Kwenye hatua mbalimbali za maisha yangu nilikuwa napata malengo tofauti ambayo nilikuwa nataka kuyafuata na kutimiza. Kuishi maisha kwenye mazingira magumu ilinipa malengo ya kutaka kufanikiwa na kusaidia wengine maishani.
Nakumbuka vipindi vyote ambavyo ndugu na watubaki walijitokeza kunisaidia mimi, mama au familia yangu katika kipindi kigumu. Msaada wao ulijenga mbegu kubwa sana ndani yangu ya kutaka kusaidia watu nikifanikiwa.
Nakumbuka kuanza kupenda kusoma na kujifunza vitu vipya kwenye maisha wakati mama yangu alivyotengeneza maktaba ndogo chumbani kwangu. Nikagundua nguvu kubwa iliyopo kwenye kujua vitu na kujifunza. Niligundua kuwa kuna vitabu kwa ajili ya kila kitu duniani.
Vitabu kuhusu chanzo cha ulimwengu, maisha, dini, urafiki, utajiri, biashara, mahusiano, jamii, siasa, sayansi na vingi zaidi. Hii ikanitengenezea ndoto ya kutaka kuwashirikisha watu wengi zaidi wapende kusoma na kujifunza zaidi.
Kukua kwenye maisha ya umasikini ukiwa umezungukwa na majirani wenye uwezo na wanaendesha biashara zao ikanipa ndoto ya mimi pia kutaka kuja kufanya biashara mbeleni. Nilikuwa sijui nitaanzaje lakini nikajipa ndoto ya siku moja kujaribu.
Ilinivutia sana kuona namna wajasiriamali na wafanyabiashara walikuwa na uwezo wa kutatua matatizo ya jamii, kupata kipato, kujenga utajiri na bado kuwa na uwezo wa kusaidia watu na kuwa na uhuru wa muda na maisha yao.
Wakati nipo chuo mwaka wa kwanza rafiki yangu mmoja alipata nafasi ya kufanya mafunzo ya vitendo kwenye ofisi moja kubwa sana duniani ya maswala ya uhasibu na ukaguzi, alikuwa anipa stori nzuri na za kufurahisha kuhusu maisha ya ofisini. Na mimi nikapata ndoto ya kutaka kujaribu maisha yale.
Ulipofika mwaka wa pili chuoni na mimi nikapata nafasi ya kuchukuliwa kwenye ile ofisi kwa ajili ya mafunzo ya vitendo. Na kila alichokuwa anasema rafiki yangu kilikuwa kweli. Ile ikanipa mimi lengo la kutaka kuajiriwa kwanza kwa miaka kadhaa kabla ya kuacha na kuanzisha na kuendeleza biashara zangu na kuwa mjasiriamali kama wale majirani wakati nakua.
Wakati nakua nililelewa na mama peke yake. Baba yangu hakuwahi kuwa kwenye maisha yangu na ile ilinipa hamasa kuwa siku nikiwa na uwezo wa kuanzisha familia nitajitahidi niwe mume bora na baba bora. Nitengeneze familia yenye upendo na umoja kwa wakati wote.
Pia wakati nakua nilikuwa napenda sana kucheza mpira, ingekuwa inaruhusiwa kuchagua mchezo mmoja ambao ningefanya ndo maisha yangu na chanzo cha kipato changu tangu utotoni basi ningecheza mpira wa miguu.
Hayo ni baadhi ya malengo ambayo nimeshawahi kuwa nayo kwenye maisha katika nyakati mbalimbali na ni ndoto ambazo bado nipo nazo na nilijaribu kufanyia kazi kwa njia tofauti tofauti.
Kuwa tajiri, niwasaidie watu kwa hali na mali, niwasaidie watu kusoma na kujifunza vitu mbali mbali. Kupata uzoefu wa maisha ya kuajiriwa, pia kuja kuanzisha baishara. Kuanzisha familia, kuwa baba bora na mume bora. Kucheza mpira wa miguu na pia kuendelea kujifunza vitu.
