Kama unahitaji kuhamasishwa kuanza jambo, basi umeshafeli.

Zamani nilikuwa natafuta njia zozote za kupata hamasa kwenye maisha. Kutokea kwenye familia ya kipato cha chini, kuzungukwa na umasikini na ndugu wasio na kipato ilikuwa inakatisha tamaa. Kila nilipopata hamasa au moyo kidogo nilikuwa naona maisha kwa jicho la utofauti.

Nikaanza kuwa mpenzi mkubwa sana wa vitu vyote vilivyogusa masuala ya hamasa, mawazo chanya na fikra sahihi kufanikiwa kwenye maisha. Na nikaanza kuwapatia ndugu, jamaa na marafiki pia. Nikaanza kutuma vingine kwenye mitandao ya kijamii.

Sikuishia hapo tu, nikaanza kuandaa matukio mbalimbali na kualika watu kuja kuongea au kusikiliza mambo ya hamasa na kubadilisha maisha. Nilipenda sana mada ya kutokukata tamaa, kufuata ndoto na kuamini kuwa kuna siku itawezekana tu.

Siku moja nilihudhuria sehemu ambayo mgeni rasmi alikuwa ni mfanyabiashara mkubwa sana afrika mashariki. Kuna mtu alimuuliza swali, “ni sentensi gani ambayo unaweza kuniambia ili nipate hamasa na kutoka kukata tamaa kwenye safari ya ujasiriamali?”

Yule mgeni rasmi alimuangalia machoni, bila tabasamu wala chembe za hisia za kujali akamjibu,”kama unahitaji kuhamasishwa ili kuanza kufanya kitu basi umeshashindwa.”

Akarudi kututazama wote mle ukumbini kisha akasema “mwenye swali jingine, la maana zaidi?”

Ukumbi mzima ulikuwa kimya.

Nilipotoka pale ukumbini lile jibu lilinikaa kichwani muda wote. Niliendelea kutafakari kwa undani sana lile jibu lake, “kama unahitaji kuhamasishwa ili kuanza kufanya kitu basi umeshashindwa.”

Nikaona ukweli kwenye maisha yangu, kwa sasa nilikuwa nahangaika kutafuta hamasa za kuanza kufanya vitu, miaka imepita na sina chochote cha kuonyesha ukiachana na hamasa.

Nikagundua hamasa na fikra chanya zinasaida kujisikia vizuri kwa muda au kuanza kitu, lakini hazina msaada wa kuendeleza. Nikakumbuka msemo mmoja maarufu wa Zig Ziglar, unasema, “hamasa ni kama kuoga, sio kwa kuwa umeoga leo basi hauhitajiki kuoga kesho”

Nikagundua kuwa kila siku unahitaji hamasa, kama ambavyo kila siku unahitaji kuoga. Lakini ni ngumu kuwa na hamasa na kuwaza chanya pale mambo yanapokuwa magumu. Inahitajika sababu nyingine ya nguvu na muhimu zaidi kufanya uendelee kupambana na kutokata tamaa.

Nikagundua kuwa sivutiwi na misemo mizuri au hamasa za watu. Navutiwa na stori za watu ambao walianza chini wakiwa hawana kitu na kutimiza ndoto zao. Wakiwa wanaelezea maisha yao na stori zao mimi ndo huwa nahamasika.

Nikagundua kuwa watu tofauti huwa wanahamasika kwa vitu tofauti. Hivyo kutumia muda mwingi kutafuta hamasa sio sawa. Nahitaji kitu kingine chenye nguvu zaidi kunisaidia mimi kufuata malengo yangu.

Nikagundua kujua dhumuni la mimi kuwa duniani, ndoto zangu na malengo yangu ni vitu vyenye nguvu sana ya kunifanya niendelee kupambana hata mambo yakiwa magumu. Sihitaji hamasa ya mtu yeyote kubadili maisha yangu na ya familia yangu. Umasikini, dharau, mateso na manyanyaso mama yangu aliyopitia kunilea ni hamasa tosha milele.

Nikagundua nikijibu maswali yafuatayo, nitakuwa na sababu ya kuanza na kuendeleza;

Sababu ya kwanini naanza jambo fulani?

Kwanini nataka kufanikisha jambo fulani?

Kwanini nisikate tamaa hata mambo yakiwa magumu?

Mafanikio yanahitaji dhumuni, lengo, nidhamu, uvumilivu na sio kupata tu hamasa. Nikaelewa kwa undani kwanini yule mgeni rasmi alisema kama unahitaji kuhamasishwa kufanya jambo basi umeshashindwa.

Kama unahitaji rafiki zako wakuhamamasishe kuanza mazoezi basi wakiacha na wewe unaacha mazoezi.

Kama unahitaji wazazi wakupe hamasa ya kusoma au kufanya kazi basi wakiacha na wewe unafeli.

Lakini siku ukaamka unaumwa na daktari akakwambia usipofanya mazoezi utapoteza maisha ndani ya miezi sita, nina imani utakuwa unakuwa wa kwanza kwenda kwenye mazoezi na wa mwisho kutoka.

Kama mama yako mzazi unayempenda na kumjali ni masikini, anadharauliwa na kunyanyaswa na umasikini, hautasubiri mtu akupe hamasa ya kusoma wala kufanya kazi kwa bidii.

Kwenye maisha yako jiulize dhumuni, malengo na ndoto zako na hautahitaji hamasa kutoka kwa mtu yeyote kuanza, kuendelea, kuinuka tena baada ya kuanguka hata mara saba.

Kama kuna kitu kwenye maisha yako sasa hivi unasubiri hamasa, naomba nikwambie, nikikuangalia machoni, UMESHAFELI.

#iThinkSo

Uwe na furaha

Uwe na afya

Uwe huru na matatizo

Uwe na amani

Kama kuna kitu umejifunza, mtumi mtu wako wa karibu mmoja unayemjali

Rogers Katuma

Financial Artist, Senior Adventurer, Occasional Storyteller, and Amateur Golfer


Discover more from iThinkSoo

Subscribe to get the latest posts sent to your email.