Niliacha kazi yangu kwenye kampuni ya PwC Tanzania miaka kumi iliyopita. Sikuwahi kufikiria ni muda kiasi gani umepita tangu niache kazi na kujaribu maisha mtaani. Wiki iliyopita nilipata muda wa kutembelea kwenye mtandao wa Instagram na kuona ukurasa wa mtu mmoja ambaye nilianza naye kazi na yeye akabaki.
Kwenye ukurasa wake aliweka kila aina ya mafanikio, sasa hivi ana fanya kazi benki moja kubwa sana nchini akiwa kama mkurugenzi. Pia kuna biashara kubwa sana ameweka kuwa anafanya. Nikaangalia wengine pia nao walikuwa hivyo hivyo. Watu wapo kwenye nafasi kubwa za maisha, biashara nzuri, wamejiendeleza kielimu na hata kifamilia. Mimi nikajiona kama sijapiga hatua yeyote ya maana kwenye maisha tangu niache kazi.
Nikaona nitoke Instagram na kuingia WhatsApp, kwenye status nikamuona rafiki yangu mmoja ambaye tunalingana umri ameposti picha za watoto wake wanne. Nikajibu kwenye status yake, “hongera, una watoto wazuri sana”. Nilikuwa ile meseji huku nikijisikia unyonge, mimi sina hata mtoto wa kusingiziwa nikajiona bado sana.
Jana asubuhi nikashtushwa na meseji ya kwanza kuingia kwenye simu yangu, ilikuwa ni kutoka kwa yule rafiki yangu ambaye nilitoka kuangalia instagram yake wiki iliyopita. Alijua kuwa niliangalia akaunti yake, hivyo akaona anitafute.
“Kaka kwema, kitambo sana. Tunaweza kukutana kama upo free? Ninahitaji ushauri wako kwenye biashara yangu maana inasuasua sana. Napata changamoto kazi na biashara, wewe upo mtaani kitambo utakuwa una njia.”
Nilishtuka sana, maana nilivyoangalia akaunti yake binafsi na ya biashara yake sikuona kama ana changamoto yeyote ile. Nikasema jioni nitamjibu ili nijue zaidi pengine kuna kitu nitajifunza. Ilipofika jioni nikapata meseji nyingine ya yule rafiki yangu niliyemwambia ana watoto wazuri sana.
Alijibu akisema, “ ahsante, lakini mambo sio mazuri kabisa. Mwanangu mkubwa amelazwa hospitali mwezi wa nane huu. Anateseka sana na familia nzima haina amani wala furaha. Na shemeji yako tumegombana, hatupo pamoja.”
Nikashtuka sana kwa sababu picha alizoweka kwenye WhatsApp status ilionyesha kila mtu kwenye familia ana afya, furaha na upendo. Usiku ule nikatumia muda mwingi sana kufikiria kuhusu maisha yangu na maisha ya rafiki zangu wale wawili.
Kwenye hekaheka zangu za kufikiria nikakumbuka somo kubwa sana nililojifunza wakati nakaa kwa bibi yangu. Bibi yangu alikuwa anafuga wanyama mbalimbali kama mbuzi, kuku, bata na sungura wakati wa uhai wake.
Kwa wanyama wote aliokuwa anawafuga, bata walikuwa wanaongoza kwa kunikera. Bata ni wachafu sana, wanakula muda wote, wavivu na wasumbufu wakiwa wamefunguliwa. Ila kwa wanyama wote ambao bibi alikuwa nao, ni hao bata walinifundisha somo kubwa sana kuhusu maisha.
Uwezo mkubwa sana ambao bata wanao ni kuogelea. Na tofauti na wanyama wengi sana, ni ngumu kuona namna bata anavyoogelea kwa sababu kuu mbili. Kwanza akiwa kwenye maji sehemu ya juu ambayo inaonekana kwa watu inakuwa imetulia sana. Hautaona kichwa wala mwili wake ukiteseka kwenye kupiga kasia kama binadamu.
Pili miguu ya bata huwa inafanya kazi kubwa sana kupiga kasia kwa chini wakati anaogelea, lakini haionekani wala haifanyi sehemu ya juu ya mwili kuhangaika. Ukitafuta video moja ya bata akiogelea utahisi ni vitu viwili tofauti vinaogelea.
Na haijaliishi bata anaogelea kwenye maji gani, yaliyotulia au yenye mkondo mkali na yanaenda kwa kasi, hamna tofauti. Sehemu ya juu ya mwili inakuwa imetulia sana lakini miguu inafanya kazi kubwa sana.
Binadamu nasi tumechukua hii tabia ya bata kwenye maisha yetu. Kwenye mitandao ya jamii tunaonekana tumetulia sana, tumefanikiwa, tuna marafiki wengi, tunafuraha na afya bora kabisa. Lakini kwenye maisha halisi mambo ni kama miguu ya bata ikipiga kasia kwa nguvu zote bata asizame.
Rafiki yangu mkurugenzi amefanikiwa sana kuonyesha kwetu kwamba mambo mazuri kazini na biashara yake ni nzuri sana. Lakini alivyonitafuta haraka sana akaomba msaada kwa sababu biashara ipo hatiani kuzama.
Rafiki yangu wa pili alikuwa kila siku anaposti familia yake ya watoto wanne ina furaha na upendo. Kumbe mtoto mmoja yupo hospitali mwezi wa nane sasa hivi na mume wake wametengana baada ya ugomvi.
Kwenye maisha usione watu wana onyesha furaha na mafanikio ukahisi unachokiona ndio cha kweli. Kila mtu unayemuona huku nje ana pitia matatizo ambayo usingependa kuwa kwenye nafasi yake kama ungepewa nafasi ya kubadilishana maisha.
Mimi ambaye hawa marafiki zangu walikuwa wananielezea shida zao wakati huo pia nilikuwa napitia changamoto zangu za kutosha tu muda ule. Nimeacha kazi miaka kumi iliyopita lakini haimaniishi biashara na kila kitu kinaenda kama nilivyotarajia. Binadamu wote tunapitia shida.
Ukiona nimeweka kitu chochote cha maisha yangu haimaanishi sina matatizo au changamoto. Na mimi kama bata tu, najitahidi kuwa mtulivu nje lakini ndani changamoto za kupiga kasia nisizame zinaendelea sana tu.
Na hiyo ipo kwa kila mtu, Raisi wa nchi, wazazi wako, mabosi zako, viongozi wako wa dini na hata wasanii wako pendwa wanoingiza hela kwa kuigiza au kuimba shida zao na za watu. Usijisikie vibaya kuona sehemu ya juu ya watu imetulia, wewe jua tu sehemu ya chini moto unawaka huko.
Uwe na furaha,
Uwe na afya,
Uwe huru na matatizo
Upate amani
Kama kuna kitu umejifunza, mtumie mtu mmoja unayemjali.
#iThinkSo
Rogers Katuma
Financial Artist, Senior Adventurer, Occasional Storyteller and an Amateur Golfer
