Chura Asiyesikia, Juu Ya Mti Mkubwa

Mama yangu alinitambulisha kwenye ulimwengu wa kusoma vitabu nikiwa mdogo sana. Alinitengenezea maktaba ndogo chumbani kwangu na akawa analeta vitabu vya aina mbalimbali. Sijui alikuwa anavitoa wapi lakini kwangu vilibadilisha maisha.

Mwanzoni ilikuwa ngumu sana mimi kukubali kusoma vitabu vyake. Sababu kubwa ni kuwa alitaka nisome vitabu muda ambao nilikuwa nataka kwenda kucheza mpira. Hakuna mtoto yeyote angependa. Akatambua mapema sana tatizo lipo wapi, akanipa ofa ya kuwa nikisoma kitabu kwa dakika thelathini ataniruhusu kucheza mpira mpaka giza litakapoingia. Haraka sana nikakubali.

Kitabu cha kwanza kukisoma kutoka kwenye maktaba aliyotengeneza mama chumbani kwangu ilikuwa ni mjumuisho wa stori fupi fupi kuhusu vyura. Na stori ya kwanza kabisa iliitwa “Chura Asiyesikia, Juu Ya Mti Mkubwa”

Naomba nikusogeze kwenye maktaba yangu ndogo, karibu kwenye sofa lililochakaa chumba kikiwa na mwanga hafifu wa mishumaa, tujikumbushe wote stori hii:

Hapo zamani kulikuwa na chura mmoja mdogo aliyeishi kwenye jamii ya vyura kwenye maeneo yasiyokuwa na miti. Chura huyu alikuwa na ndoto na mapenzi makubwa sana ya kutaka kupanda miti. Mwanzoni alikuwa anaogopa kumwambia chura yeyote ndoto yake kwa sababu jamii nzima ilikuwa haisapoti.

Akaificha na kujitesa sana na ndoto yake, lakini kadri siku zilivyozidi kwenda ndio alivyozidi kupata hamasa ya kufuata ndoto yake. Siku moja akaamka asubuhi sana na kukimbilia porini ambako kulikuwa na miti.

Vyura wenzake walivyoona akikimbilia porini kwenye miti wakamfuata ili wamrudishe. Porini kulikuwa na na hatari za kila aina. Vyura walikuwa wanavamiwa na nyoka, kunguru na wanyama wengi sana. Pori lilikuwa kubwa na linatisha pia.

Chura yule mwenye ndoto ya kupanda mti alikuwa na hamasa na furaha kubwa sana, spidi aliyokuwa nayo ya kwenda porini ilikuwa kubwa kwa wale chura wanaomfuata kumkuta kwa wakati.

Alipofika porini akatafuta mti mkubwa kushinda yote, na kuanza kujaribu kupanda tawi la chini kabisa. Haikuwa rahisi kwake, alikuwa hajui afanye nini na wala aanzie wapi. Aliruka sana, kuanguka sana na kupata vidonda na maumivu mengi. Lakini hakukata tamaa.

Baaada ya masaa machache akafanikiwa kuruka juu zaidi na kufika kwenye tawi la kwanza la mti mkubwa kabisa kwenye pori. Furaha yake ilikuwa kubwa sana kiasi ambacho maumivu yote yalipotea. Akiwa anendelea kufurahia hatua yake kubwa akaona chura wenzake wakija kwa kasi sana.

Akapumzika kidogo na kuwasubiria, akafikiria kuwa pengine na wao wana ndoto ya kupanda mti kama yeye. Wale chura wengine walivyofika pale na kumkuta ameshapanda kwenye mti wakapata hofu zaidi.

Itakuwaje akianguka na kuumia au kufa. Itakuwaje kunguru wakimuona kutoka hewani na kumvamia. Itakuwaje nyoka akimfuata kule juu na kumn’gata au kummeza. Hofu ile ikawafanya wapige kelele nyingi sana huku wakirukaruka kumwambia ashuke.

Yule chura alipoangalia chini na kuona wakirukaruka akahisi wanampa moyo wakuendelea. Akapata nguvu mpya ya kunza tena kutafuta tawi linalofuata. Hamasa ikaongezeka, uchovu ukaisha na maumivu yakapotea. Akafanikiwa kufika tawi la juu zaidi.

Wale chura wa chini wakazidi kupiga kelele na kurukaruka kumuomba ashuke. Kumwambia hakuna chura anayeweza kupanda mti mkubwa vile. Kumwambia kuwa kunguru wapo karibu na ni hatari sana.

Yule chura akawa kila akiangalia chini na kuona wanarukaruka anaendelea kupata hamasa na nguvu. Baada ya masaa kadhaa akafika juu kabisa ya ule mti mkubwa kushinda yote porini. Akawa hawaoni tena wale chura wenzake chini. Akatimiza ndoto yake.

