Nilipojiunga chuo kikuu cha Dar es Saalam, nikaanza kupata hamasa ya kupenda magari. Na upendo ulikuwa zaidi kwenye magari ya chini yenye uwezo mkubwa wa kukimbia na injini za kelele sana. Gari yangu ya kwanza niliyoiweka kwenye ndoto ikawa ni Toyota Celica. Niliweka picha zake nyingi sana ukutani, nikalipa na jina, Prince Awesome.
Nilipofanikiwa kununua gari hilo baada tu ya kumaliza chuo ilikuwa wakati wangu bora zaidi kwenye maisha. Gari lilinipa mzuka wa kama naendesha Ferrari, ambayo ilikuwa ni gari ya kifahari na ya mamia ya mamilioni ya bei. Wakati gari yangu ilikuwa bei ndogo sana.
Watu walikuwa wanasimama na kuniulizia kuhusu gari yangu. Polisi wa barabarani walikuwa wanasimamisha gari kuuliza tu nimelipataje, linaitwaje na kuomba kuangalia ndani. Nilikuwa naishi ndoto yangu na kuhamasisha watu wengi zaidi kutengeneza ndoto zao kupitia gari yangu.
Nakumbuka nilikuwa naliosha gari langu asubuhi na jioni. Nilikuwa nafanya matengenezo kwa haraka na kuchunguza kila kitu. Niliamini inabidi nilitunze gari yangu ili initunze pia. Kwenye barabara mbovu nilikuwa naendesha kama nimebeba mgonjwa, taratibu sana.
Uhalisia ni kwamba kila kitu huanza kuchoka na kupata changamoto, kuanzia binadamu mpaka vitu. Na gari yangu haikuwa na utofauti, miaka michache mbele ikaanza kusumbua, ingawa niliijali na kuitunza sana.
Ilianza taratibu kwa kuchelewa kuwaka kipindi cha asubuhi, baadaye ikawa tairi zinaisha upepo bila sababu mara ikawa inatetemeka sana ukiendesha muda mrefu. Tatizo kubwa zaidi ambalo lilikuwa linakera ni betri ilipoanza kuchoka.
Kwanza ikawa inachelewa kuwaka kwasababu betri haina nguvu. Baadaye ikawa kuna siku haiwaki mpaka nichaji betri au mtu ashtue betri yangu kwa kutumia betri ya gari yake. Na kwasababu ilikuwa haitabiriki basi ilikuwa inaumiza sana.
Nilivumilia matatizo haya yote kwasababu nilikuwa naipenda na kuijali sana gari yangu, lakiji kuna siku ilinifanyia tukio ambalo nililaani sana. Nilijuta kuwa na lile gari. Siku hii ilikuwa muhimu sana, sio kwangu bali kwa mdogo wangu ambaye alikuwa anasoma shule ya bweni, ilikuwa ni siku yao ya kutembelewa. Aliniomba niende kumtembelea miezi nyuma kabla, sikutaka kumuangusha
Mara nyingi nilikuwa nafanya kazi mpaka siku ya jumamosi, na nilikuwa mpenzi mkubwa sana wa suti. Siku hii nilikuwa na suti yangu pendwa ya bluu, na gari yangu nyekundu, nilikuwa nahisi nipo juu ya dunia yangu mwenyewe.
Nilichelewa kutoka ofisini kufika shuleni kwa mdogo wangu, muda nafika pale sehemu zote za kuegesha magari karibu na shule zilikuwa zimejaa maana wazazi wengi waliwahi na wengine walipaki vibaya.
Hivyo ikanilazimu kuegesha gari sehemu ya mbali kidogo na shule. Ilikuwa changamoto kwasababu umbali wa kutembea mpaka kufika shuleni, jua kali, barabara ya vumbi na suti yangu ya bluu vilinitoa kwenye furaha kidogo. Lakini nilikubali kufanya hivyo kwa upendo wa mdogo wangu.
Nilifika shuleni na mdogo wangu alifurahi sana, wakati huo kichwani kwangu nawaza namna ya kuwahi kuondoka kabla wazazi wengine hawajatoka na kutengeneza foleni kubwa au kwenda kuniziba kabisa nilipo egesha gari. Pia nlikuwa nataka kuwahi kula kipupwe cha kwenye gari, joto lilikuwa kali sana.
Nlipomaliza tu kuongea naye na kusalimia walimu nikatembea haraka sana kuwahi kwenye gari, kumbe nlikuwa nakimbilia matatizo. Nlifungua mlango kwa haraka na kukaa kwenye siti, kisha kufunga mlango na kuingiza funguo kwenye sehemu yankuwashia gari, haikuwaka.
Niliishiwa nguvu sana, kichwani nikasema leo sio siku na sehemu sahihi kabisa ya gari yangu pendwa kunifanyia hivi. Nikajaribu tena mara tatu, betri ilikuwa imeisha kabisa kiasi hakuna mlio wowote uliotoka. Sikuwa na nguvu ya kufanya kitu kingine chochote, nikaanza kutoka jasho, hasira zikaongezeka na nikatoka nje.
