Siku ya kufa nyani, miti yote huteleza

Nlilipia kununua gari yangu ya kwanza siku ya mwisho ya mtihani chuo kikuu, na ilichukua miezi miwili kufika Tanzania kutoka Japan. Wakati nalipia gari nilikuwa na hela ya kuagizia tu, nikapiga mahesabu ya kodi na gharama nyingine zitakazo hitajika gari ikifika Tanzania na kuanza kujipanga.

Mpango wangu ilikuwa kwamba kwa sababu nimepata kazi haraka baada ya kumaliza tu chuo, basi miezi miwili ambayo gari itakuwa njiani kuja Tanzania nitakuwa na mshahara wa hiyo miezi. Nikajua nikiongeza akiba yangu kidogo na kuchukua mkopo mdogo kwa rafiki yangu nitalipia gharama nilizokadiria kulipia ushuru.

“Rogers, tafadhali pokea makadirio ya gharama za kodi ya gari yako iliyofika bandarini jana,” nilianza kusoma barua pepe iliyotumwa na wakala wa forodha niliyemtumia kunisaidia kutoa gari bandarini.

“Gharama nilizokadiria kutoka mamlaka ya mapato Tanzania inaonyesha ni mara mbili ya kiwango tulichokadiria kabla gari haijafika huku. Pole sana lakini inabidi ujipange vizuri.” Sikumbuki maelezo mengine yeyote yaliyofuata kwenye ile barua pepe, kwa sababu nilichanganyikiwa nikajikuta nampigia ili tu aniambie ananitania.

Baada ya kumpigia akaniambia ule sio utani, na akaniongezea taarifa nyingine mbaya, “halafu nilisahau kukwambia, kila siku gari inavyoendelea kukaa bandarini kuna faini na ushuru unaongezeka, ni muhimu tumalize hili swala mapema.” Akasema na kukata simu.

Ile simu ilikuwa mbaya sana kwangu. Na sio tu ilikuwa mbaya pale bali kila siku itakayokuwa inafuata itaendelea kuwa mbaya sababu ya ushuru na faini kama wakala wangu alivyosema. Ina maanisha sikuwa na muda wa kulia wala kulalamika, inabidi nitafute suluhu.

Nikapata wazo kuwa nikiweza kumuomba rafiki wa pili mkopo nikajumlisha mshahara wangu na nikaongeza kutoka kwenye akiba naweza kutatua tatizo hilo. Nikapata moyo kidogo na kuanza kupiga simu.

Nikampigia rafiki yangu wa kwanza ambaye nilishamuelezea shida yangu kabla, hakuwa na hiyana, akanitumia kiasi tulichokubaliana muda ule ule. Nikampigia yule rafiki wa pili na yeye alikubali kunisapoti. Nikafurahi sana kwa sababu hapa kilichobakia ni mshahara wa mwezi huu uje, niongezee nikalipie.

Mshahara ulikuwa unaingia asubuhi ya saa nne siku ya tarehe ishirini na tano. Katika siku zote, hii siku ya leo nilikuwa nahesabu kila dakika kwa sababu mshahara huu ulikuwa na umuhimu sana. Ikafika mpaka saa kumi jioni sikupata meseji ya mshahara kwenye simu yangu, nikaanza kupata hofu.

Nikauliza wafanyakazi wenzangu wakasema kuwa wao wamepata, kama kuna shida itakuwa kwangu tu. Kwa kuwa muda ulikuwa umeisha ikabidi nisubiri siku inayofuata. Asubuhi sana nikaenda kwa mhasibu kudai mshahara wangu.

“Rogers, kuna fomu haukujaza kwa kazi uliyofanya mwezi uliopita, hivyo hautapokea mshahara mpaka zikamilike na kutufikia ofisini,” alisema mhasibu huku akiangalia kompyuta yake kuhakikisha anachosema.

Mimi nakumbuka vizuri kabisa kuzijaza zile fomu kwa wakati na kumpelekea meneja wangu kwa wakati. Yeye ndio inabidi anieleze nini kilitokea. Nikampigia meneja akawa hapatikani, nikatuma barua pepe ikaonyesha kuwa meneja yupo nje ya ofisi kikazi.

