Mapango ya Amboni ni miongoni mwa sehemu zenye historia kubwa sana Tanzania. Wapiganaji walitumia kupambana na wakoloni wakijerumani kwa sababu ya sehemu na muundo wa mapango hayo.
Nilisoma shule ya sekondari ambayo ilikuwa karibu kabisa na mapango ya Amboni kwa miaka miwili lakini sikupata nafasi ya kwenda kutembelea. Miaka mitano baada ya kumaliza shule nikatembelea kama mtalii wa ndani.
Nilifurahia sana safari ile, nilivutiwa na maelezo ya kina kutoka kwa kiongozi wa pale pangoni. Alisimulia stori moja yenye funzo kubwa sana. “Mapango haya bado hayajafanikiwa kuchunguzwa kwa undani sana, yanasemekana yanatokea nchi ya Kenya.” Alianza kuelezea kwenye stori yake.
“Kulikuwa na mtalii mmoja mzungu alikuja na mbwa wake. Alisema kizazi chake kilikuwa Tanzania na kilishawahi kupita kwenye mapango yale upande wa Tanzania na kutokea nchini Kenya. Kuenzi utamaduni wa familia yake na yeye atafanya hivyo. Yule mzungu aliingia mapangoni na hakuonekana tena, mbwa wake alipatikana nchini Kenya. Inasemekana alipotea kwenye njia za mapango, na badala ya kusimama na kutafuta msaada akaendelea kwenda kwenye mapango yaliyo mpoteza zaidi.”
Sina uhakika na ukweli na uhalisia wa stori hii lakini nina kubaliana na funzo kubwa sana ambalo lipo kwenye stori hii. Funzo ni kwamba ukigundua umepotea, simama na uliza. Ukijikuta upo kwenye shimo, acha kuchimba. Funzo hili lilinisaidia mimi miaka michache mbele kwenye hekaheka zangu za utalii wa ndani.
Mara nyingi sana huwa napenda kwenda kwenye fukwe za bahari ambazo hazina watu wengi na zipo nje ya mji. Nina gari yangu kubwa ambayo ina uwezo wa kuingia mpaka ufukweni bila kusumbuliwa na mchanga. Na nina uzoefu wa kutosha kuendesha kwenye fukwe mbalimbali.
Safari hii ilikuwa tofauti sana, gari ilikwama sehemu ambayo siku nyingine zote tulikuwa tunapita. Kwenye udereva mara nyingi akili ya kwanza inakuambia kukanyaga mafuta zaidi na kuilazimisha gari. Lakini nikakumbuka funzo la kwenye mapango ya Amboni na kupotea kwa mzungu.
Nikajua kuna shida ambayo siyo ya kawaida ndio maana gari ikakwama, nikazima gari na kushuka kukagua. Nikagundua eneo lile kuna mtu mwingine alikwama muda sio mrefu. Pia inawezekana mvua kubwa ilinyesha na mchanga umekuwa laini.
Tukauliza wenyeji kuhusu kilichotokea na wakatuambia. “Kuna jamaa alikuja na gari yake ndogo akalazimisha kuingia nayo ufukweni, mvua ilikuwa imenyesha wiki nzima na mchanga umekuwa laini saini. Akakwama hapa na gari ikalala siku mbili. Jana ndio amekuja kutolewa kwa kuvutwa.”
Baadaye akatuonyesha sehemu nzuri ya kupita kwenda ufukweni na kurudi. Tungeamua kutosimama na kulazimisha gari ipite pale pengine tungekaa siku mbili pia. Lakini hekima ya kusimama, kuchunguza na kuuliza ilituokoa.
Mara nyingi kwenye maisha yetu tunajikuta kwenye mashimo, na badala ya kusimama na kujiuliza kwanini tupo kwenye mashimo hayo na njia ipi sahihi ya kutokea huwa tunaendelea kuchimba.
Tunatumia hela vibaya, zinaisha na matumizi bado hayajakamikika. Badala ya kusimama na kutafakari tumefikaje hapo tunaomba misaada au kukopa na kurudia matumizi yaleyale ya mwanzo.
Tunafanya kazi kwa nguvu bila kujali afya ya mwili na akili, tunachoka, kuumwa au kuishia kuharibu kazi. Na badala ya kusimama na kutafakari tumefikaje hapo tunaendelea kufanya kazi na kuharibu zaidi.
Tunaingia kwenye urafiki au mahusiano ambayo sio mazuri kwetu, yanatutesa na kutuumiza. Badala ya kusimama na kutafakari tumefikaje hapo ndio kwanza tunaongeza jitihada, ukaribu au kwenda hatua ngumu zaidi za mahusiano.
Yule mtalii mzungu angesimama na kutafakari muda aliogundua amepotea pengine angekuwa hai na mbwa wake. Yule jamaa aliyekwama kabla yetu pale ufukweni angesimama na kukagua mazingira na kuuliza wenyeji asingelala pale siku mbili na gari yake.
Na wewe ukiweza kusimama na kuuliza kwanini mara zote unaishiwa fedha pengine usingejikuta upo kwenye madeni yanayo kufanya ukimbie watu na kudhalilika. Pengine ungesimama na kujiuliza mahusiano yako yamefikaje hapo wakati mpo wachumba usingeumia zaidi kutafuta talaka baada ya kuoana, au kufia kwenye ndoa.
Pengine ungesimama na kutafakari ndugu, jamaa na marafiki gani wanakutumia kwa ulichonacho usingeumia baada ya wao kuondoka na kukuacha na shida maisha yalipo badilika.
Sio kila pango au shimo tunalojikuta tumo tulipenda au tulifanya makusudi kuwemo, lakini kwenye kila shimo na pango tutakalokuwemo tuna maamuzi ya kuacha kuingia ndani zaidi ya pango au kuacha kuchimba shimo.
Jifunze kusimama, kutafakari na kuuliza.
Ukijikuta ndani ya shimo, acha kuchimba.
Kama kuna kitu umejifunza, mtumie mtu mmoja unayemjali.
#iThinkSoo
Uwe na furaha
Uwe na afya
Uwe huru kutoka kwenye matatizo
Uwe na amani
Rogers Katuma
Financial Artist, Senior Adventurer, Occasional Storyteller and an Amateur Golfer
