Wakati Unaomba Mvua Inyeshe, Jiandae Kulowa Na Matope Pia

Mapenzi yangu ya kusoma na kujifunza yalianza na maktaba ndogo ambayo mama yangu alinitengenezea chumbani kwangu. Ikaendelea kukua mpaka nikajiunga na maktaba ya taifa. Nikawa naenda maktaba kila mwisho wa wiki, nasoma vitabu tofauti na kuazima vingine na kwenda navyo nyumbani.

Hiyo iliendelea kwa miaka mingi mpaka muda intaneti ilipofika. Kipindi hicho ilikuwa tunaenda kwenye vibanda vyenye kompyuta na intaneti, unalipia kwa saa na kutafuta vitu mbalimbali mitandaoni baadaye unarudi nyumbani. Kitu cha kwanza kuwahi kutafuta mtandaoni ilikuwa ‘hadithi fupi fupi zenye mafundisho maishani’.

Nikapata hadithi moja fupi sana na yenye mafundisho makubwa sana kwenye maisha. Ni miaka zaidi ya kumi na nane imepita na bado mafundisho yake yanahitajika kuyaelewa kwenye maisha. Kwa upendo mkubwa naomba nikusimulie stori hiyo:

Hapo zamani kulikuwa na kijiji kimoja ambacho kwa karne nyingi sana walibarikiwa kuwa na mvua kila mwaka, mazao yanakuwa kwa wakati na kila sehemu kuna ukijani wa miti, matunda na nyasi. Miaka ya karibuni mambo yakabadilika.

Kijiji kilipitia miaka kadhaa bila mvua, hii ikafanya mazao yafe. Kijiji kikawa hakina miti, matunda wala majani. Ukame ukatembelea kijijini na kuhatarisha maisha yao wote. Wazee wa kijiji wakakubaliana kuitisha kikao maalumu kujadili wafanye nini.

Kwenye kikao chao wakakubaliana inahitajika wafanye maombi kwa miungu yao. Wanakijiji wengi sana wakaja siku ya maombi kwenye uwanja mkubwa sana pale kijijini. Uwanja ambao zamani ulikuwa na nyasi na miti mizuri pembeni, sasa hivi ulikuwa na vumbi tu. Mwenyekiti wa kijiji akawatangazia watu wote wafanye maombi ya kuomba mvua kwa Mungu yeyote wanayemuamini.

Kabla ya maombi kufanyika kuna kitu cha kushangaza kikatokea. Kuna binti mdogo sana akawa anakaribia kwenye uwanja wa maombi akiwa amebeba mwamvuli na viatu vya mvua. Watu wakashangaa sana, na mzee mmoja aliona ule mshangao, akamsubiri yule binti asogee kisha akamuuliza;

“Mjukuu wangu, kwanini umebeba mwamvuli na kuvaa viatu vya mvua wakati tuna miaka kadhaa hatuna mvua?”

Yule binti akafunga mwamvuli wake, akatabasamu na kusema, “Babu yangu aliwahi kuniambia kuwa, ukiomba mvua, jiandae kulowa na kutembea kwenye matope pia”

Hii stori fupi iliishia pale, haikuelezea kuhusu maombi yao wala upatikanaji wa mvua. Nilitumia muda mwingi sana kuitafakari ile kauli ya yule binti mdogo kuhusu maombi. Miaka mingi mbele nilielewa kwanini iliishia pale.

Kipindi ambacho nimetoka kuisoma hadithi ile fupi na mimi nilikuwa kwenye maombi mengi sana kwa Mungu wangu. Nilikuwa naomba mama yangu aendelee kupata fedha ili anilipie ada. Nilikuwa naomba niwe miongoni mwa wanafunzi bora shuleni. Nilikuwa naomba nikimaliza kusoma tu nipate kazi. Nilikuwa naomba nikiwa mkubwa nianzishe biashara. Naomba siku moja nimiliki gari.

Lakini sikuwahi kuwa na imani kuwa maombi yangu yalikuwa yanawezekana. Sikuwa na ushuhuda wa mtu aliyefanikiwa na maombi kama yangu. Na sikuwa naishi maisha nikiwa na imani maombi yangu yatafanikiwa. Na zaidi sikuwahi kufikiria gharama zinazohitajika kulipa maombi yangu yakitimia. Mimi sikuwa tofauti sana na wale wanakijiji.

Na hauwezi kuwalaumu wale wanakijiji wala mimi, ni asili ya binadamu. Tumeumbwa kuwa na mitazamo tofauti kuhusu imani. Tukiwa wadogo huwa tunaamini kila kitu kinawezekana kwenye maisha. Tunaamini tunaweza kuwa chochote na yeyote tunayetaka tukiamua.