Nikampigia fundi wangu, nikamlalamikia sana kuhusu changamoto ile, kisha nikaacha funguo ya gari kwenye duka la karibu, nikanunua maji ya kunywa na kuondoka zangu. Nilijisikia kusalitiwa, kudhalilishwa na kuvunjiwa heshima na gari ambayo miaka kadhaa hapo nyuma ilikuwa ni ndoto yangu.
Kwa dakika kadhaa nilifikiria na kuamini kuwa kununua ile gari ilikuwa ni kosa kubwa sana ambalo nimeshawahi kufanya kwenye maisha yangu. Nililaani kila mtu na kila kitu kwenye maisha yangu. Nikaanza kutafuta usafiri, nilvyoona watu wanagombea daladala haraka nikachukua bajaji na kurudi nyumbani.
Wakati nipo kwenye bajaji, na kuona namna watu walivyobanana kwenye daladala nikaanza kupatia picha maisha yangu yangekuwaje miaka mitano yote hii ningekuwa napanda daladala na sina ile gari yangu. Kwanza siku kama ya leo nisingeweza kuvaa suti, tena ya bluu.
Nisingekuwa na lile gari nisingeweza kwenda safari za mbali na mpenzi wangu ambazo zilitufanya tuwe karibu zaidi. Nisingeweza kuwa na mizunguko ya usiku kazini na kwenye ujasiriamali wangu. Nisingeweza kukutana na watu wengi sana wa maana ambao mazungumzo ya kwanza yalianzia kwenye gari.
Nikakumbuka pia gari ni kama vitu vingine, baada ya muda huchoka na kuanza kuwa na matatizo. Binadamu ambaye ameumbwa na Mungu huwa na matatizo, kuna siku anaamka mchovu, kuna siku ana hasira, kuna siku anaumwa na kuna siku anafariki kwahiyo gari sio ajabu sana.
Hasira zikakata na nikaanza kuwa na shukrani zaidi kwa gari yangu ya ndoto, na pia nilijua fundi wangu atatengeneza na kuirudisha nyumbani salama kabisa. Mawazo yakaenda mbali zaidi ni namna gani binadamu huwa tunatabia ya kulaani vitu pekee ambavyo tunavyo.
Wazazi wetu watatukwaza kuhusu vitu fulani au walikosea wakati wanatulea, tutatumia maisha yetu yote kulaani na kulalamika kuhusu makosa yao, upungufu wao na namna wamesababisha vitu vibaya kwenye maisha. Tunasahau walitupa zawadi ya uhai ambao ndio kitu pekee tulichonacho. Na tunawalalamikia wazazi hao hao ambao ndio pekee tuliokuwa nao.
Tunafanya kazi na kukutana na changamoto au bosi mkatili basi tunatumia muda wote kulalamika na kulaani kuhusu kazi yetu au bosi wakati kwa uhalisia ndio kazi pekee tuliyokuwa nayo. Na wengi unakuta hawana hata sifa nyingi za kupata kazi nyingine.
Mimi nilianza kulaani gari yangu kwa matatizo wakati ndio usafiri pekee niliokuwa nao, sikuwa na baiskeli, pikipiki wala chombo kikingine chochote cha usafiri. Nashukuru haikunichukua muda mwingi kujikamata mwenyewe nikiwa nalaani kitu pekee nilichokuwa nacho.
Watu wengi huwa hatupati muda wa kukaa na kufiria kuhusu vitu tunavyolalamika na kulaani. Kwasababu ya hasira na maumivu tunaona mabaya na madhaifu ya vitu tunavyovilaani, ingawa tukitulia tutagundua kuna mazuri mengi zaidi yametokana na kitu tunacholaani. Na pia haina maana kulaani kitu ambacho ndio pekee, hauna uwezo wa kukiacha au kukibadilisha kwa muda huo.
Mbeleni, ukjikuta upo kwenye mazingira ambayo unalaani kitu au mtu kwasababu yeyote ile jiulize yafuatayo:
- Una kitu kingine au mtu mwingine bora zaidi ya unachokilalamikia au mlalamikia?
- Kitu unachokilalamikia au mtu unayemlalamikia haijawahi kutokea kukupatia zaidi ya ulichokuwa unataka muda fulani huko nyuma?
- Kuna mtu yeyote ameshawahi kukwambia kwamba kuna kitu kikamilifu duniani ambacho hakiaribiki, hakisumbui, hakichoki na hakiishi au ni mtu mkamilifu ambaye haumwi, hachoki, haumii, hana matatizo na kila siku atakuwa mtiifu na mnyenyekevu kwako tu?
Kama kuna jibu la hapana kwenye maswali hapo juu, acha kulaani vitu na watu pekee ambao unao.
Uwe na furaha.
Uwe na afya.
Uwe huru kutoka kwenye matatizo
Uwe na amani.
Kama umejifunza kitu, mtumie mtu mmoja unayempenda.
#iThinkSo
Rogers Katuma
Financial Artist, Senior Adventurer, Occasional Storyteller and an Amateur Golfer
