Nimetumia muda mwingi wa ukuaji wangu na mama au familia yake. Na kipindi hicho niliweza kujifunza tabia zao nyingi sana. Tabia moja kubwa wote walikuwa nayo na walijitahidi kutufundisha ni nidhamu.
Na mama alikuwa na haki ya kutufundisha nidhamu kwa sababu yeye ndio alikuwa baba na mama kwa wakati mmoja kutukuza sisi. Kutunza watoto watano peke yake muda mwingi ni kazi kubwa sana. Na jambo la mwisho alilokuwa anahitaji kwenye maisha yake ni kuwa na mtoto mmoja ambaye kila siku alikuwa anachelewa kurudi nyumbani kwa sababu alienda kucheza mpira wa miguu mbali (mimi huyo).
Kama wazazi wetu wengi kwa kipindi hicho, njia kuu ya kufundisha nidhamu kwa mtoto ni kumchapa na fimbo. Mara zote nilizokuwa nachelewa kurudi nyumbani alikuwa anaficha fimbo sehemu, anasubiri nikaoge, nile chakula cha usiku na kisha kunipiga sana.
Kuna kipindi nakumbuka nilipigwa kila siku karibu mwezi mzima kwa sababu ile ile, kwenda kucheza mpira, kuchelewa kurudi nyumbani. Ikafika siku ikabidi nichague kimoja, kumheshimu yeye na matakwa yake au niendelee kucheza mpira na kupigwa kila siku. Nikaamua kuacha kucheza mpira, vile vipigo vilikuwa vimezidi.
Kwa kipindi kile nilikuwa naona mama yangu ni katili na ana roho mbaya sana. Lakini marafiki zangu walikuwa wanampenda na kumsifia sana mama yangu kwa upendo na ukarimu. Walikuwa wakija nyumbani anawapa zawadi, chakula na kucheka nao sana. Wakati huo mimi nilikuwa siwezi kuweka neno “mama” kwenye sentensi moja na “ukarimu” au “upole”.
Baada ya kipigo cha karibu mwezi mzima kwa sababu ya kuchelewa kurudi na mimi kufanya maamuzi ya kuacha mpira mama akabadilika. Akaacha kunipiga, akaja na mbinu mpya, sasa hivi nikikosea akawa anakaa kimya. Nina imani umeshawahi kusikia msemo wa “kimya kingi kina mshindo mkubwa,” nadhani mama yangu aligundua huo msemo.
Ukimya wa mama yangu ulikuwa ni pale unapomkosea au kukosea, akachukia na kuamua kukaa kimya. Hasemi chochote kuhusu ulichokosea, lakini anabadilika namna anavyoongea na wewe, uchangamfu unapotea na maneno yanakuwa machache sana.
Mama yangu alikuwa ananiandalia chai, anasubiri ninywe, ataosha vyombo vyangu, atafanya kazi zote ambazo alikuwa ananituma mimi nifanye zamani, ananipa nauli ya kwenda shule na haongei chochote na mimi.
Alikuwa haulizi naendeleaje, nimefanya nini shule, kwanini nimechelewa kurudi au nilikuwa wapi. Wikiendi ambazo siendi shule nashinda nyumbani zamani ilikuwa natumwa sana kila saa, safari hii alikuwa haniongeleshi wala hanitumi. Na alikuwa na uwezo wa kufanya hivi mwezi mzima. Maumivu ya kufanyiwa hivi na mama yako mzazi ni makubwa sana kushinda kupigwa kila siku.
Alisubiri mpaka mimi nishindwe kuvumilia, niende kuomba msamaha. Kwenye kuomba msamaha hapo ndio ilikuwa kama kuongeza chumvi kwenye kidonda, alihakikisha unajisikia vibaya kwa matendo yako kwa namna nzito sana kwa mtoto. Mara nyingi mazungumzo ya msamaha na mama yangu yalikuwa hivi:
“Mama samahani,” naanzisha mazungumzo wakati anapika,
“Samahani ya nini?” atajibu huku akiniangalia kwa jicho kali sana,
“Nilichelewa kurudi nyumbani kwa sababu nilienda kucheza mpira kwa kina Robert,” nitajielezea,
“Kwanza kuna shida wewe ukichelewa kurudi nyumbani?” atajibu kwa upole bila kuniangalia machoni.
“Kwa sababu haupendi,” nitajibu kwa uoga.
“Mimi nisipopenda kitu kuna shida gani, wewe si umeshakuwa mkubwa?” atauliza.
Mazungumzo haya yataendelea kwa staili hii kwa muda mrefu. Atanifanya nijisikie vibaya, nijidharau, nijidhalilishe, nijutie na nilie sana mpaka atakapoamua kupokea msamaha wangu. Baada ya hapo atauliza kwanini sikuomba msamaha mapema, itafuata na risala ndefu sana ya makosa yangu yote.
Kama haujawahi kupitia kitu kama hiki hauwezi kuelewa mateso ya kisaikolojia ambayo binadamu hupitia kufanyiwa hivi na mtu anayempenda na kumtegemea, mama mzazi. Maumivu niliyokuwa nayapata kwa kufanyiwa hivyo yalikuwa ni makubwa na ya muda mrefu sana.
