Wote tunapenda kusafiri. Kwa watu waliokaribu na wanafunzi wa chuo wanatambua ambavyo kila mtu kwenye CV yake ameweka kusafiri kuwa miongoni mwa vitu anavyopenda kufanya. Kusafiri kuna maanisha fursa ya kujifunza, kupata uzoefu na kujua vitu tofauti.
Sikuwahi kuweka kusafiri kama kitu ninachopenda kwenye CV wakati namaliza chuo lakini ni kitu ambacho kimekuwa kipaumbele kwangu maisha yangu yote. Kwangu mimi kusafiri ndio njia ya haraka zaidi kujua maisha tofauti na ya kwangu.
Miaka kadhaa nyuma nilisafiri kwenda Dubai kama mtalii. Kwa sababu ilikuwa ni safari ya kwanza ratiba zote zilipangwa na kusimamiwa na kampuni ya utalii ya Dubai. Tuliruhusiwa kufanya vitu tulivyolipia pekee na kwa muda tuliokubaliana nao.
Kabla ya kusafiri kwenda Dubai niliona video na muvi nyingi sana zikielezea historia ya familia ya mtawala wa Dubai na namna alivyoibadilisha Dubai kutoka kuwa sehemu masikini sana mpaka jiji la kifahari. Niliona pia hekalu analokaa, kubwa sana na la kifahari. Nilifurahi tulivyoambiwa kuwa tunaweza kutembelea eneo lile.
Mimi huwa napenda kujifunza kwa watu walionizidi kwenye maisha. Ingawa hamna kitu tunachofanana na mtawala wa Dubai nilihamasika kuwa kwenye maisha unaweza kutoka chini na kufika juu kama historia yao. Na nikaamini nikitembelea hekalu lao nitakuwa karibu zaidi na historia yao na kujifunza mengi zaidi kutokana na wanavyoishi.
Siku ya kutembelea hekalu la mtawala wa Dubai ilianza vizuri sana. Dereva alikuwa anatupa taarifa za ndani kabisa na stori nyingi za kuvutia kuhusu hekalu tunaloenda na familia ya mtawala. Njia za kwenda hekaluni zilikuwa kubwa na za kuvutia pia. Hamu ya kuwahi kufika ikaongezeka. Dereva akawa anajisifia ni mara ngapi amefika pale kuleta watalii. Tukamuamini kwa kila kitu.
Tukafika sehemu ya maegesho ya magari ya watalii, ilikuwa kubwa na ya kifahari sana. Muda tulioenda ulikuwa mzuri pia hivyo kulikuwa hakuna watu wengi. Nikafungua mlango haraka kuwahi kushuka kwenye gari, nikasikia dereva anasema, “Rogers, subiri kidogo, kuna utaratibu wa kufuata ukiwa maeneo haya.”
Nikafunga mlango na kumsikiliza kwa makini, “ Hauruhusiwi kutembea kuvuka kizuizi cha polisi ambao wapo mbele ya geti la nje la kuingia kwenye hekalu la mtawala wa Dubai. Hairuhusiwi kuwapiga picha wala kuchukua video hao polisi. Unaruhusiwa kupiga picha kwenye gari la polisi lakini sio kwenye geti,” akaendelea.
Maneno yake yalinikatisha tamaa sana, yani tumesafiri kutoka Tanzania mpaka Dubai ili kuja kuishia nje ya geti la hekalu kubwa zaidi duniani pengine. Tena haturuhusiwi hata kupiga picha hapo getini. Bora hata wangeturuhusu kuingia getini na kuchungulia ndani kupoje.
Na akanimaliza zaidi aliposema pale tunaruhusiwa kukaa kwa dakika thelathini tu tangu gari isimame. Nikaangalia saa na kugundua ameshatumia dakika sita kutoa maelezo tu. Nikashuka kwa unyonge na kuanza kutalii mazingira ya nje.
Kitu pekee cha kuvutia pale ilikuwa ni gari ya polisi. Dubai wana magari ya polisi ya kifahahari sana. Kuanzia Bugatti, Lamborghini, Ferrari na G-Wagon. Polisi wa pale nje ya geti la hekalu ya mtawala wa Dubai walikuwa na G-Wagon mpya kabisa. Nikaenda kusimama mbele na kupiga picha nyingi sana.
