Vitu Sio Gharama, Ni Wewe Ndio Hauwezi Kuvinunua

Kukuzwa na mama bila baba kuwepo kwenye maisha yangu kulinipitisha sehemu nyingi sana ambazo nilikuwa nakumbushwa kuwa vitu ninavyotaka ni gharama, hususani shule ya msingi . Mara nyingi nilikuwa nikiomba sare za shule mpya naambiwa “ Sare zenu ni gharama sana, hakikisha unatunza ulizokuwa nazo mpaka mwakani”

Nilipomuomba mama aniunganishe na mimi kuwa kwenye ratiba ya wanafunzi wanaopanda gari ya shule wakati wa asubuhi na jioni niliambiwa gharama ni kubwa sana. Nijitahidi kupambana na daladala na siku nyingine nisiwe mvivu wa kutembea kwa miguu.

Majibu hayo ya mama hayakuwa yananiumiza sana kwa sababu nilikuwa naona wenzangu pia wenye uwezo mdogo wakipitia changamoto ile ile. Niliumia sana pale niliponyimwa kununuliwa vitu vya kuchezea mpira wa miguu. Nilikuwa ni miongoni kwa wachezaji watatu tu tunaocheza peku kwenye timu ya shule.

Kocha wa timu akasema nisipopata viatu ataniondoa kwenye timu. Nilirudi nyumbani na kumbembeleza sana mama aninunulie, na akakataa. Sababu yake ni ileile, viatu vya mpira wa mguu ni gharama sana. Nililia sana ile siku, na siwezi kuisahau maishani.

Kila siku niliyokuwa nakosa kwenda mazoezini na kwenye mechi nilikumbuka ni kwa sababu viatu vya kuchezea mpira na vitu vingine vyote ninavyotaka kwenye maisha ni gharama. Ingawa nikawa nawaza, kama hivi vitu ni gharama kwanini wazazi wengine waliweza kuwanunulia watoto wao?

Miaka kadhaa ikapita na nikafika chuo, hela ya kujikimu tuliyokuwa tunapewa ilikuwa inanitosha kununua viatu pea mbili vya kuchezea mpira kila baada ya miezi sita. Sikumbuki muda wowote ambao nilijisikia kuwa ni gharama kama mama alivyokuwa anasema.

Nilipomaliza chuo na kupata kazi nakumbuka nilikuwa na pea zaidi ya tano za viatu vya kuchezea mpira. Na sikuwahi kukumbuka kuwa viatu vya mpira ni gharama. Ila kuna siku moja nilikuwa nazunguka Mlimani city kwenye maduka, nikaona duka jipya la vifaa vya michezo limefunguliwa.

Nikaingia na kwenda moja kwa moja kwenye viatu, nikauliza bei na jibu nililopewa kwa mara ya kwanza nilielewa kwanini mama yangu alikuwa anasema viatu vya kuchezea mpira ni gharama. Gharama ya viatu pea moja kwenye lile duka ilikuwa ni sawa na pango la miezi mitatu ya nyumba niliyopanga pale sinza.

Nikawa sivioni viatu tena, namuona mwenye nyumba akiniangalia. Nikatamani kumpigia simu mama na nimuombe msamaha kwa usumbufu niliokuwa nampa. Wakati mama anakataa kuninunulia viatu sio kwamba shida ilikuwa ni bei, shida ni kwamba kwa uwezo wake na bajeti yake alikuwa hawezi kununua.

Alikuwa akifikiria gharama za ada, sare za shule, chakula, nauli, madaftari na vitabu anaona kuongeza viatu vya mpira haiwezekani. Uwezo aliokuwa nao ndo ulimfanya aone viatu vya mpira ni gharama.

Wakati nimeanza kupokea fedha ya kujikimu chuo kikuu, nilikuwa sina majukumu mengine hivyo nilikuwa na bajeti ya kutosha kununua viatu pea hata mbili mtumbani. Nilivyopata kazi na mshahara kuongezeka, uwezo wa kununua hata pea tano ulikuwepo.

Lakini uwezo wa kununua pea tano viatu vya mtumbani ulikuwa haufiki kununua hata pea moja pale Mlimani city. Nilikuwa sioni tena viatu, naona namna ile hela ingetumika vizuri kama pango la nyumba.

Nilitoka pale dukani na kuachana na vile viatu. Nikaendelea na maisha yangu ya viatu vya mtumba kwa sababu uwezo ulikuwa unaruhusu. Sikufikiria tena kwa undani kuhusu swala la vitu kuwa vya gharama au mimi kutokuwa na uwezo wa kuvimudu.