Nikaenda kwa msaidizi wake akaniambia, “amesafiri kwenda nje ya nchi, atarudi baada ya wiki mbili”. Nikaishiwa nguvu, nikakaa kwenye kiti cha yule msaidizi wake bila kuomba ruhusa.

Akajaribu kuniuliza shida ni nini, nikamwambia aniache kwanza nahitaji kutoka nje kunyosha miguu kabla sijafanya maamuzi ya kijinga. Katika wakati wote ambao mshahara haukutakiwa kukatwa ni sasa hivi. Siku zinaongezeka bandarini, gharama zinaongezeka na sina njia ya kupata fedha kamili kulitoa gari langu.

Nikaanza kujuta kuagiza lile gari. Ghafla likanijia wazo, benki nina hela ya pango la chumba ninachokaa, wao wanategemea niwalipe ndani ya siku tatu. Pia nikiuza baadhi ya vitu vyangu vya thamani nitapata hela ya ziada. Nikitumia fedha zile kulipia ushuru wa gari, litatoka. Wakati huo nitaanza kutafuta kodi ya chumba na pengine tatizo la mshahara litakuwa limetatuliwa.

Nikazima simu nisipate usumbufu kutoka kwa mtu yeyote, nikarudi ofisini haraka na kubeba vitu vyangu na kukimbilia benki. Nikaenda nikatoa fedha yote ya kulipia pango la chumba na kuongezea kwenye zile hela nyingine. Nikauza simu yangu na ipad kwa bei ambayo mpaka sasa naona aibu kuwaambia watu.

Muhimu ni kuwa fedha ikatimia kiwango cha kulipa gharama za mwanzo za ushuru. Faini haikuwa kubwa sana ile siku mbili, yule wakala alinilipia. Nikafanikisha kulikomboa gari langu kutoka bandarini. Furaha na amani ya moyo ikarudi jioni ile.

Nikiwa na furaha ya kukomboa gari, siku ya tatu ikafika na sikuwa na suluhisho lolote la pango. Ila nikasema kwakuwa sijawahi kuwasumbua kuhusu pango lao kwenye kuwalipa nitawaelezea changamoto yangu na watanielewa.

Ile nyumba ilikuwa inamilikiwa na familia, dada na kaka watatu. Walikuwa wanapokea kodi na kugawana kwenye kila chumba. Hii siku ambayo mimi nilipanga nije kuwaelezea changamoto yangu na kushindwa kulipa kodi kwa muda walikuwa wote kwa pamoja jioni wakati narudi, wakiisubiria hela yao.

Mmoja wa wale ndugu alinielewa, lakini ndugu zake hawakutaka kusikiliza kitu. Wakakubaliana inabidi niondoke usiku ule watafute mpangaji mwingine. Nikaishiwa nguvu, nikajisikia kudharaulika sana. Lakini sikuwa na namna, ikabidi nitafute utaratibu wa kutoa vitu vyangu.

Uzuri ilikuwa ni chumba kimoja na sikuwa na vitu vingi. Nikampigia jirani yangu mmoja chumba cha pili kama atanisaidia niweke vitu kwake akirudi, mimi nitafute sehemu ya kulala. Akakubali, na akanipa ofa kuwa yeye yupo safarini, naweza kuweka vitu na kulala kwake pia wakati natafuta sehemu nyingine ya kuhama.

Nikachukua godoro langu nikaweka juu ya godoro la jirani yangu. Nikachukua chaga na mbao za kitanda changu na kuweka chini ya uvungu wa kitanda chake. Vitu vingine nikavifunga kwenye mifuko ya plastiki na kuweka kwenye kona. Nikawakabidhi funguo na kuhamia kwa jirani yangu nijiandae kulala. Nikasema mambo hayawezi kuwa mabaya zaidi ya hapo, nilijidanganya.

Wiki kadhaa nyuma nilikuwa nimeanza mahusiano na msichana ambaye alikuwa ananivutia tangu mwaka wa kwanza chuoni. Yeye alipokubali kuwa kwenye mahusiano na mimi ilikuwa kitu kikubwa sana. Wiki nzima iliyopita alikuwa anomba kuja kulala kwangu, nikawa nampa sababu nyingi sana kwa nini asije. Nipo bize, nitachelewa kurudi, nasafiri kikazi na nyingi sana.

