Njia Ya Kupata Furaha Sio Kwa Kuongeza Vitu

Shule ya msingi mtakatifu Joseph ilikuwa ni miongoni mwa shule za kwanza Tanzania kufundisha kwa mtaala wa kiingereza. Ilikuwa inaendeshwa na masista wa kanisa katoliki Tanzania. Na sifa moja bora waliyokuwa nayo ni sare zao za shule. Rangi ya kaki kwenye bukta na sketi na masweta ya bluu au kijani. Kipindi ambacho shule nyingi walikuwa wanavaa bukta na sketi za bluu.

Uongozi wa shule ulikuwa unashauri wanafunzi wawe na angalau pea tatu za sare ya shule kwa ajili ya usafi na matumizi ya muda mrefu zaidi. Lakini hawakuweka hiyo kama lazima kuzuia sisi wanyonge tusiokuwa na uwezo wa kuwa na pea tatu za sare.

Mwanzoni mwa mwaka nilikuwa na sare pea mbili, lakini kadri miaka ilivyokuwa inaenda nikajikuta nina sare moja ya maana ya kuvaa. Nyingine ilikuwa imechoka sana au imechanika na ilikuwa aibu kuivaa mbele za watu. Kwa maisha niliyokuwa nayo sikuwa na cha kufanya zaidi ya uvumilivu.

Nilikuwa najipa moyo kuwa kile ni kipindi cha mpito, niliamini nitakuwa na furaha zaidi kwenye maisha nikiwa na uwezo wa kununua nguo nyingi kadri ya ninavyotaka. Kwa kipindi hiki nikawa navaa sare zangu asubuhi, nafua jioni ili zikauke usiku na kuzirudia, maarufu sana kama kauka nikuvae.

Nilikuwa naumia kwa hali hii, na nikahisi kuwa itaisha shule ya msingi, lakini haikuwa tofauti sana na nilipofika sekondari pia. Mama aliwekeza nguvu nyingi sana kwenye kununua vitabu, madaftari na hata kunipeleka tuisheni. Nikaendelea kutamani wenzangu wenye sare nyingi za shule na nguo nyingi za kuvaa kadri wanavyotaka. Niliamini nitakuwa na furaha zaidi nikipata nguo zaidi.

Mungu akasikiliza kilio changu, akanichagua mimi kuwa miongoni mwa wanafunzi waliopata mkopo wa elimu ya juu nilivyofika chuo kikuu. Mkopo huu ulikuwa unakuja na hela za ziada za matumizi ambazo zilinipa uwezo wa kununua nguo kidogo za kubadilisha.

Nikaanza kuwa na nguo nyingi za mitindo tofauti tofauti kwa kadri ya akiba niliyokuwa nabakiwa nayo. Ikafika kipindi nikawa nabadilisha nguo hata mara tatu kwa siku. Nilikuwa na nguo za asubuhi kwenye vipindi vya kwanza, narudi hosteli na kubadilisha kwa ajili ya semina halafu narudi tena kubadilisha kwa ajili ya michezo.

Ingawa nilikuwa kwenye nafasi ya kubadilisha nguo sasa hivi bado sikuwa na furaha ya kweli. Nikaamini kuwa nahitaji hela zaidi kuanza kununua nguo nzuri zaidi ambazo ni za bei ya juu. Kwa sasa nilikuwa na uwezo wa kubadilisha nguo mara tatu kwa siku wakati shule ya msingi na sekondari ilikuwa ni kauka nikuvae, lakini sikutosheka.

Nikaendelea kuomba Mungu anipe kazi ambayo ingekuwa na mshahara wa kuweza kununua nguo kila ninapotaka na za aina yeyote ninayotaka. Mungu akasikiliza maombi yangu na kuyatimiza. Nilipata kazi kabla sijamaliza chuo, na kabla ya kuanza kazi kampuni ikatupatia laki tatu ya kwenda kutafuta nguo za kuvaa ofisini, Mungu alifanya kazi yake.