Na pale ndio ndoto yangu kutaka kuja kumiliki G-Wagon ilizaliwa pia. Baada ya kumaliza kupiga picha hapo getini dakika zetu thelathini ziliisha, tukarudishwa kwenye gari na kuanza safari kwenda kwenye ratiba nyingine. Safari ile niliumia sana kufika hadi getini na kutoruhusiwa kuingia ndani.
Miaka michache mbele nikaandaa safari nyingine, safari hii ilikuwa Zanzibar kwenye hotel ya nyota tano ya Melia. Kama kawaida, niliangalia kila video na taarifa kuhusu hoteli hii ya kifahari kwenye mitandao. Nikaona video za mamilionea na mabilionea wakitembelea na familia zao. Nikajua ni sehemu nitakayo hamasika.
Harufu ya samaki na karafuu ilikuwa kitu cha kwanza kusikia tuliposhuka kwenye bandari ya Zanzibar. Kanzu na misuli ilikuwa mingi nje ya sehemu ya kuegeshea magari, nikiwa natafuta namba ya dereva taxi wetu mzee Mwinyimvua nikasikia naitwa pembeni, alituona kabla yetu.
“Mimi nimeenda sana pale Melia kupeleka wageni,” mzee Mwinyimvua akaanza stori. “Yani ile hoteli ni ya kifahari kweli kweli, ni kama upo ulaya hivi,” aliendelea. Mimi sikuwa na hamasa ya kutaka kusikia sana kuhusu stori zake kwa sababu nakumbuka mambo ya Dubai.
Dereva wa Dubai alitupa stori nyingi sana za hekalu la mtawala wa Dubai na mwisho tukaishia nje ya sehemu ya kusimama magari. Ingawa safari hii ya Zanzibar nilikuwa na uhakika wa kuingia getini na kulala ndani ya hoteli Ila bado kuna hofu nilikuwa nayo.
Dereva alitushusha sehemu ya kupokelea wageni na kuondoka zake. Sisi tukapokelewa kama wafalme. “Karibuni juisi ya baridi mpoze koo,” alituambia mfanyakazi mmoja wa mapokezi aliyevaa suti nyeusi na tai ya kijivu.
Mizigo yetu ilibebwa kwa umakini na ustadi wa hali ya juu. Baada ya kumaliza kukagua taarifa zetu wakatuambia tushuke chini kuna dereva anakuja kutuchukua kutupeleka kwenye vyumba vyetu.
Dereva alikuja amevaa suti ya kaki, bila tai akiwa anaendesha zile gari ndogo zinazotumika sana kwenye mchezo wa gofu. Wakati tupo njiani tukapishana nazo kama nane hivi, kumbe ndo usafiri wao mle ndani wa kutoa wageni sehemu moja kwenda nyingine, hakuna kutembea kwa miguu.
“Mkiangalia upande wenu wa kulia ni mwanzo wa mbuga yetu ndogo ya wanyama. Kuna tausi, digidigi, ndege wa aina tofauti na wanyama wengi zaidi. Pia upande wa kushoto kuna wanyama wengi wa mitini kama kima na nyani,” dereva alisema.
Kichwani kwangu nikasema watu wanaishi, ndio maana mamilionea na mabilionea wanakuja eneo lile. Akili yangu ikarudi Dubai, nikasema kama Melia Zanzibar kupo hivi na watu wanalipia kuangalia je kwenye lile hekalu la mtawala wa Dubai?
Siku mbili nilizokaa pale Melia Zanzibar nilijifunza vitu vingi sana. Niliona namna matajiri wanaishi na familia zao. Nilipata wasaa wa kuongea na baadhi yao kujua wanafanya biashara gani kuwawezesha kukaa pale siku nyingi zaidi na kwa gharama kubwa zaidi. Nikahamasika kufanya kazi kwa bidii zaidi na mimi nirudi pale kama wao.
Najua na wewe unapenda kusafiri. Najua pia umesikia au umeona mazuri na maajabu mengi sana ya sehemu kama Dubai. Najua pia kuna sehemu nyingi ulienda na kuhamasika kama mimi nilivyohamasika Melia Zanzibar. Ila kuna safari moja tunaifanya kila siku ambayo hatuitendei haki, SAFARI YA KUJIFUNZA.
