Ukiachana na familia, sijawahi kuona mtu aliyekuwa kwenye mahusiano ya uhakika wakati nakua. Nilikuwa na marafiki ambao hawakuwa na uwezo wa kuwa na mwanamke mmoja, wanabadilisha wanawake kila wiki au mwezi. Wakati nipo darasa la tano nilikuwa na rafiki yangu mmoja ambaye alikuwa na mahusiano ya uhakika.
Huyu rafiki yangu aliyafanya mahusiano yake yaonekane marahisi sana. Walikuwa na furaha muda wote na walikuwa poa kila wakati. Na mimi nikaamini kuwa mahusiano ni kitu chepesi sana. Sikuwa na haraka ya kutafuta mahausiano lakini nilikuwa nina imani ni kitu kimoja chepesi sana.
Mara yangu ya kwanza nikaonja mahusiano ni mwaka wa kwanza chuo. Nilikuwa na rafiki wa kike tulikuwa tunatumia muda mwingi sana pamoja. Hatukuwahi kuzungumza kuhusu kuwa kwenye mahusiano lakini tulikuwa tunafanya karibu kila kitu ambacho watu kwenye mahusiano hufanya.
Nikifikiria vizuri sasa hivi nagundua kuwa yeye alijua tupo kwenye mahusiano lakini mimi nilihisi ni marafiki tu wa faida. Na sikufanya makusudi, ni kwa sababu nilikuwa sijui mahusiano ni nini. Mimi nilikuwa nafurahi kuwa naye karibu muda mwingi, kupeana zawadi, kuongea vitu vya siri na ndani vya kwetu na watu.
Lakini sikuwa tayari kwenye vitu vingine kama kukatazwa kuongea na wanawake wengine, kutoa taarifa nilipo na ninachofanya kila saa kwake. Sikuwa tayari kuwa karibu na marafiki zake, kuonekana tupo pamoja kama wapenzi darasani na vingine vingi.
Yeye alikuwa anataka tuangalie muvi za kikorea mimi nilikuwa nataka kuangalia muvi za kupigana. Jioni yeye alikuwa anataka kwenda Mlimani city kutembea mimi nilikuwa nataka kwenda uwanjani kucheza mpira. Mimi nilikuwa nafurahi wanawake wengine wakinikumbatia lakini nilikuwa sitaki wanaume wamkumbatie yeye.
Mara akaanza kuwa na mawazo ya familia, kuuliza kuhusu watoto na ndoa wakati mimi ndio kwanza nilikuwa nafikiria namna ya kuanzisha biashara na kuacha chuo maana sikielewi na ndo kwanza tupo mwaka wa kwanza.
Nikagundua kuwa mahusiano ni magumu sana. Mimi nikiwa najitafuta kujitambua mwenzangu ana malengo yanayohusu mimi na yeye. Nikaanza kujiuliza kama mapenzi magumu hivi na sasa hivi nimefika chuo hivi yule rafiki yangu aliyekuwa kwenye mapenzi darasa la tano alikuwaje?
Baada ya migogoro mingi sana kwenye mahusiano yangu ya kwanza, ikabidi niyavunje kabla sijachanganyikiwa. Nikampigia rafiki yangu kumuomba ushauri alikuwa anafanyaje kipindi kile cha darasa la tano kufanya mahusiano yake yawe mepesi sana.
Akacheka sana, kisha akaniambia “kaka hamnaga mapenzi mapesi, mimi matokeo yangu ya shule yalianza kuwa mabovu nilipoingia kwenye mahusiano. Nimepoteza muda mwingi sana, hela nyingi sana kwa kujaribu kupambania mahusiano yale. Na bado tulipofika darasa la saba aliniacha.”
Sikumuamini alichokuwa anakisema, kwa watu wote tuliosoma naye tulimaliza shule tukiamini wale ni wapenzi ambao wamepangwa na Mungu. Na mapenzi yao yalikuwa yanaonekana yana furaha, amani, upendo na uaminifu. Na zaidi walionyesha kuwa mahusiano ni kitu rahisi sana.
Akaendelea kusema, “nimeshawahi kumkamata akiwa na wanaume wengine mara tatu, na nikamsamehe kwa sababu sikuwa tayari kuwa peke yangu. Nimeshafunga safari nyingi sana kwenda kwao kumtembelea na akanifungulia mbwa baada ya kuachana, hamna mapenzi rahisi kaka”
Nikakumbuka msemo mmoja maarufu sana unasema, “kila kitu kwenye maisha kinaonekana chepesi pale tu kinapokuwa kinafanywa na mtu mwingine, na sio wewe.” Utamuona msanii anaandika nyimbo, utasema ni kazi rahisi sana, mpaka utakapojaribu.
Utamuona mtu anacheza mpira wa miguu na kuwapiga watu kanzu na tobo, utaona ni rahisi sana mpaka pale utakapo jaribu. Utaona mtu anafanya biashara na inakuwa, wateja wengi na utaona rahisi sana mpaka pale utakapofungua biashara yako.
Mimi niliona mapenzi rahisi kwa rafiki yangu mpaka pale nilipojikuta kwenye mahusiano ya kwanza na yakanishinda, haikuchukua zaidi ya miezi minne, bora rafiki yangu alikaa miaka miwili kabla ya kufunguliwa mbwa.
Najua na wewe kuna vitu unaviona rahisi sana kwa sababu haujajaribu. Una maamuzi mawili, kujaribu na uone ugumu wake ili ujifunze au kuheshimu wanaofanya na kuwaomba ushauri na kufuata maelekezo yao.
Mimi sikuhizi kila nikimuona mtu anafanya kitu sikijui au sijawahi kujaribu namuheshimu. Nikiona mtu anatembeza mchicha kwenye jua kali, nampa heshima yake kwa sababu kuna kitu cha kujifunza.
Nikimuona mtu amejiajiri na hajakata tamaa nampa heshima yake. Nikiona mtu ameajiriwa na amepanda cheo nampa heshima yake. Kwa sababu najua hamna kitu chepesi duniani. Vitu vyote vyepesi ni vile ambavyo wewe haujajaribu.
Uwe na furaha
Uwe na afya
Uwe huru kutoka kwenye matatizo
Uwe na amani
Kama umejifunza kitu mtumie mtu mmoja unayemjali
#iThinkSo
Rogers Katuma
Financial Artist, Senior Adventurer, Occasional Storyteller and an Amateur Golfer