Nakumbuka miaka yangu miwili kazini nilinunua suti za gharama nane, pea zaidi ya kumi za viatu, mashati na suruali hazihesabiki. Nilikuwa naishi maisha ya ndoto yangu. Nilikuwa nina uwezo wa kutorudia nguo moja hata kwa miezi miwili. Lakini kuna kitu kilikuwa kinakosekana, furaha ambayo nilitarajia itakuja kwa kuwa na nguo nyingi.

Uhalisia ni kuwa nilikuwa nikinunua nguo mpya, nina pata furaha ya muda mchache baada ya hapo inapotea na naanza kutafuta nguo nyingine tena. Na baada ya kuzunguka kwenye gurudumu hilo kwa muda nikaanza kujifunza maana ya furaha.

Furaha ya kweli haipatikani kwa kuongeza vitu. Hupatikana kwa kupenda na kufurahia kile ulichonacho. Hii ilikuwa ni kweli hata kwenye nguo ambazo nilikuwa ninanunua. Kuna nguo zilizokuwa zinanipa furaha kila nikivaa na nilikuwa nazirudia mara kwa Mara.

Nikagundua kuwa kama nitaweza kuwa na nguo kama hizo kwenye maisha yangu muda wote ninakuwa na furaha na nguo zangu. Nikaanza kuondoa nguo zote ambazo nilikuwa mvivu wa kuzivaa na kuacha zile zilizonipa furaha.

Nikaanza kununua nguo za aina ile ile, rangi ile ile na saizi ile Mara nyingi zaidi. Na furaha yangu ya nguo haijawahi kuondoka. Sina presha nikiona watu wanahangaika na fasheni mpya, mimi nafurahi na nilichokuwa nacho.

Nikagundua pia hiyo shida haijaishia kwenye nguo tu, kila kitu kwenye maisha nilikuwa nahisi nikiongeza au nikipata kipya nitakuwa na furaha zaidi. Nilihisi nikiwa na marafiki wengi zaidi nitakuwa na furaha zaidi. Nikiwa na simu mpya zaidi nitakuwa na furaha zaidi. Nikiwa kwenye mahusiano mengi zaidi ndio nitapata raha zaidi.

Sio mimi pekee niliyekuwa na huo mtazamo, nina imani hata wewe leo hii unahisi kuna kitu ukipata cha ziada, au watu fulani wakiwa karibu yako ndio furaha yako itakuja zaidi. Unahisi ukipata hela zaidi, magari zaidi na nyumba ndio utakuwa na furaha.

Uhalisia ni tofauti na hivyo, furaha ya kweli hupatikana hapo ulipo na hicho kidogo ulichonacho. Kama una rafiki wachache wanakuthamini na kukujali basi wafurahie hao, wakiongezeka watapoteza kitu kwako. Kama una simu ndogo au kubwa lakini inafanya kazi vizuri, furahia hiyo kwa sababu simu mpya unayoitaka nayo itapitwa na wakati baada ya muda fulani.

Kabla haujafikiria kuitafuta furaha kwa kuongeza kitu, jaribu kukipenda ulichonacho. Na ikitokea ulazima wa kubadilisha kitu kwenye maisha yako hakikisha unachagua kitu ambacho kitakaa muda mrefu, kina ubora na utakuwa unakifurahia kila ukiwa nacho.

Furaha ya kweli haipo kwenye kuongeza vitu.

Uwe na furaha.

Uwe na afya.

Uwe huru kutoka kwenye matatizo.

Upate amani

Kama umejifunza kitu, mtumie mtu mmoja unayemjali

#iThinkSo

Rogers Katuma

Financial Artist, Senior Adventurer, Occasional Storyteller and an Amateur Golfer


Discover more from iThinkSoo

Subscribe to get the latest posts sent to your email.