Hauwezi kuwa na utajiri wowote kwenye maisha wakati una utajiri wa visingizio

“Tunaenda kukimbia leo?” Nilimtumia ujumbe mfupi Peter, ambaye ni rafiki yangu na mfanyakazi mwenzangu.

“Leo hapana kaka, nimechoka sana.” Alinijibu kwa ufupi. Mimi nikaenda kukimbia siku ya kwanza, ilikuwa ni saa kumi alfajiri, giza limetanda na baridi kali inayosikika kwenye mifupa.

Mimi na Peter tulikuwa tumejisajili kukimbia kwenye Marathoni ya kilomita ishirini na moja ambayo kampuni yetu ilikuwa miongoni mwa wadhamini. Ili kuweza kushiriki tulihitaji kufanya mazoezi ya kukimbia asubuhi sana kabla ya kwenda ofisini kwenye majukumu yetu ya kila siku.

“Vipi leo, tunaenda kukimbia?” Nilimpigia Peter siku ya pili kumuuliza baada ya kusema amechoka jana.

“Leo sijachoka kaka, lakini nimeacha viatu vya kukimbilia ofisini, unataka nikimbie na mabuti?” Alinijibu kwa utani. Mimi nikaamka na kwenda kukimbia tena peke yangu, mida ilikuwa ni ile ile, saa kumi asubuhi.

Wiki tatu mbele nikampigia tena asubuhi kumuuliza kama tunakimbia, akasema “Kaka hauoni hiyo mvua nje?” Nikamwambia naiona, nikakata simu na kwenda zangu kukimbia maana ilikuwa imebaki wiki moja kabla ya marathoni.

Siku ya marathoni Peter alikuja kushiriki, kwasababu ofisini walikuwa wanategemea wote twende kwenye mbio zile. Peter alikimbia kwa tabu sana kwakuwa hakuwa na mazoezi. Ndani ya kilo mita mbili tu za kukimbia akaumia na kushindwa kuendelea.

Mimi nilimaliza mbio zangu za kilomita ishirini na moja, nikapata medali yangu na kuiwakilisha vizuri kampuni. Nilijifunza funzo kubwa sana la maisha kwenye zike mbio; VISINGIZIO HAVILETI MATOKEO UNAYOYATAKA.

Kwa haraka haraka Peter alikuwa na sababu kubwa sana za kutokujumuika na mimi kwenye yale mazoezi ya asubuhi. Siku ya kwanza Peter alikuwa amechoka. Siku ya pili Peter alikuwa amesahau viatu vya kukimbilia ofisini. Siku ya tatu kulikuwa na mvua kubwa sana.

Najua na wewe unakubaliana na sababu za Peter, kwa kuwa kwenye vitu vingi vya maisha yako huwa unapata sababu kama hizo.

Unachelewa kufika kazini, unasema kulikuwa na foleni kubwa sana asubuhi, hata bosi wako anajua kuhusu foleni ya lile eneo maarufu.

Unasogeza mbele kuanza biashara kwa sababu bado hauna mtaji wa kuanzia, hata kwenye historia ya kidato cha tatu kilisema kukosekana kwa mtaji ni tatizo kubwa sana linalochelewesha maendeleo Afrika.

Unasubiri rafiki zako au mpenzi wako aanze kukutafuta kwa sababu ukimtafuta wewe utakuwa umejishusha na una shobo kwenye mahusiano au urafiki.

Peter naye alikuwa na kila kisingizio ili asiamke asubuhi kufanya mazoezi. Mimi pia nilikuwa nachoka sana, na nilikuwa nafanya kazi kama yake. Lakini nilijikaza na kujilazimisha kuamka na kufanya mazoezi.

Mimi pia sikuwa na viatu vya kukimbilia kabla ya kujisajili kwenda kwenye marathoni. Lakini nilienda kununua na kuhakikisha kila siku vinakuwepo nyumbani muda ninaotaka kukimbia asubuhi.

Mimi pia nachukia kufanya mazoezi kwenye mvua, lakini nilijilazimisha kwenda hivyo hivyo kwa sababu nilijua muda ulikuwa unakaribia na sitakuwa na siku nyingi za mazoezi.

