Mara nyingi napata mafunzo mengi sana kutoka kwenye mchezo wa mpira wa miguu. Mafunzo hayo yanakuja kwa njia tofauti. Mengine kutoka kwa makocha wa timu na uzoefu wao, mengine kutoka kwa wachezaji wenzangu. Ila mafunzo mengi zaidi yametokana na kuchunguza na kufuatilia vitu uwanjani.
Nimeshacheza mechi zaidi ya elfu kwenye maisha yangu. Mechi moja ambayo nilijifunza vitu vingi sana ilikuwa nusu fainali ya mashindano ya ligi ambayo moja ya timu yangu ilishiriki. Timu ilikuwa na wachezaji tegemezi wanne, ambao walikuwa wanatoa mchango mkubwa sana kila mechi. Mimi nilikuwa mmoja wao.
Kutokana na umuhimu wa mechi hii, kocha alituanzisha wote wanne kwa wakati mmoja. Ila ni mimi peke yangu nilicheza mpaka mwisho. Wengine walitoka kwa sababu tofauti tofauti zenye mafundisho makubwa sana.
Mchezaji wa kwanza ambaye ndio alikuwa kapteni wa timu alikuwa ni bora kushinda wote. Changamoto yake kubwa ilikuwa ni hapendi mazoezi. Kocha alijitahidi sana kumlazimisha lakini haikuwahi kuzaa matunda.
Mara nyingi alikuwa mjanja wa kukwepa mazoezi. Na mechi hii haikuwa tofauti. Wakati sisi tunafanya mazoezi mepesi ya kujiandaa na mechi yeye alikuwa anajificha nyuma ya mtu au anaongea na mashabiki.
Mwanzo wa mchezo ilikuwa spidi kubwa sana. Ndani ya dakika chache tu kapteni wetu akapata pasi moja nzuri sana. Pasi iliwekwa kwa mbele ili kuwahadaa mabeki. Ilibidi kapteni wetu aongeze spidi kidogo tu kuifikia, kumpiga chenga kipa, kufunga na kwenda kwenye kona kushangilia.
Hiyo siku haikuwa leo, alipojaribu kukimbilia ule mpira mwili wake ulikataa. Akashtua misuli na kuanguka chini kama mfuko wa viazi. Maumivu kwenye macho yake yalisema kila kitu, ule ndio ulikuwa mwisho wake kwenye ile mechi na yale mashindano. Kapteni wetu alishindwa kufanya mazoezi ya kupasha mwili kwa ufasaha na akaishia kutuangusha timu nzima siku ambayo tulikuwa tunamtegemea.
Alipotolewa akabadilishwa na mchezaji mwingine ambaye hakuwa kwenye mipango ya kocha na ni wa kawaida sana. Na presha ilimuingia kabla hata hajaanza kucheza kwa sababu aliingia kuchukua nafasi ya kapteni, mchezaji bora wa timu. Haya yalikuwa ni mabadiliko yaliyofeli kabla hata ya kuanza.
Mchezaji wetu bora wa pili alikuwa miongoni mwa watu wanaopenda sana mazoezi. Alikuwa ni yule mtu wa mfano ambaye kocha alikuwa anamuita pale anapotaka kuonyesha njia sahihi ya kufanya zoezi. Shida yake kubwa ilikuwa ni kwamba ana hasira za karibu sana. Kitu kidogo tu kitakacho tokea kitakuzwa na kuwa vita ya dunia.
Ilimchukua dakika ishirini tu na kuchezewa vibaya mara tatu kumfanya aanzishe ugomvi. Alimpiga ngumi beki wa timu pinzani na refa akampa kadi nyekundu ya moja kwa moja. Tukampoteza mchezaji wetu wa pili bora, na alituacha tucheze pungufu tukiwa tumebaki na zaidi ya saa zima la mchezo.
Mchezaji wetu wa tatu bora alikuwa ni miongoni mwa watu wema sana. Alikuwa kapteni msaidizi, na hakuwa mvivu kabisa. Alikuwa mpole kiasi kwamba ulikuwa na uwezo wa kumchoma kisu akiwa anakokota mpira, akainuka, akajifunga kidonda na kutabasamu huku akikuangalia.