Wale chura wa chini wakaanza kushangilia kwa mwenzao kufanikisha ndoto yake. Wakajiona wanabahati kubwa sana kushuhudia chura wa kwanza kwenye jamii yao kupanda mti, tena mti mkubwa zaidi kushinda yote porini. Wakaanza kupiga kelele kumuomba ashuke ili kuwafundisha namna alivyofanya na wao waige.

Yule chura alikuwa juu sana kiasi ambacho alikuwa hawaoni wale chura chini. Furaha yake ilikuwa kubwa sana kiasi ambacho hakuwa na haraka ya kushuka chini. Ndoto yake ilikuwa imetimia.

Baada ya masaa kupita mama wa yule chura kule juu akafika porini na kuwakuta wale chura wengine wapo chini wakimsubiria mwenzao. Wakamueleza mama yake kitu mwenzao alichofanya na namna walivyojitahidi kumkataza wakati anapanda.

Mwisho wakamuuliza, “kwanini tunampigia kelele muda sana ashuke aje kutufundisha na sisi namna ya kupanda mti na hataki kushuka?”

Mama yake akatabasamu na kuwaambia, “mwanangu ni kiziwi, asikii kitu chochote. Mlivyokuwa mnapiga kelele na kurukaruka yeye aliona kama mna muhamasisha apambane zaidi. Kelele zenu na kuruka kwenu kwake ilikuwa ni motisha. Nina imani asingekuwa asikii angewasikiliza na angeshindwa kupanda huu mti”

Stori hii ilinihamasisha sana, ilibakia kidogo tu usiku wa kwanza naisoma kunifanya niende nje na mimi nipande kwenye mti mkubwa kabisa nje ya nyumba yetu, karibu na makaburi. Mwisho wa ile stori kwenye kitabu wakaweka na funzo likasema;

Kama una ndoto na malengo, na una amini katika uwezo wako basi utahitaji kuwa na uwezo wa kufunga masikio yako na kutosikiliza pale ambapo watu wataanza kukukatisha tamaa wakati unafanyia kazi ndoto na malengo yako.

Watu wengi watakukatisha tamaa kwenye safari ya kufuata ndoto zako. Kuna ambao watakukatisha tamaa kwa sababu hawaielewi ndoto yako. Kuna wale ambao watakukatisha tamaa kwa sababu walishindwa kufuata ndoto zao, hawataki wewe uwe tofauti na wao.

Kuna wale ambao watakukatisha tamaa kwa sababu walijaribu kufuata ndoto zao wakashindwa na wana maumivu. Hawataki wewe upitie maumivu hayo au wanaamini kuwa kwa sababu wao walishindwa na wewe utashindwa pia.

Ndoto yako inaweza kua kufuata kipaji chako. Inaweza kuwa kuingia kwenye siasa. Inaweza kuwa kuanzisha biashara. Inaweza kuwa kufuata maono yako ya kiroho au kifamilia. Inaweza kuwa kutafuta kazi ya aina fulani.

Ukiamua kufuata ndoto yako kila siku asubuhi utakuwa na vitu viwili vya kuchagua. Kuchagua kuwasikiliza na kukata tamaa au kuchagua kuziba masikio na kuendelea kujaribu. Ukiendelea kujaribu kwa muda mrefu tobo lako litapatikana, utafanikiwa sana na watu waliokuwa wanakukatisha tamaa watakusubiri chini uje uwasaidie na kuwapa ushauri ulifanyaje.

Nakumbuka nilimsimulia stori hii mama ynagu baada ya kuisoma na kumwambia ana bahati sio ndoto yangu kucheza mpira wa kiushindani. Nataka kusoma sana, nije nianzishe kampuni na kufanya biashara. Alifurahi sana kwa sababu alikuwa hapendi mimi nikicheza mpira.

Miaka mingi mbele nakumbuka wakati namwambia mama kuwa nataka kuacha kazi ili nifuate ndoto yangu ya kufungua kampuni na kufanya biashara alinipinga sana. Akanielezea mabaya yote ya kufanya hivyo, akanipa mifano yote ya waliojaribu na kushindwa.

Nikamkubushia kuhusu stori hii ya chura, na maongezi tuliyokuwa nayo kuhusu mimi kusoma. Akatabasamu na kunikumbatia, ishara ya kwamba ingawa hakupenda maamuzi yangu alijua hataweza kunizuia, ni bora asapoti.

Kwenye maisha, utapingwa au kutopewa sapoti na watu wako wa karibu sana kipindi unaanza kufuata ndoto yako na malengo yako. Kuwa tayari kuziba masikio kila siku. Haukuzaliwa kiziwi lakini una uwezo wa kutosikiliza watu wanaokukatisha tamaa kwenye ndoto ambayo hawailewi.

Uwe na furaha.

Uwe na afya.

Uwe huru kutoka kwenye matatizo

Uwe na amani.

Kama kuna kitu umejifunza, mtumie mtu mmoja unayemjali.

#iThinkSo

Rogers Katuma

Financial Artist, Senior Adventurer, Occasional Storyteller, and Amateur Golfer


Discover more from iThinkSoo

Subscribe to get the latest posts sent to your email.