Mungu Anaona Ndani Yako, Watu Wanaona Vya Nje

“Baba yake ni mtu wa Ulaya, ameishi sana Afrika Kusini kabla ya kuja hapa chuoni,” Robert alianza kutupa stori kuhusu mwanafunzi mmoja wa kike mrefu, mzuri na anayeonekana kama chotara.

“Subiri kwanza, umeshawahi kuongea naye?” Nilimuuliza Robert kwa shauku maana angekuwa ametisha sana.

“Naanzia wapi mchovu mimi, kuna watu wanakaa naye karibu wanamjua ,” alijibu na wote tukacheka.

Haya yalikuwa ni mazungumzo ya kawaida sana kwetu sisi wakati tupo mwaka wa kwanza chuo kikuu cha Dar es salaam. Tulizungumzia wanawake tuliokuwa tunawaona, magari na wamiliki wake, walimu wa chuo na hata namna washkaji wanavyovaa. Kuna wengine tuliwaita wapendwa, wengine mabishoo na wengine watanashati kwa kuangalia tu nguo zao.

Na hii haikuwa sisi tu, hata wewe huwa unafanya hivyo. Unaona watu au kitu na kuwa na mtazamo nacho, kutengeneza stori yako na kuishi nayo.

Na usijisikie vibaya, ni hulka ya binadamu. Kila tunachokiona tunakitafsiri kwa mazoea yetu au uelewa wetu. Mambo ya kusubiri kuelezwa au kuona uzuri wa ndani tunamuachia Mungu.

Tulikuwa marafiki kama sita hivi wakati Robert anamuelezea yule msichana mpya ile siku. Lakini aliposema tu yule chotara wa Afrika kusini wote tulijua anamzungumzia nani. Na wote hatujawahi kuongea naye wala kujua jina lake.

Miaka michache chuoni yule “chotara wa Afrika Kusini” tuliyekuwa tunamzungumzia akaja kuwa rafiki yangu wa karibu na pia mchumba wangu. Nikaja kujua kuwa baba yake sio mtu wa ulaya na yeye hajawahi kuishi Afrika kusini.

Ni kawaida kwa binadamu kuwa na mtazamo wa kila kitu na kukiundia stori hata bila mhusika kupata nafasi ya kujielezea.

Sasa hivi akija kwako mtu amevaa suti nzuri anakusimamisha na kukuuliza kitu utamsikiliza kwa makini sana. Tofauti na ambavyo mtu akija na nguo chafu na imechanika akijaribu kukusimamisha, utahisi ni omba omba.

Sasa kwenye maisha ya watu wewe ndo yule mtu mwenye suti kapotea anasimamisha watu wamuelekeze au ni yule jamaa mwenye nguo zilizochanika na chafu akisimamisha watu wanamuona omba omba.

Hakuna mtu atakupa nafasi nyingine ya kusema yule mwenye suti ni tapeli mzoefu na huyu mwenye nguo chafu zilizochanika aliibiwa na kuteswa sasa katoroka anahitaji msaada. Hiyo kazi watu wamemuachia Mungu.

Ni majukumu yako kuweka jitihada kuhakikisha unatengeneza mazingira ambayo stori watu wakatakayo iweka kichwani kuhusu wewe ni stori nzuri.

Vaa vile ambavyo ungependa watu wakuchukulie. Hauwezi kuvaa kama msanii na watu wakakuchukulia kama mfanyakazi wa benki. Hauwezi kuvaa nusu uchi na watu wakakuchukulia mpendwa.

Hauwezi kuishi maisha kama mjinga na haujielewi na watu wakakuchukulia una hekima na uzoefu. Hauwezi kufanya vitu kama haujali na watu wakakuchukulia kama unajali.

Kama haupo kwenye mahusiano na unaishi kama haupo kwenye mahusiano watu watakufata na kutaka kuwa na mahusiano na wewe. Ukiwa haupo kwenye mahusiano lakini unaishi kama upo kwenye ndoa miaka hamsini watu wataachana na wewe.

Ukipata kazi, basi kuwa na muonekano unaoendana na kazi yako na fuata masharti na vigezo vya kazi yako na watu watakuheshimu kazini na kukupa fursa zaidi.

Ukianzisha biashara basi itangaze biashara yako kwa namna unataka watu waitambue biashara yako na kuvutia wateja ambao biashara yako imekusudia.

Ukiingia kwenye mitandao ya jamii utaona namna watu wakijirekodi wakifungua maboksi ya simu zao mpya za iPhone. Wakiwa na furaha na mbwembwe nyingi sana. Sijawahi kuona watu wakifanya hivyo wakinunua simu za Techno au Oppo.

Watengenezaji wa simu za iPhone wameweza kuziweka simu zao kama ishara ya mafanikio, ubora na kujipata. Na wateja wanachukulia hivyo pia. Techno na Oppo wamejiweka kama simu za walala hoi. Na watu wanazichukulia hivyo pia.

Ukienda kukutana na mtu unayetaka kuwa na mahusiano naye ukiwa mchafu, unanuka na unaonesha haujijali, atakuchukulia hivyo pia. Na kuna dalili nyingi sana hatataka kukutana na wewe mara nyingine.

Jali muonekano wako, jali stori ambazo watu wanazitengeneza na kuambiana kwa muonekano, matendo, mienendo na tabia. Mungu pekee ndo anoana wewe ni mtu wa namna gani moyoni, sisi tunaangalia nywele zako, viatu, nguo, unachoposti mitandaoni na kila kinacho onekana.

Uwe na furaha

Uwe na afya

Uwe huru kutoka kwenye matatizo

Upate amani

Kama kuna kitu umejifunza, mtumie mtu wako mmoja unaye mjali.

#iThinkSo

Rogers Katuma

Financial Artist, Senior Adventurer, Occasional Storyteller and an Amateur Golfer


Discover more from iThinkSoo

Subscribe to get the latest posts sent to your email.