Mungu alitafuta njia nyingine nzuri ya kunikumbusha. Miaka kadhaa mbele niliweka akiba ya dola za kimarekani elfu tatu ili kwenda hotel ya nyota tano ya Gran Melia Zanzibar kusheherekea sikukuu ya kuzaliwa ya mpenzi wangu.

Kwangu mimi ile ilikuwa ni gharama kubwa zaidi kuwahi kuipitia kwa ajili ya kulala hotelini kwa siku mbili. Na nikajiambia tutajifunza mengi kwa kuwa mazingira yale.Siku ya pili nikiwa ninatoka chumbani kwangu nikamuona jamaa mmoja mzungu, kijana, kavaa shati na kofia yenye bendera ya marekani akitokea kwenye vyumba vya gharama zaidi.

Na hakuwa peke yake, alikuwa na familia yake jumla wapo wanne. Nikajikaza na kuondoa aibu na kumuuliza “ Kaka, mmelipia shilingi ngapi na mnakaa kwa siku ngapi kwenye hivyo vyumba?”. Akacheka sana kisha akasema “ Zanzibar hoteli ni bei rahisi sana, hauwezi kuamini hapa tunalipa dola elfu tisa kwa siku na tunakaa kwa wiki mbili, ni tofauti na Monaco, kule tulilipa dola elfu ishirini kwa siku.”

Nikabaki mdomo wazi, swali liliofuata ni anafanya kazi gani kuweza kuona dola elfu tisa kwa siku na kulipia wiki mbili sio gharama. Akaniambia biashara yake na nikamuaga aendelee kufurahia maisha.

Usiku kucha nikawa nawaza, ningemwambia mama nimekuja sehemu na nimelipa dola elfu tatu angesema ni gharama sana. Lakini ningemwabia kuna mtu amelipa dola elfu tisa ambayo hata mimi naona ni gharama zaidi angecheka. Ila angeshangaa ningemwabia mtu huyo anasema hiyo ni bei rahisi sana.

Hapa ndio nilikaa na kutafakari kwa undani uhalisia wa maisha. Vitu vyenyewe huwa havina sifa ya kuwa na gharama kubwa au ndogo. Swala linakuwa ni nani anauliza bei na yupo kwenye hatua gani kwenye maisha yake.

Kwa mama ambaye ana watoto wanne anawalea peke yake kununua sare ya shule ya ziada na viatu vya kuchezea mpira wa miguu ni gharama sana. Lakini kwa kijana ambaye ana mshahara mzuri baada ya kutoka chuo viatu vya mpira na suti pea mbili haikuwa gharama.

Kwa kijana ambaye ameanza maisha ya kujitegemea maeneo ya Sinza, kununua kiatu cha mpira chenye bei sawa na pango la miezi mitatu ni gharama kubwa sana. Lakini kwa mzee ambaye ana biashara za maana na nyumba zake nyingi ni kitu kidogo.

Kwa kijana ambaye najitafuta kutoa dola elfu tatu kwa ajili ya hoteli kwa siku mbili ni gharama kubwa sana. Ila kwa mmarekani mwenye makampuni ya uwekezaji na aningiza hela nyingi kwa dola basi kulipia dola elfu tisa kwa siku na kukaa wiki mbili ni kawaida.

Maisha ndo yapo hivyo, ukiona kuna biashara na vitu au huduma ni gharama kubwa kwako haimaanishi na watu wengine ipo hivyo. Kwa wengine bado wanaona hiyo ni bei nafuu zaidi na watakimbilia.

Mimi usiku ule nilijifunza kuwa kila nikiona mtu analipia huduma au bidhaa ya gharama nijiulize anafanya kitu gani cha utofauti na mimi kumuwezesha yeye kufanya vile. Pili ilinihamasisha kujipeleka sehemu nyingi zaidi ambavyo kwangu naona vitu ni vya gharama ili nikutane na hao watu na niulize maswali mengi zaidi.

Sasa hivi nikiona kitu ni cha gharama sana huwa najikumbusha kuwa ni cha gharama kwangu na sio kila mtu. Kama ambavyo viatu vya mpira wa miguu vilikuwa ni gharama kwa mama yangu lakini wazazi wa watoto wengine walikuwa wanawanunulia kila vikiisha.

Uchaguzi ni wako, kuendelea kuona vitu ni vya gharama au kuanza kuuliza watu wanawezaje kununua.

Uwe na furaha,

Uwe na afya,

Uwe huru na matatizo,

Upate amani

Kama umejifunza kitu mtumie mtu mmoja unayemjali.

#iThinkSo

Rogers Katuma

Financial Artist, Senior Adventurer, Occasional Storyteller and an Amateur Golfer


Discover more from iThinkSoo

Subscribe to get the latest posts sent to your email.