Tunapojaribu vitu tunakutana na uhalisia. Tunafeli kwenye vitu mbalimbali, watu wetu wa karibu wanaanza kutukatisha tamaa. Tunaanza kupata uhalisia kuwa sio kila maombi yanapokelewa. Tunaanza kuelewa kuwa sio kila maombi yanapokelewa kwa muda tunaotaka sisi.

Mara ngapi umejaribu kufanya kitu kipya au cha utofauti na wazazi wako wakakukatisha tamaa kuwa haiwezekani?

Mara ngapi unawaambia rafiki zako kuwa haiwezekani kwao kutimiza malengo yao kwa sababu wewe ulishindwa au mtu fulani aliyekuwa na sifa kushinda wao alishindwa?

Majibu ya maswali yote hayo ni MARA NYINGI SANA.

Hii inaanza kutubadilisha namna tunavyoona vitu kwa namna mbili;

Kwanza tunaanza kukubali kuwa sio kila tunachotaka kwenye maisha tutakipata. Tunakubali kuwa kuna vitu hatuvipati na hatutakuja kuvipata kamwe. Ndoto zetu zinaanza kuwa jela na utumwa. Matumaini yanaanza kuwa hofu. Taratibu tunaanza kuacha kuamini kuwa maombi yetu na ndoto zetu zitatimia.

Ni kama wale wanakijiji, walikaa miaka mingi bila mvua na inawezekana walifanya maombi mengi sana binafsi bila mafanikio. Hawakuwa na imani ya kutosha kuwa kwa pamoja itawezekana ingawa walikubali wito.

Pili kwenye maisha ukiwa unafanya maombi unatumia muda mwingi sana kufikiria unachokitaka kiasi kwamba hautumii mwingi kutafakari kwa undani gharama na changamoto zinazokuja kwa kupata unachotaka maishani.

Dunia inafanya kazi kwa njia ambayo kila unachokitaka kwenye maisha kina gharama yake.

Unaomba upate mchumba au mume/mke, ufunge ndoa na mjenge familia. Unatumia muda mwingi kwenye hayo maombi na unaacha kujianda na gharama na changamoto za mume/mke, ndoa na kulea watoto. Ndoa zina mapishano, utofauti wa tabia, utofauti wa mahitaji na ndoto kwa sababu mlilelewa tofauti na kuwa na tabia tofauti kwenye maisha yenu yote kabla hamjakutana. Ndoa haitakuja na upendo na maua tu, itakuja na haya mengine.

Unaomba kuwa tajiri mwenye mali nyingi sana. Unasahau changamoto ambazo matajiri wenye mali nyingi wanapitia. Matajiri huombwa pesa na mali na kila mtu kila wakati. Ndugu, jamaa na marafiki wapo tayari kuua ili warithi mali. Watu wanaowazunguka matajiri wapo tayari kuiba au kudhulumu. Watu wanaacha kupenda na kujali kwa dhati, wanajali watapata nini kutoka kwako. Hizi ni changamoto ambazo hauwezi kuziepuka wakati unaomba utajiri.

Unaomba upandishwe cheo kazini, unasahau changamoto zinazokuja na cheo kipya. Cheo kipya kinakuja na majukumu mapya na makubwa zaidi. Cheo kipya kinakuja na lawama nyingi zaidi. Cheo kipya kinakuja na wivu kutoka kwa wafanyakazi wenzako. Usitegemee cheo kipya kije na changamoto za zamani.

Unaomba upate umaarufu na nguvu kwa jamii na hautumii muda mwingi kufikiria changamoto zinazokuja na umaarufu huo. Watu kufuatilia maisha yako binafsi, kukusema bila sababu. Kutokuwa na uhuru wa kufanya vitu vya kawaida kama kutembea kwa miguu, kula kwa mama ntilie au kurudia nguo.

Hii hufanya watu kujuta baada ya kupata vitu walivyoviomba kwa sababu hawakujiandaa na changamoto ambazo zinakuja na vitu wanavyoomba. Ni kama wale wanakijiji, maombi yao yangefanikiwa, mvua kubwa ingenyesha wangelalamika sana kwa kulowa na ile vumbi kugeuka na kuwa tope.

Kwa maisha yako chukua hekima ya yule binti ambaye alibeba mwamvuli na kuvaa viatu vya mvua wakati anaenda kwenye maombi ya kuomba mvua inyeshe.

Wakati unaomba na kupambana kupata jambo fulani kwenye maisha hakikisha unatafakari na kujiandaa na changamoto ambazo zitakuja.

#iThinkSo

Uwe na furaha

Uwe na afya

Uwe na amani

Uwe huru kutoka kwenye matatizo

Jiunge kwenye listi ya barua pepe uweze kupokea kila wiki moja kwa moja. Kama kuna kitu umejifunza pia, mtumie mtu mmoja unayempenda na kumjali.

Rogers Katuma

Financial Artist, Senior Adventurer, Occasional Storyteller, and Amateur Golfer


Discover more from iThinkSoo

Subscribe to get the latest posts sent to your email.