Hautakuwa Na Mipango Mizuri Ukipata Pesa; Kuwa Na Mipango Mizuri Kwanza Ili Upate Pesa

Miongoni mwa muda niliopitia changamoto kubwa sana kwenye maisha ni wakati tulipopishana mawazo na malengo na rafiki zangu kwenye kuendesha kampuni ambayo niliianzisha.

Nilifungua kampuni nikiwa chuo kikuu, na nilikuwa na amini nitatumia maisha yangu yote kuijenga. Tulipopishana malengo na kuamua kujitoa, ilipoteza malengo yangu yote ya maisha. Sikuwa na mpango mwingine wowote.

Nikaacha kila kitu na kuchukua likizo fupi kutafakari kuhusu maisha yangu na mipango ya biashara nyingine. Nikapata wazo lingine na kuanza kuwa na furaha ya kujenga kitu kipya.

Sikuwa na haraka ya kuijenga kampuni mpya kwa presha, nikataka kujifunza kwenye makosa niliyopitia mwanzo. Sikuwa na mipango mingi sana, nilitaka kufanya vitu kwa utulivu. Sikuwa na mpango hata wa kutafuta mtaji wa kampuni haraka maana ndio chanzo cha ugomvi nilipotoka.

Siku moja nikaalikwa kwenye tukio moja kubwa sana nchini la mashindano ya kampuni changa zenye mawazo mazuri na makubwa. Washindi walikuwa wanapewa uwekezaji na mitaji kwenye biashara zao.

Mimi kwa kuwa sikwenda kutafuta mtaji wala wawekezaji nikasema nitatumia fursa ile kutangaza wazo langu na pengine kupata wateja wachache.

Kwa kuwa sikuwa na presha kubwa ya kushinda ilikuwa rahisi mimi kuwa mtulivu na kuelezea vizuri kushinda wengine. Nikashtuka sana mwishoni wakati wanatangaza washindi, mimi nikawa wa kwanza.

Wawekezaji watatu walikuwa tayari kutoa hela kuwekeza kwenye kampuni yangu. Wakaniuliza nahitaji kiasi gani ili biashara ikuwe? Nikawa sina jibu kwa sababu nilikuwa sina mpango wowote wa kutafuta hela.

Nikaomba muda kidogo wa kufikiria, wakanipa dakika thelathini. Nikapigia watu wangu wa karibu na wote wakashauri nisikatae hela. Nichukue tu, halafu mipango itakuja.

Nikarudi na kuwaambia wakinipa dola elfu kumi na tano ambayo ni sawa na karibu milioni arobaini ya kitanzania kwa sasa. Wakakubali bila kufikiria, mpaka nikaanza kujuta kwanini sikutaja kiwango cha juu zaidi.

Miezi kadhaa mbele wakatupa hizo hela zote mkononi na kutuachia mzigo mzito. Mwanzoni niliamini nikipata hela nitakuwa na mipango ya maana kwahiyo haina shida. Haikuwa hivyo.

Ukiwa na hela ndani na hauna mipango, kuna namna inapungua bila kuelewa. Tukaanza kuwa na malipo yasiyo ya lazima. Tukaanza kurusha hela kwenye matatizo yaliyohitaji kuzungumza au kusubiri.

Pia ikaja tatizo jingine la kwamba wawekezaji walioweka hela wakaanza kuuliza mipango yetu. Wakawa wanauliza mipango ya kampuni na kuomba tuibadilishe iendane na wanachotaka. Ikawa vigumu sana kubishana nao.

Haikuchukua muda mrefu nikaanza kukosa furaha na mwenendo wa biashara. Nikaanza kupata presha ya kuishiwa hela kwa sababu tuliingia kwenye mikataba mibovu kwa kuwa tulikuwa na hela mwanzo bila mipango na sasa hela inaanza kuisha.

Miaka miwili mbele ikabidi kufanya maamuzi magumu ya kuifunga biashara ile. Funzo kubwa nililobaki nalo ni kuwa hela inayokuja bila mipango huwa inaisha bila kuelewa.

Ukisubiri mshahara uje mwisho wa mwezi ndo uweke mipango mara nyingi utakuta ikifika katikati ya mwezi hela imekata, ulichofanya hakieleweki na vitu vingi haujafanya bado.

Na hii sio hela ya mshahara tu, kila hela inayokuja bila mipango mizuri huwa inapotea bila maelezo. Iwe umepewa zawadi, posho, umepata faida au mapato ya aina yeyote ile.

Mimi ilinihitaji milioni arobaini za kitanzania kuisha bila mipango ili nijifunze kuhusu umuhimu wa kuwa na mipango mizuri kwanza kabla hela haijafika. Nina imani hautafika kwenye hatua hiyo ya kupoteza kiwango kikubwa sana kujifunza makosa tuliyofanya wengine.

Kuwa na malengo, yatengenezee bajeti nzuri na subiri hela ifike. Na hela ikifika jilazimishe kuitumia kwenye bajeti na malengo yako.

Usipofanya hivyo utahisi kila siku una mikosi hela zako hazikai au hauna hela za kutosha kwenye maisha. Hauwezi kuwa na mipango mizuri ukipata hela. Kuwa na mipango mizuri na utavutia hela.

Uwe na furaha.

Uwe na afya.

Uwe huru kutokana na matatizo.

Uwe na amani.

Kama kuna kitu umejifunza mtumie mtu mmoja unayemjali.

#iThinkSo

Rogers Katuma

Financial Artist, Senior Adventurer, Occasional Storyteller and an Amateur Golfer


Discover more from iThinkSoo

Subscribe to get the latest posts sent to your email.