Changamoto yake kubwa ilikuwa ni kuwa presha ya mechi na mashabiki ikimuingia basi hakuna atakachokifanya mechi nzima. Alikuwa anahitaji muda mwingi na watu wengi wa kumpa hamasa na kumpa moyo kila dakika.
Baada ya kapteni wetu kutoka kwa kuumia na mchezaji wetu wa pili kupewa kadi nyekundu yeye akawa kapteni na watu wote wanamuangalia yeye. Ile ikampa presha na mashabiki wakaanza kumzomea. Akaanza kukosea sana kiasi ambacho hakuna mtu alikuwa anaamini kama jamaa alikuwa anajua kucheza mpira. Ikabidi kocha amtoe.
Ulipofika muda wa mapumziko kocha akaja kutupa moyo, mwisho akasema kitu kimoja ambacho kimekuwa fundisho kubwa sana kwenye maisha yangu. “Jitunze na jijali wewe kwanza, ili uweze kuwatunza na kuwajali wengine,” alianza kusema kocha.
“Kapteni wenu alishindwa kujitunza na kujijali kwa kufanya mazoezi ya kupasha mwili akaishia kuumia, kapteni msaidizi kashindwa kuhimili presha ya mchezo ikabidi nimtoe. Mwingine hapa hasira zimemzidi karusha ngumi,” akaendelea.
Akanipa mimi kitambaa cha kapteni na kusema, “Rogers, ili uweze kuisaidia timu kwanza jijali na jitunze mwenyewe. Usiumie, usipate hasira ya kucheza vibaya au kuanzisha fujo ukapewa kadi nyekundu na muhimu zaidi usiruhusu presha ya mchezo ikupande kichwani.”
Nilirudi kipindi cha pili nikiwa na morali na hamasa kubwa sana ya kusaidia timu ishinde. Maneno ya kocha yalikuwa yanajirudia kichwani mwangu kila nikipata mpira.
Tukafanikiwa kupata goli kipindi cha pili ambalo ilitokana na mimi na kocha alifurahi sana. Mchezo ukaisha na tukafanikiwa kwenda fainali. Kumbukumbu kubwa zaidi ilikuwa ni somo la kocha, “Jitunze na jijali wewe ili uweze kuwatunza na kuwajali wengine.”
Ni msemo mmoja mdogo sana wenye mantiki kubwa sana kila sehemu ya maisha. Ukiweza kufanya kazi kwa bidii, kupata kipato na kuwekeza na kuweka akiba yako mwenyewe utakuwa kwenye nafasi nzuri sana ya kusaidia wengine kwenye kutafuta kipato, kuwekeza na kuweka akiba, hususani watu unaowapenda na kuwajali.
Ukiweza kutunza mwili wako, kula vizuri, kupumzika na kuwa na afya njema utakuwa kwenye nafasi nzuri sana ya kuwatunza na kuwajali ndugu na jamaa ambao wana matatizo ya kiafya.
Ukiweza kuwa na amani na furaha kwenye maisha yako binafsi utakuwa na uwezo wa kuwapa furaha na amani watu wako wa karibu.
Kujijali na kujitunza wewe sio ubinafsi, ni njia sahihi ya kuwa na uwezo na nyenzo za kusaidia na kujali watu wengine. Hauwezi kuwapa watu kitu ambacho hauna.
Fanya kazi kwa bidii, jenga maisha yako, kuza biashara zako, tengeneza mahusiano yako, kuwa na furaha, amani na upendo kwanza wewe na ndio utakuwa kwenye nafasi nzuri ya kusaidia ndugu, jamaa na marafiki.
Wakati unasoma hii chukulia kocha wetu anaongea na wewe muda wa mapumziko kwenye mchezo muhimu wa fainali ambayo wewe ndo umepewa kitambaa cha kapteni na anakwambia, “Jitunze na jijali wewe ili uweze kuwatunza na kuwajali wengine.
Uwe na furaha.
Uwe na afya.
Uwe huru kutoka kwenye matatizo.
Upate amani.
Kama kuna kitu umejifunza, mtumie mtu mmoja unayemjali.
#iThinkSo
Rogers Katuma
Financial Artist, Senior Adventurer, Occasional Storyteller and an Amateur Golfer
