodi kila kitu na bado hatuna kumbukumbu ya kitu chochote tulicho rekodi.

Sasa hivi hali ni mbaya zaidi, teknokojia imekuwa kubwa sana kiasi kwamba bila simu na kurekodi ni sawa na hamna kilichofanyika.

Sasa hivi ni rahisi kumfikia kila mtu kwa simu lakini ni ngumu zaidi kumfikia mtu kihisia na kujuana kiundani. Ni rahisi sasa hivi kuwa na makundi na marafiki wengi kwenye mitandao lakini kukosa rafiki wa kweli kwenye maisha halisi.

Sasa hivi ni rahisi mtu kuwa na maisha tofauti kati ya mitandao ya jamii na maisha halisi ya mtaani. Kwenye mitandao kila mtu amejipata, ana kazi nzuri au biashara na ana marafiki wazuri sana.

Kwenye maisha halisi watu hao hao hawana kazi wapo nyumbani, hawana rafiki aliyekuwa tayari hata kuwaletea chakula wakiumwa na hawajulikani hata wanakaa wapi.

Nina rafiki yangu mmoja, kwa ukweli siwezi kusema ni rafiki bali mtu ambaye hapo zamani alikuwa kwenye kundi moja la WhatsApp na mimi. Alikuwa kwenye kundi ana chati sana, kila mtu anamjua yeye na alikuwa admini wa kundi pia.

Kuna siku akaandika meseji akasema “jamani naombeni msaada wenu, bibi yangu anaumwa na amelazwa hospital. Kaambiwa wataacha kumtibu isipopatikana elfu kumi na saba ya kitanda cha siku iliyopita”.

Wakati mimi naingia kwenye WhatsApp ile meseji yake ilikuwa na masaa nane tangu atume. Hakuna ailyejibu. Ilivyofika jioni, watu wakaanza mada za mpira wa simba na yanga na shida yake ikapuuzwa.

Mimi nikamfata pembeni na kumtumia ile hela, kisha nikajiondoa kwenye kundi lile na makundi mengi zaidi ya WhatsApp.

Ile hali ilinikumbusha uhalisia wa watu wengi, tunajuana na watu wengi lakini hatupo karibu nao. Tuna presha ya kutaka kuonyesha vitu mitandaoni ambavyo havipo kwenye uhalisia.

Mimi wakati natoa simu yangu kurekodi yale maonesho Dubai nilikuwa nimetoka kupoteza hela, nimetoka kuchelewa treni kwenda kwenye sinema na nilikuwa naharisha baada ya kula chakula ambacho nadhani kilichacha.

Lakini ile video ningetuma kwa lengo la kuonyesha kuwa Dubai kila kitu ni poa na nakula bata. Najua na wewe unapitia hali kama hiyo.

Una watu ambao njia pekee ya kuwasiliana ni kujibu kwenye status za WhatsApp. Upo kwenye makundi zaidi ya mia lakini ukipata shida hakuna wa kukusadia.

Bado una presha pia ya kutaka kuonekana umejipata na maisha ni poa. Unavimba kwenye mitandao kuwa asiyekusalimia haumsalimii, asiyekutafuta haumtafuti.

Lakini ukiwa pekee yako unaumia.

Jaribu kukaa chini na kutafakari maisha yako ya ukweli na presha za mitandao na teknolojia. Anza kujenga mahusiano ya kweli na watu wachache bora.

Anza kuwatafuta watu bila kuomba vitu au kupitia kujibu tu status zao. Jifunze namna ya kutembelea watu makwao na kujua wanachofanya. Jifunze kuongea na watu bila kushika simu au kurekodi kila kitu.

Maisha ya kweli yenye furaha, amani na upendo bado yanajengwa kwa njia za kawaida. Usiruhusu teknolojia iwe ukuta wa maisha yako.

Na usirubunike kudhani kila mtu kwenye mitandao ya jamii ana maisha mazuri kushinda wewe.

Acha kurekodi, anza kuishi.

Uwe na furaha,

Uwe na afya,

Uwe huru na mateso,

Upate amani

Kama umejifunza kitu, mtumie mtu mmoja unayemjali.

#iThinkSo

Rogers Katuma

Financial Artist, Senior Adventurer, Occasional Storyteller and an Amateur Golfer


Discover more from iThinkSoo

Subscribe to get the latest posts sent to your email.