Uvumilivu ni kuendelea kuweka juhudi wakati ukiwa haufikirii matokeo.

Nilipoanzisha kampuni yangu ya kwanza miaka tisa iliyopita, nilikuwa sina mategemeo yeyote makubwa. Jina la kampuni lilianzishwa na baba yangu kabla hajafariki. Alikuwa na ndoto ya kuanza biashara baada ya kustaafu kazi. Alisajili jina, na kuanza taratibu za kufungua biashara kabla umauti haujamfika.

Kuendeleza pale alipoishia nikaamua kuchukua jina lake la biashara na kufungua kampuni nyingine. Nilikuwa na wazo la kuanzisha huduma kama ya Uber au Airbnb kwenye maswala ya kufua nguo kwa mashine. Wazo lilikuwa kutengeneza programu ya simu ambayo watu wanaweza kuweka oda ya kufua. Nguo kufuatwa na kurudishwa kwao.

Wazo hili lilinijia usiku wa mwaka mpya miaka tisa iliyopita wakati nikiwa mapumziko Bagamoyo. Siku iliyofuata tu nikarudi nyumbani na kuanza kufanyia kazi wazo lile. Nilikuwa sijui kitu chochote kuhusu kutengeneza programu kama ile. Nikaingia kwenye mitandao na kuanza kujifundisha.

Ndani ya siku nne nikafanikiwa kutengeneza programu ile na ilikuwa tayari kupatikana kwenye simu za watu wote duniani. Wakati nafanya hivi vitu sikuwa najua itanifaidisha nini wala itanipeleka wapi. Niliamini kuwa nikifanyia kazi wazo langu basi matokeo yatakuja mbeleni au nitajifunza kitu.

Nikaanza kuwatumia majirani, marafiki na baadaye kwenye mitandao ya jamii. Nikaanza kutafuta njia ya kuingia ubia na wafanyabiashara wa kufua kwa kutumia mashine pia. Nilikuwa sijui chochote kuhusu upande wao wa biashara, lakini nilikubali kuweka juhudi.

Kwakuwa nilikuwa sina wateja na sijui chochote kuhusu biashara yao sikuweza kupata ubia na mfanyabiashara yeyote wa kufua na mashine. Nikamuomba rafiki yangu ambaye alikuwa na mashine ya kufulia nyumbani kwake. Nikajifunza kwenye mitandao kuhusu kufua kwa mashine na kuwa tayari ikiwa wateja watatokea.

Wiki kadhaa mbele nikaanza kupata oda za watu wakihitaji kufua. Nikaanza kwa kuwa nazifuata nguo mwenyewe, kwenda kuzifua kwa rafiki yangu na kuwarudishia wateja. Watu wakaanza kuijua zaidi ile programu na wateja wakaongezeka.

Nikapata wazo la kuanza kutafuta wawekezaji ili kukuwa na kuwafikia watu wengi zaidi. Ndani ya miezi mitatu wateja walikuwa wakutosha, nilipata mfanyabiashara moja aliyekubali kufanya kazi na mimi yeye alikuwa na mashine za kufulia. Wakiongezeka wawekezaji tungekuwa zaidi, lakini sikuwa na namna ya kuwafikia hivyo nikaendelea tu kuweka juhudi.

Muda wote huu nilikuwa naweka juhudi ya kuikuza biashara nikiwa sina mategemeo yeyote itanifikisha wapi. Miezi mitano mbele nilialikwa kwenye tukio moja la ujasiriamali la biashara changa. Mimi nilienda pale kufanya matangazo na mauzo. Nikakutana na mtu aliyependa sana wazo langu.

Nikapewa nafasi ya kuelezea wazo langu mbele ya wawekezaji. Nikaelezea vizuri sana na kuonyesha historia kuanzia wazo lilivyokuja Bagamoyo, kutengeneza programu mwenyewe, kuanza na mashine ya kufulia ya rafiki yangu mpaka tulipokuwa muda ule.

Wakatokea wawekezaji wawili wakasema wapo tayari kununua hisa kwenye kampuni ili kuikuza zaidi. Wakanipatia dola elfu kumi na tano, ambazi ni sawa na takribani milioni arobaini taslimu ya hela za kitanzania kwa wakati huu.

Kitu kikubwa nilichofaidika kwenye ile biashara haikuwa ile milioni arobaini ya uwekezaji, ilikuwa ni funzo lililotokana na kuanza wazo mpaka kufika pale. Ilinifundisha kuwa ukiweka juhudi kwenye kitu kwa miezi, mwaka au miaka hauwezi kuchagua lini matunda yatakuja. Na hapo ndio kipimo cha uvumilivu.

Dunia ina njia zake za kulipa uvumilivu, na hizo njia binadamu hatuzijui. Tunachotakiwa sisi kukijua ni kuwa uvumilivu wa kweli ni kuendelea kutia juhudi bila kujali matokeo. Ukiweka juhudi na kusubiria matokeo ni rahisi kukata tamaa na kuacha.

Utapitia vitu vingi kwenye maisha ambavyo utaweka juhudi lakini hautaona matokeo au matunda kwa muda uliotegemea. Haimaanishi kuwa havitakuja, vitakuja lakini sio kwa wakati wako au namna unayoitaka.

Ukiwa kazini unaweza kufanya kazi kwa bidii kushinda kila mtu. Ukawa wa kwanza kuingia ofisini na wa mwisho kutoja. Ukianza kusubiria kuongezwa cheo na mshahara kwa juhudi zako utakata tamaa kabla havijafika. Endelea kuweka juhudi kwa sababu ipo chini ya uwezo wako. Kupandishwa cheo na mshahara haipo kwenye uwezo wako.

Unaweza kuwa na kipaji kikubwa sana, unafanyia mazoezi kipaji chako lakini hauoni matunda ya kipaji chako. Ukianza kusubiria matunda na matokeo yatakuja lini utakata tamaa. Juhudi na kufanya kazi kwenye kipaji chako ipo chini ya uwezo wako. Matokeo na matunda havipo chini ya uwezo wako, unahitaji uvumilivu kuendelea.

Kwenye mahusiano unaweza kufanya kila kitu sahihi. Ukampenda mtu, uka msikiliza, uka mheshimu na kujitolea kila ulicho nacho. Lakini ukitegemea na yeye afanye kama wewe utakata tamaa. Kuwa mwenza bora ipo chini ya uwezo wako, mwingine kuona thamani yako na yeye kuwa bora haipo kwenye uwezo wako. Atabadilika au utaletewa mwingine, lakini inahitaji uvumilivu.

Hii ipo hivyo kwenye kila kitu. Kwenye biashara, shule, ndoto zetu na hata siasa. Wewe jukumu lako ni kuendelea kuweka juhudi na kuvumilia. Kuacha kutegemea matokeo fulani au matunda fulani yaje kwako kwa wakati fulani au namna fulani kwa sababu ya juhudi fulani.

Uvumilivu wa kweli ni kuweka juhudi bila kuangalia matokeo na matunda.

#iThinkSo

Uwe na furaha.

Uwe na afya.

Uwe huru kutoka kwenye matatizo

Uwe na amani.

Kama kuna kitu umejifunza, mtumie mtu mmoja unayemjali.

Rogers Katuma

Financial Artist, Senior Adventurer, Occasional Storyteller, and Amateur Golfer


Discover more from iThinkSoo

Subscribe to get the latest posts sent to your email.