Akaona nina sababu nyingi sana, akaamua aje mwenyewe kwa kunishtukiza. Katika siku zote ambazo angechagua kuja, akaamua kuja siku hii ambayo nimefukuzwa kwenye chumba changu. Alikuja wakati namalizia kuhamisha vitu kwa jirani yangu.

Hakusema kitu chochote lakini lugha ya mwili na sauti yake ilionyesha maumivu yake. Kichwani kwake alijua kuwa sababu ya mimi kukataa yeye kuja ni ile. Hakuonesha kukereka wala hakutaka kuzungumzia kinachoendelea. Alinikumbatia na kubadilisha mada.

Kichwani kwangu nikasema katika siku zote za kudhalilika Mungu amechagua hii, nimemkosea nini mimi. Nikasema kwa kweli siku ya kufa nyani miti yote huteleza. Nikasema hakuna tena kitu kibaya zaidi kitatokea usiku ule kuongeza maumivu, sikujua lililofuata.

Umeme ukakatika usiku. Chumba kidogo, kimejaa vitu vyangu na vitu vya jirani yangu. Nimetembelewa na mpenzi wangu kwa mara ya kwanza na umeme unakatika. Kama umeshawahi kujaribu kukumbatiana na mtu unayempenda kwenye joto usiku wa manane unaelewa hali ilivyokuwa.

Inawezekana unasoma hii na kusema hii ni siku mbaya kabisa kwenye maisha yangu. Au unaweza kusema hiki kilikuwa kipindi kibaya zaidi kwenye maisha yangu. Uhalisia ni kuwa hii ni kawaida sana.

Tangu nimejitambua nimeelewa kuwa dunia ndio ipo hivyo. Utapitia kwenye vipindii kama hivi mara nyingi sana kwenye maisha. Kila kitu kinaenda kombo kwa wakati mmoja na haupewi mapumziko.

Kama mwanafunzi unaweza kuchelewa kuamka siku ya mtihani muhimu zaidi. Na siku uliyochelewa kuamka ndo siku ambayo unakutana na foleni kubwa sana kuwahi kutokea. Na unafika kwenye chumba cha mtihani ukiwa umechelewa unagundua umesahau kitambulisho au peni.

Kama mfanyakazi inaweza ikatokea siku uliyoamka hauna morali ndio siku unaambiwa uongee mbele ya wenzako. Ndio siku ambayo jasho linaamua kutoka kwa wingi. Ukiwa unajitahidi kutulia unagundua umeacha wazi zipu yako na nguo yako ya ndani inaonekana.

Kama mfanyabiashara unaweza pitia kipindi ambacho yule mteja mmoja unayemtegemea akulipe akawa hapatikani au kughairi kununua. Ukiwa una mawazo hayo bahati mbaya unamwagia chai kwenye kompyuta yako ambayo ina taarifa muhimu zinazohitajika kupeleka mamlaka ya mapato ili usilipishwe kodi nyingi.

Kwa nafasi yeyote uliyokuwepo jifunze kukubaliana na ukweli huu. Kwenye maisha changamoto zitakuja. Vitu vitaenda kombo na kinyume na matarajio. Na zaidi ni kujua kuwa vitu hivyi vitatokea katika wakati mbaya zaidi kwa kipindi hicho.

Usitumie muda mwingi sana kulalamika kwanini vitu vimetokea?

Kwanini vimetokea kwako?

Kwanini vimetokea sasa hivi?

Kubali kuwa huo ndio uhalisia wa maisha na anza kutafuta suluhisho.

Muhimu zaidi ni kujiandaa kisaikolojia kila siku kwenye maisha yako kujua kuwa kuna kipindi kitakuja mbeleni ambapo kila kitu kitaenda tofauti na malengo na matarajio. Na vitu hivyo vitafuatana kwa mfululizo mpaka utahisi umemkosea Mungu wako.

Wahenga walisema siku ya kufa nyani, miti yote huteleza. Walikuwa hawawazungumzii nyani wa porini, walikuwa wanazungumzia mimi na wewe.

#iThinkSo

Uwe na furaha.

Uwe na afya.

Uwe huru kutoka kwenye matatizo.

Upate amani.

Rogers Katuma

Financial Artist, Senior Adventurer, Occasional Storyteller, and Amateur Golfer


Discover more from iThinkSoo

Subscribe to get the latest posts sent to your email.