Baada ya kuanza kupata uelewa kuhusu mimi na kuanza kujifunza kutengeneza malengo, nimetengeneza zaidi ya malengo mia moja. Lengo la kwanza siku zote limekuwa kuwa tajiri na mali za kutosha. Sijawahi kuamini kuwa kuna kitu cha muhimu zaidi kwenye maisha zaidi ya hivyo, na nashukuru sijawahi kuumwa kwa miaka yangu yote ya kujitambua.
Sijawahi kulazwa hospitali kwa ugonjwa wowote ule, mara ya mwisho kuumwa ni kwa msongo wa mawazo wakati nashabikia mpira mwaka 2008 na Manchester United ilikuwa imefungwa goli nne na Liverpool.
Mara nyingi nilikuwa nikienda hospitali ni kwa ajili ya shida za utofauti na zinazochukua masaa machache na nyingi zilitokana na maumivu ya kwenye mpira au misuli na vidonda tu vya kawaida. Mara nyingi nilikuwa nikienda hospitali ni kutembelea ndugu, jamaa na marafiki wakiwa wanaumwa au kulazwa.
Hayo yote yalibadilika mwaka jana ambapo nilipata changamoto za kiafya. Ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kutumia muda mwingi zaidi hospitali, tena sio moja wala mara moja. Ilianza jioni moja wakati nimetoka kuoga na kuanza kupaka mafuta. Nikajigusa mgongoni na kuhisi kuna uvimbe ambao upo kwa ndani na sio wa kawaida.
Nikajaribu kujiangalia vizuri kwenye kioo, na nikaona kwa uzuri kabisa uvimbe. Haukuwa wa kawaida na nikaanza kupata hofu. Kama walivyo watu wengi kwenye kizazi hiki, kama kitu sikielewi naingia kwenye mitandao na kuanza kutafuta.
Majibu yote ya kwenye mitandao yakawa yanakuja na vitisho, kwamba inawezekana uvimbe wangu ni kwa sababu ya ugonjwa hatari zaidi duniani, kansa. Sikuweza kulala usiku ule, nilisubiri kukuche ili niwahi hospitali ya jirani.
Asubuhi ilipofika ilinikutia kwenye geti la hospitali. Nikaomba kufanya vipimo vya muhimu kwenye ule uvimbe, wakanipa na kuniambia nikae pembeni kusubiria majibu. Kwa kumbukumbu yangu, ule ulikuwa miongoni mwa muda wa kusubiri wa maumivu zaidi kwenye maisha yangu kama nilivyokuwa nasubiri Manchester United arudishe zile goli nne alizofungwa na Liverpool mwaka 2008.
Nilikuwa na hofu sana kwamba maisha yangu yatabadilika ikiwa nikagundulika nina kansa. Majibu yalipofika daktari alikuwa na tabasamu, ikanipa moyo kidogo. Akaniambia uvimbe ule ni wa kawaida, unaitwa lipoma. Ni mafuta yaliyoganda chini ya ngozi, na nikitaka kuutoa operesheni yake ni ya dakika chache kwa gharama nafuu.
Nikamshukuru daktari na kuondoka, nilipata amani ya moyo kidogo. Lakini siku chache baada ya kutoka hospitali hali yangu ikawa mbaya zaidi. Nikaanza kupata maumivu ya mgongo, baadaye maumivu ya kifua na tumbo. Ikawa ikifika usiku napata shida kupumua na mwili wote unauma nikilala.
Nikawa najipa moyo kuwa ni uchovu wa mazoezi na haitakuwa mbaya zaidi ya hii. Nilijidanganya, siku zilizofuata maumivu ya tumbo yakaongezeka mara dufu, sasa hivi nikawa nasikia kichefuchefu, natapika. Pia ikawa maumivu hayaishi hata baada ya kutumia sawa kali za maumivu. Nikaenda tena kwenye mitandao, na majibu yote yalionesha nitakuwa na kansa.
Nikajikaza kwa unyonge na hofu kwenda hospitali nyingine. Sasa hivi nikawaomba wachukue vipimo vyote ambavyo inawezekana kuchukuliwa kwenye mwili wa binadamu. Walichukua kila kipimo walichonacho hospitali. Nilipimwa damu, haja ndogo, kubwa, x-ray, ultra sound na vingine vingi. Nilipimwa tumbo, kifua, mgongo, moyo, shingo, mapafu mpaka maini.
Madaktari bingwa na wenye uzoefu walikaa na mimi kuniuliza kuhusu historia yangu ya maisha, familia, afya na kuomba maelezo ya undani kuhusu maumivu ninayoyasikia na vitu vinavyo nipa hofu kwenye maisha. Wakaniambia nisubiri masaa machache kwa ajili ya majibu.