Na kadri alivyokuwa ananifanyia hivyo ndio nilivyozidi kuathirika kisaikolojia na kubakia na maumivu ndani yangu. Ikafika muda nikawa naomba nikikosea bora nipigwe yaishe. Mwanzoni nilidhani kupigwa kila siku kwa sababu ya kuchelewa kurudi kutoka kwenye mpira ilikuwa ni mbaya. Sasa hivi nikagundua kununiwa na kuteswa kisaikolojia ni mbaya zaidi.
Sina makovu yeyote ya vipigo nilivyopewa na mama yangu. Ila bado nina maumivu ya kisaikolojia kwa njia yake ya pili. Na mbaya zaidi na mimi nikaanza kuiga njia ile kwa watu wakinikwaza na kunikosea. Na inaumiza sana kujua maumivu wanayopitia nikifanya hivyo.
Miaka mingi baadaye niliweza kuongea na mama na kumuelezea madhara ya kisaikolojia yaliyotokana na njia yake ya kununa, kususa na kukaa kimya tukikosea. Alijisikia vibaya nilipomwambia ni bora alivyokuwa ananipiga. Aliomba msamaha na kuahidi kubadilika. Akaahidi kuwa sasa hivi tukimkosea atakuwa anatuambia, ili tujielezee au tuombe msamaha na yaishe.
Na kweli mama yangu akabadilika, na mimi nikaanza kubadilika na kuacha ile tabia kwa watu wengine. Mtu akikosea na ninamjali namwambia ukweli, akiomba msamaha heri, asipoona kosa lake ni heri pia mimi nitakaa pembeni kwa amani na furaha.
Miaka michache nyuma nilimtembelea mama kazini kwake kabla hajastaafu. Kuna mfanyakazi mwenzake mmoja akawa anatania kuwa mama yangu ni mkali sana. Mtu akikosea chochote kile yeye huwa anamuita pembeni na kumwambia. Watu wengi wanaogopa kukosea mbele yake.
Nikacheka sana kusikia vile, ikanikumbusha utotoni wakati marafiki zangu wanasema mama yangu ni mpole sana na ana upendo wakati mimi nilikuwa namuona katili kwa kunichapa kila siku kisa tu kuchelewa kurudi baada ya kwenda kucheza mpira.
Sasa hivi mimi namuona mama yangu anajali kwa kuwa mkweli na muwazi mtu akikosea na huku mfanyakazi mwenzake analalamika. Na hapo ndio kuna funzo kubwa sana la maisha, hamna kitu kibaya au kizuri, ni namna unavyokitazama ndio hufanya kiwe kibaya au kizuri.
Namba sita na tisa zote zina muonekano sawa ukizitazama kwa njia tofauti. Vitu unavyoviona wewe vizuri kuna watu wanaviona vibaya sana. Fedha, mamlaka, dini, ndoa, urafiki, familia, makabila, ajira na biashara.
Kuna watu wanaona fedha na wenye fedha ni wabaya sana, wabinafsi na hawataki kusaidia vitu wao wanataka. Kuna watu wanaona wenye fedha ni mhimili muhimu sana kwenye jamii kwa ajira, fursa na misaada wanayotoa.
Kuna watu wanaona kuajiriwa ni bora sana kwasababu kuna uhakika wa mshahara, marupurupu na pensheni baada ya kustaafu. Kuna watu wanaona kuajiriwa ni utumwa wa muda, ukosefu wa uhuru na jela kufanya usifuate ndoto zako.
Kuna watu wanaamini ndoa ni muhimu, sababu ya furaha na mhimili wa mafanikio. Kuna wengine wanaamini ndoa ni jela, sababu ya mateso, unyanyasaji na ukosefu wa uhuru, amani na furaha. Ndio maana kuna watu wapo kwenye ndoa hazina furaha wala upendo lakini wanabaki kwasababu wana amini ni lazima wawe humo. Kuna watu wanakila sababu ya kuoa au kuolewa lakini wanasema bado wapo wapo sana.
Kuumwa ni kitu kibaya sana kwa mtu yeyote yule, lakini kuna watu wengi sana wangechagua mtu wao waliyekuwa wanampenda sana akafariki arudi hata kwa siku chache tu, akiwa anaumwa waweze kuwa naye mara ya mwisho.
Chochote unachopitia kwenye maisha tambua kinaweza kuwa kizuri kwako lakini kibaya sana kwa mwingine. Na kile unachokiona kibaya kwa mwingine inawezekana kwake yeye ni bora zaidi. Usiishi maisha yako kuaminisha watu kipi ni kibaya au kizuri. Usiyumbishwe kwenye maamuzi yako kwa sababu kuna mtu anaamini ni mbaya.
Kama ambavyo sita na tisa ni namba moja iliyotazamwa kutoka sehemu tofauti na hivyo ndio kila kitu kwenye maisha. Hamna kitu kibaya wala kizuri, inategemea na namna unavyo kitazama.
Uwe na furaha.
Uwe na afya.
Uwe huru kutika kwenye mateso
Uwe na amani.
Kama kuna kitu umejifunza, mtumie mtu mmoja unayemjali.
#iThinkSo
Rogers Katuma
Financial Artist, Senior Adventurer, Occasional Storyteller and an Amateur Golfer