Na mimi kama binadamu wengine, kuacha shuka lenye kunipa joto wakati natoka kwenye usingizi mzito wa saa kumi asubuhi ni changamoto sana. Lakini nilijua kuwa nikiendelea kulala basi lengo langu la mazoezi na marathoni halitatimia.

Kwenye maisha kila unachokitaka kinahitaji juhudi, uvumilivu na jitihada. Matokeo chanya hayaji kwenye kitu chochote kwenye maisha bila hivyo vitu. Na ukikosa hivyo vitu mara nyingi unakuwa na kitu kimoja tu, VISINGIZIO.

Visingizio ni zile stori unazo jiambia wewe mwenyewe au kuwaambia watu kwa kushindwa kuanza au kumalizia jambo fulani. Na Mungu ametubariki wengi wetu na utajiri wa visingizio. Na utajiri huu wa visingizio ndio sababu kubwa sana ya kushindwa kupata utajiri mwingine kwenye maeneno mengine ya maisha.

Tunakosa utajiri wa mali, afya, urafiki na mahusiano kwa sababu tuna utajiri wa visingizio.

Unahitaji kula vizuri, kula matunda, kufanya mazoezi na kupumzisha mwili. Unahitaji kujizuia kula vyakula vyenye mafuta mengi au kuzuia matumizi yako ya pombe ili uwe na utajiri wa afya. Na kufanya hivyo vitu unahitaji juhudi, nidhamu na uvumilivu. Wengi tuna utajiri wa visingizio tayari, ndio maana hatuwezi kufanikisha hilo.

Kuondoa kitambi na nyama uzembe unahitaji kuacha kula na kunywa vyakula na vinywaji vya aina fulani na kuanza kufanya mazoezi ya aina fulani. Lakini kwa sababu tayari una utajiri wa visingizio hauwezi kufanya hivyo vitu miaka nenda na kurudi.

Kupata utajiri wa mali unahitaji kuongeza kipato chako kwa njia ya biashara au kuongezwa mshahara kazini, pia kuanza kuweka akiba kwenye kipato chako halafu kuwekeza hiyo akiba kwenye vitu mbalimbali na kusubiria.

Lakini kwa kuwa tuna utajiri wa visingizio tayari hatuwezi kufanya hivyo. Tuna visingizio vyote duniani kwanini hatuwezi kuongezewa kipato chetu kazini, faida kutokukua kwenye biashara, kushindwa kuweka akiba na kufanya uwekezaji.

Kuwa kwenye mahusiano yeyote yale yenye furaha, upendo na kudumu inahitaji kuwekeza muda, hisia na mawasiliano mazuri na mwenzako. Kwa kuwa kuna visingizio vya kutosha duniani kwanini ni ngumu kufanya hivyo unajikuta hauwezi kukaa kwenye mahusiano kwa muda mrefu.

Kila kitu unachohitaji kwenye maisha kinahitaji juhudi. Juhudi zinavyoongezeka na matokeo chanya huongezeka. Visingizio vinavyoongezeka na juhudi pia hupungua. Na kadri juhudi inavyopungua ndio unavyozidi kuwa mbali na malengo unayoyataka.

Peter ni rafiki yangu wa muda mrefu sana, lakini usiwe kama yeye kwenye maisha yako. Acha visingizio kwenye kufuata malengo yako na ndoto zako.

Ukiona hauna utajiri kwenye sehemu yeyote ya maisha yako (mali, afya, mahusiano), kuna asilimia kubwa sana kuwa wewe tayari ni TAJIRI WA VISINGIZIO.

#iThinkSo

Uwe na furaha.

Uwe na afya.

Uwe huru kutoka kwenye matatizo

Upate amani

Kama kuna kitu umejifunza jisajili na barua pepe yako kuweza kupata hizi stori moja kwa moja kwenye simu yako. Pia mtumie mtu mmoja unayemjali na yeye ajifunze kitu.

Rogers Katuma

Financial Artist, Senior Adventurer, Occasional Storyteller, and Amateur Golfer


Discover more from iThinkSoo

Subscribe to get the latest posts sent to your email.