Kila siku inayoenda tunapata fursa za kujifunza. Sio lazima kusafiri Dubai au Zanzibar ili kwenda kujifunza. Ukisoma hii unaweza kujifunza kitu. Ukiangalia video YouTube unaweza kujifunza kitu. Ukikutana na mtu amekuzidi kitu kwenye maisha unaweza kujifunza. Na ukweli ni kwamba mpaka sana tumeshajifunza vitu vingi sana kwenye maisha.
Shida yetu ni kwamba safari yetu ya kujifunza ni kama safari yangu ya Dubai. Nilifunga safari kutoka Tanzania hadi Dubai halafu nikaishia getini kwenye hekalu la mtawala wa Dubai. Sijui mle ndani kunaonekanaje, kunanukiaje au kuna nini cha tofauti.
Wengi tunajifunza vitu vingi na hatuvifanyii kazi. Hivi ni sawa na kufanya safari mpaka Dubai na kuishia getini. Kujifunza kitu kipya bila kukifanyia kazi ni kufika getini bila kuingia ndani. Umeshafika kwenye mageti mengi sana lakini haujui ndani kuna nini.
Ni kweli mageti mengi yanavutia, kama ambalo lile la hekalu la mtawala wa Dubai, lina polisi wenye magari ya kifahari na sehemu kubwa sana ya kuegesha magari na bustani za kutisha. Lakini bado haina maana kwa sababu sikuingia ndani.
Ukisoma sehemu kuhusu kuandaa bajeti kwenye maisha yako, kuweka akiba kutoka kwenye kipato chako na kutafuta njia ya kuwekeza hapo ni umefika getini bila kuingia ndani ya hekalu la maswala ya fedha. Ukianza kutengeneza bajeti kila mwezi, kuweka akiba na kuwekeza hapo unakuwa umeingia ndani. Patia picha maisha yako yatakavyo kuwa ukiwa hauna presha ya kuishiwa hela, hauna madeni, una kipato cha ziada kufuata ndoto zako?
Mtu akikwambia umuhimu wa mazoezi, kula vizuri, kujizuia kiwango cha pombe na moshi inayodhuru mwili wako hapo amekukaribisha getini bila kuingia ndani ya hekalu la maisha bora. Ukianza kufanya mazoezi, kula vizuri na kuzuia kuingia vitu vyenye madhara mwilini mwako unakuwa umeingia ndani. Patia picha maisha yako yakiwa na afya, furaha, nguvu na kunawiri.
Ukiangalia video YouTube inazungumzia namna ya kujenga mahusiano na urafiki bora hapo ni umefika getini bila kufika kwenye hekalu la mahusiano bora. Mahusiano bora yanaanza kwa kuaminiana, kuwekeza nguvu kwenye kuwasiliana, kujitolea na kupata wasaa wa pamoja mara kwa mara. Ukianza kuwa muaminifu, kuweka nguvu kutafuta watu unaowajali na sio kusubiri wakutafute, kutenga muda kwa ajili yao hapo unakuwa umeingia ndani. Haina haja ya kukwambia umuhimu wa marafiki na mahusiano bora kwenye maisha yako.
Kuanzia sana hivi kila kitu kipya unachojifunza kumbuka kuwa umefika getini tu, ukianza kufanyia kazi ndo unakuwa umeingia ndani na kuona mazuri yote ambayo yamefichwa na geti. Maisha yangu hayakubadilika kwa kuishia getini Dubai, yalibadilika kwa kuingia ndani ya Melia Zanzibar.
Kwa miaka uliyonayo, umeshajifunza vitu vingi sana. Ina maanisha umeshafika kwenye mageti mengi sana. Umeshapiga picha nyingi sana kwenye hayo mageti na kujisifia sana. Muda umefika sasa wa kuanza kuingia ndani ya hayo mageti ili ubadilishe maisha yako.
Inawezekana wakati unaisoma hii nikawa nimerudi tena Melia Zanzibar.
Uwe na furaha,
Uwe na afya,
Uwe huru kutoka kwenye matatizo
Uwe na amani.
Kama kuna kitu umejifunza, mtumie mtu mmoja unayemjali.
#iThinkSo
Rogers Katuma
Financial Artist, Senior Adventurer, Occasional Storyteller and an Amateur Golfer