Mwanzoni nilijua kuwa naweza kufanikisha hivi vitu vyote, na nikaanza kuvifanyia kazi vyote kwa pamoja. Nikaongeza jitihada darasani kwa kusoma zaidi ili nifaulu mpaka nifike chuo. Nikaanza pia kucheza mpira wa ushindani na kukubali kocha awe ananifundisha kila jioni.
Nikagundua kila nikitoka kwenye mazoezi nakuwa nimechoka sana na kuishia kulala. Siku ya pili yake asubuhi pia nakuwa mchovu sana nakosa umakini vipindi vya asubuhi darasani. Matokeo yangu yakaanza kuwa mabovu kwa kasi sana. Nikagundua hivi vitu haviwezi kwenda pamoja.
Ikanibidi nichague kati ya kucheza mpira wa ushindani, kufanya mazoezi kila siku au kusoma kwa jitihada, kwenda maktaba na kuwa msikivu darasani asubuhi. Ningeweza kufanya chochote kati ya hivi viwili lakini nisingeweza kufanya vyote. Nikachagua kusoma kwanza, mpira utasubiri.
Nilianza moyo wa kusaidia watu tangu nikiwa mdogo sana. Nilianza kusaidia watu kwa kuwafundisha darasani ili wafaulu, kuwaazima vitabu na vitu mbalimbali. Nikagundua natumia muda mwingi kufundisha watu kushinda kujisomea, na walikuwa hawaishiwi vitu vya kufundishwa, ikanibidi nichague kujisomea ili nifaulu na niwe na uwezo wa kufundisha wengine au wote tufeli kwa kutumia muda mwingi kufundishana vitu vile vile. Nikachagua kujisomea.
Nilipoanza kupata fedha kidogo nilikuwa natoa sadaka, nasaidia ndugu, jamaa na marafiki sana. Nikagundua kuwa bajeti yangu ilikuwa inaisha mapema sana kiasi ambacho ilikuwa inaniacha na madeni mengi sana.
Kuna muda nikawa nakopesha watu na hawarudishi. Kuna ndugu na marafiki wakawa hawaishiwi matatizo ya kifedha, kila wakikuona au wakiwasiliana na wewe ni wanashida ya fedha. Wakatengeneza utegemezi kwangu ambao sikuwa na uwezo wa kutimiza muda wote.
Ikanibidi nichague kujiendeleza mimi kifedha kwanza au kusaidia watu kidogo nilichokuwa nacho na wote tukose tuishie kwenye madeni na ukosefu wa hela. Nikachagua kujisaidia kwanza mimi.
Nilianzisha biashara ya pili nikiwa mwaka wa pili chuoni, nikawa natumia muda mwingi nje ya chuo kwenda kutafuta wateja, kujifunza kuhusu biashara na kukutana na watu wengine wanaofanya ujasiriamali.
Hiyo ikafanya nikose vipindi vingi chuoni na kufeli mitihani mingi sana. Matokeo yangu yakashuka sana na ikabaki kidogo tu kufukuzwa chuo. Ikanibidi nichague kufanya biashara moja kwa moja niache chuo au nisubiri kumaliza chuo mwaka mmoja uliobaki na kufanya biashara. Nikachagua kumaliza chuo na kupunguza nguvu kidogo kwenye biashara.
Nilipomaliza chuo nikaanza kuwekeza nguvu nyingi kwenye biashara. Nikakubali kuajiriwa pia kwa sababu nilikuwa na malengo ya kupata ujuzi na uzoefu wa kuajiriwa na kukusanya mtaji nikiwa kazini ili nikuze biashara yangu.
