Unalipwa Kwa Thamani Unayo Tengeneza, Sio Muda Unaotumia Kufanya Kazi

Kulikuwa na meli moja kubwa na ya zamani sana ilipata hitilafu za kiufundi karibu kabisa na bandari. Wamiliki walihangaika sana na mafundi wao kuitengeneza. Wakaanza kuleta mafundi wengine wengi zaidi kutatua tatizo bila mafanikio.

Mafundi hawa walikuwa na ujuzi mkubwa sana kutoka kwenye vyuo vya ufundi ndani na nje ya nchi. Wiki kadhaa zikapita na matumaini yakazidi kupotea bila mafanikio ya kutengeneza meli yao. Kuna wenyeji wakashauri wamtafute mzee mmoja nje ya mji anaweza kuwasaidia.

Mzee alikuja na vifaa vichache sana ukishindanisha na mafundi waliotangulia. Alikuwa amevaa nguo za kawaida na hana muonekano unaomfanya mtu yeyote amchukulie kwa umakini kuwa ni fundi wa maana. Alionekana kama kituko.

Alivyofika akazunguka ndani ya ile meli bila kuuliza chochote. Baada ya hapo akaomba kapteni wa meli aje amuelezee kwa undani historia ya ile meli. Akauliza maswali mengi sana mpaka wamiliki wakaona kama mzee ni msumbufu kwa sababu hajui anachokifanya.

Mwishoni akauliza kabla ya meli kusumbua nini kilikuwa kitu cha mwisho kapteni alisikia, aliona au kama kuna harufu. Akauliza matatizo matatu ya mwisho ambayo meli ilipitia na waliyojaribu kutafuta ufumbuzi. Walivyomjibu, akaomba apewe masaa kadhaa kukagua na kujiridhisha tatizo ni nini.

Wakamuacha peke yake huku wakijadiliana namna ya kutafuta fundi mwingine maana huyu hawakuwa na imani naye. Mzee alipotea kwenye chumba cha injini masaa kadhaa. Na kama alivyo ahidi, akarudi na kuomba kifaa kidogo tu kinunuliwe na aletewe.

Kifaa kilikuwa cha bei rahisi sana, wamiliki hawakulalamika wakampa ili wamalizane naye aondoke. Maana kilikuwa ni kitu kidogo sana kufanya meli kubwa kama ile ishindwe kuendelea na safari kwa wiki ingawa mafundi zaidi ya mia walijaribu kila kitu.

Mzee alivyoletewa kifaa chake, akapotea tena kwenye chumba cha injini. Alivyorudi baada ya masaa kadhaa akamwabia kapteni awashe meli na wajiandae na safari. Watu wote wakacheka sana, pamoja na wamiliki. Hawakuamini mzee kama yule katatua tatizo kubwa kama lile kwa masaa wakati wengine wameshindwa kwa wiki.

Kapteni akiwa hana imani, akaenda kuwasha meli, na ikawaka. Watu wote walipigwa na butwaa na kuanza kumuangalia yule mzee kama muujiza. Baada ya hapo wamiliki wakamuuliza mzee gharama zake za ufundi, na hapo ndipo walipopata mshtuko zaidi. Mzee aliomba malipo mara nne ya gharama ambayo mafundi wengine waliomba walipwe wakifanikisha ufundi.

Wamiliki wakachukia na wakajaribu kuanza kumwambia mzee kwanini wamlipe hela yote ile kwa kazi aliyoifanya kwa masaa, mzee akatabasamu na kuwajibu “ hamnilipi kwa muda niliotumia kufanya kazi yenu sasa hivi, mnanilipa kwa miaka niliyotumia kujifunza na kupata uzoefu wa kufanya kazi ya miezi iishe ndani ya masaa”.

Ingawa ilikuwa inawauma kutoa ile hela yote, wale wamiliki walimlipa mzee hela yake na akaondoka zake huku anatabasamu. Jim Rohn, aliyekuwa muandishi na mfanyabiashara nguli duniani aliwahi kusema “wakati unaanza maisha utatumia muda mwingi kufanya kazi ambayo mtu mwenye ujuzi na uzoefu ataifanya kwa urahisi na muda mchache. Kadri na wewe utakavyokuwa unaongeza ujuzi na uzoefu ndio namna utalipwa zaidi kwa kufanya kazi ya miezi ndani ya masaa”

Kwenye uchumi, kila kitu chenye thamani kuna bei yake. Na sheria ipo hivi, thamani inapozidi kuongezeka na bei ya kitu huongezeka pia. Ndio, inachukua muda kukamilisha kutoa huduma yenye thamani au bidhaa yenye thamani, lakini hakuna mtu anajali ilikuchukua muda gani kukamilisha kazi, utalipwa kutokana na thamani ya kazi yako.

Kama unafanya mauzo, hakuna mtu atakulipa kwa muda uliokuwa unamtafuta mteja, unakutana naye, una mshawishi anunue au kumsubiria. Utalipwa kutokana na mauzo uliyofanya, hakuna anayejali mteja alichukua mwaka au mwezi kununua.

Na hiyo ndio sababu kwenye kampuni moja, wafanya usafi wanafanya kazi masaa kumi na mbili kwa siku, siku sita za wiki lakini wanalipwa mshahara mdogo sana ukilinganisha na wakurugenzi ambao wanafanya kazi masaa nane kwa siku, siku tano kwa wiki. Sababu ni rahisi, wakurugenzi wanaleta thamani kubwa zaidi kwenye kampuni kushinda wafanya usafi.

Mara ngapi umesikia wasanii wakubwa au wanamichezo maarufu wakilipwa mabilioni ya fedha kwa kazi ya siku au wiki ambayo asilimia kubwa ya jamii haiwezi kufikia malipo hayo kwa maisha yao yote ya kufanya kazi. Sababu ni rahisi, wasanii hao na wanamichezo wanatengeneza thamani kubwa kwa muda mchache kushinda asilimia kubwa ya watu wanayo tengeneza maisha yao yote.

Uzuri wa thamani upo hivi, haijalishi thamani yako ni ipi sasa hivi, una uwezo wa kuongeza thamani kadri siku zinavyokwenda. Jifunze vitu tofauti, tafuta utofauti wa ufanyaji kazi wako, badilisha mazingira, tumia teknolojia mpya na omba ushauri kwa waliokuzidi kila siku na thamani yako itaongezeka.

Acha kuumiza kichwa namna gani ya kufanya kazi masaa mengi zaidi ili ulipwe zaidi, anza kujiuliza ni namna gani ya kuongeza thamani yako ili uweze kulipwa zaidi kwa kazi ya muda mchache sana kama yule mzee.

Siku nyingine ukiona mtu amelipwa zaidi yako kwenye kazi mliyofanya, usilalamike kuwa watu wanapendeleana, jiulize umetengeneza thamani kama yeye? Muhimu zaidi jiulize una thamani ya kulipwa hicho unachokitaka?

Ukumbusho, watu hawalipwi kwa muda wanaotumia kufanya kazi, wanalipwa kutokana na thamani wanayo itengeneza wakifanya kazi.

Uwe na furaha,

Uwe na afya,

Uwe huru na matatizo,

Upate amani

Kama umejifunza kitu, mtumie mtu mmoja unayemjali

#iThinkSo

Rogers Katuma

Financial Artist, Senior Adventurer, Occasional Storyteller and an Amateur Golfer


Discover more from iThinkSoo

Subscribe to get the latest posts sent to your email.