Huu ndo muda ambao niliwaza vitu vingi sana kuhusu maisha yangu. Nikawaza ikiwa nina kansa, na madaktari wakaniambia nina muda mchache wa kuishi, nitabadilisha nini kwenye maisha yangu? Malengo yangu yatakuwa yaleyale ya kuwa tajiri au nitabadilisha? Ndugu, jamaa na marafiki wa aina gani nitataka kuwa nao karibu.
“Unaweza kumuona daktari akupe majibu,” sauti ya nesi ilinishtua kutoka kwenye mawazo yangu. Muda ule ndio nilielewa kwanini watu huwa wanakimbia majibu yao ya ukimwi wakienda kupima. Ni kwa sababu unahisi ni bora uishi kwa sintofahamu kuliko kujua kitu kitakachobadilisha maisha yako yote.
“Vipimo vyako vinaonyesha hauna shida kubwa sana, una bacteria wa H.Pylori ambao wanafanya uwe na dalili za vidonda vya tumbo. Na bacteria hao hufanya karibu kila sehemu ya mwili wako kuuma” Aliendelea kunielezea vitu vingine vingi zaidi ambavyo sikumbuki kwa sababu nikarudi kwenye mawazo yangu.
Nikapewa dawa nyingi sana siku ile kwa ajili ya vitu vyote ambavyo madaktari waliona vinahitaji kutibiwa. Pia wakashauri mfumo wa maisha wa kubadilisha kama vile chakula, vinywaji, kulala muda sahihi na pia kuwa na mtazamo chanya.
Nilivyofika nyumbani siku ile kitu cha kwanza nilichofanya ni kuchukua kitabu changu nilichokuwa naandika malengo yangu, nikafuta lile lengo la kwanza la kuwa tajiri mwenye mali nyingi na kubadilisha kwenda kuwa na afya njema.
Nilifanya hivyo kwa sababu muda wote nikiwa hospitalini sikuwaza chochote kuhusu mali, umaarufu, utajiri, marafiki wala familia. Niliwaza kitu kimoja tu, nisiwe na ugonjwa ambao utabadilisha maisha yangu. Nisiumwe kitu ambacho kitanifanya niwe hospitali muda mwingi.
Nikaandika kuwa ili niwe na afya njema nahitaji mazoezi zaidi, chakula chenye rutuba na kisichokuwa kimetengenezwa kiwandani, kupumzika na kwenda kufanya uchunguzi wa mara kwa mara kuhusu afya yangu.
Watu wengi tunachukulia kwa wepesi afya zetu kwa sababu hatujapitia changamoto kubwa ya kufanya vitu vingine vyote visiwe na maana kwenye maisha. Kama tulipitia vitu hivyo basi ilikuwa muda mrefu sana na tumeshasahau.
Ukiwa nzima ni rahisi kuwa na malengo mengi sana, unataka nyumba kali, gari kali, kusafiri na kutalii, kula bata na vingine vingi. Uhalisia ni kuwa hivi vyote haviwezi kutokea ukiwa unaumwa. Watu wote waliokuwa hospitali wana lengo moja tu, kupona na kurudi na afya njema.
Ni kweli kuna magonjwa hauwezi kuyazuia, inawezekana ya kurithi, Mungu alipanga au bahati mbaya tu. Lakini pia kuna matatizo mengi sana ya kiafya tunayapata kwa kutojali ushauri wa madaktari bingwa kuhusu afya. Umuhimu wa mazoezi, chakula asili, kulala muda sahihi, kuacha pombe kali, sigara na vingine vingi.
Mimi nashukuru kwa kupitia ile nikapata hamasa kubwa sana ya kubadilisha malengo ya maisha yangu na kuipa afya kipaumbele. Ile Hali niliyopitia kwa wiki chache ilinionyesha namna matatizo ya kiafya huaribu maisha ya mtu. Inaleta shida kifedha, mahusiano, ufanyaji kazi na hata kutoa uhai kwa mtu mwenye ndoto kubwa sana.
Sikuombei upitie changamoto za kiafya kama mimi ili uweze kupata hekima na hamasa ya kujali afya yako. Nakuombea uwe na busara ya kujifunza kwa watu waliokuzunguka. Patia picha u,kwa hospitali, umelazwa, na unapitia changamoto ya kiafya ambayo ungeweza kuizuia.
Jiulize muda huo ukiwa kitandani, malengo yako makubwa yatakuwa nini?
Hauhitaji kuumwa ili kupata mafunzo ya wagonjwa. Kama una afya njema basi una utajiri mkubwa sana tayari.
Uwe na furaha,
Uwe na afya,
Uwe huru kutoka kwenye matatizo,
Uwe na amani.
Kama umejifunza kitu mtumie mtu mmoja unayemjali.
#iThinkSo
Rogers Katuma
Financial Artist, Senior Adventurer, Occasional Storyteller and an Amateur Golfer