Nikafanikiwa kufanya kazi vizuri na kupata mshahara uliosaidia kuongeza mtaji kwenye biashara yangu, lakini sikuwa napata muda wa kwenda kwenye biashara na kuisimamia vizuri. Ikanibidi nichague kazi au biashara, siwezi kufanikiwa kwa kufanya vyote.
Nikajipanga vizuri kuweka akiba kidogo na kuchagua muda sahihi wa kuacha kazi na kufanya ujasiriamali moja kwa moja.
Ndoto yangu ya kuwa na familia bora, baba bora na mume bora ilinifanya nichukulie mahusiano kwa uzito mkubwa sana. Nikagundua kuwa kujenga mahusiano inahitaji uwekezaji wa muda na fedha.
Unahitaji uwe na muda wa kuongea na mwenzako, uwe na muda wa kuwa pamoja na pja uwe na fedha za kufanya vitu pamoja au kumnunulia zawadi.
Nikagundua ni ngumu sana kuwa na mahusiano wakati ambao nimetoka kuacha kazi, nina biashara changa ambayo inahitaji muda wangu na kila senti ninayokuwa nayo. Ikanibidi nichague kati ya biashara yangu changa au mahusiano machanga. Siwezi kukwambia nilichagua nini, ila jua kuna kitu kilipungua ili kingine kisimame.
Mapenzi yangu ya kufundisha watu, kusimulia stori za mafunzo na hekima yalinifanya nifikirie kuanzisha biashara ya utangazaji au chombo cha habari. Ikanifanya nipende kuandika, kuongea mbele za watu na kujiunga na mitandao ya jamii.
Mapema sana nikagundua ni rahisi kusimulia na kufundisha watu vitu ulivyopitia kushinda kusimulia na kuelezea vitu vya watu wengine. Sikuwa na amani ya kufundisha na kusimulia maisha na mafaniko ya watu na kuyafanyia biashara.
Nikachagua kuanza kuishi maisha yangu kwanza, kupata uzoefu, hekima na stori za kutosha kabla ya kuanza kuandika.
Nikaanza kufuata ndoto zangu, kutafakari maamuzi na vitu ninavyojifunza na kuvirekodi. Nikipata muda nikawa naandika sehemu, na hivi ndio vitu unavyovisoma kwenye www.ithinksoo.com.
Ilipofika hapa, nikagundua kuwa nina uwezo wa kufanya kila kitu duniani. Nina uwezo wa kufuata malengo yangu yote na kuyatimiza lakini ikanibidi nikubali kuwa siwezi kufanikisha vyote kwa wakati mmoja. Siwezi kufanya kila kwa wakati mmoja.
Katika kila kitu ninachokitaka inabidi nikubali kuacha kitu kimoja. Ni miongoni mwa maamuzi magumu sana ambayo kila mtu inabidi ayafanye kwenye maisha yake.
Inabidi kuchagua kitu kimoja ambacho utakipa nguvu, jasho na muda wako kwa muda mrefu mpaka kifanikiwe. Na hicho kitu kikifanikiwa kinakuandaa na kukupa nafasi nzuri ya kujenga kitu kingine.
Ukifanikiwa kitu kimoja, kitakupa rasilimali na uwezo wa kufanya kingine, na kingine na hivyo ndio namna ya kuishi maisha. Kuna vitu vichache sana ambavyo vinaweza kwenda pamoja kwa wakati mmoja.
Hivi ni vitu ambavyo inabidi viwe vipaumbele vyako kwenye maisha. Na ni vichache sana. Vitu vingine vyote unaweza kuvifanya na kufanikisha lakini sio kwa wakati mmoja.
#iThinkSo
Uwe na furaha,
Uwe na afya,
Uwe huru kutoka kwenye matatizo,
Uwe na amani
Kama kuna kitu umejifunza, mtumie mtu mmoja unayemjali na anahitaji kuisoma hii.
Rogers Katuma
Financial Artist, Senior Adventurer, Occasional Storyteller, and Amateur Golfer
