Wapishi wazuri wanajua kiwango sahihi cha chumvi

Kukua kwangu kote nimezungukwa na wanawake. Na sio tu wanawake wa kawaida, bali wale waliopenda na kujua sana kupika. Bibi yangu alikuwa anafanya biashara ya vitumbua kwa maisha yangu yote niliyomjua. Nakumbuka wakati wa likizo sisi wajukuu ndio tulikuwa wauzaji wake.

Mama yangu ni miongoni mwa wapishi wangu bora kabisa duniani. Na hii ni kitu cha kutegemea kwa sababu bibi aliyekuwa na biashara ya vitumbua ni mama yake. Kajifunza kutoka kwa mwalimu bora sana.

Mwanzoni nilikuwa nachukia kutumwa vitu jikoni wakati bibi au mama wanapika. Baada ya muda nikaanza kupenda kuangalia na kujifunza. Pia kulikuwa na fursa ya kuonja vitu vingi sana, hususani siku za pilau na nyama.

Wakati naanza wote walikuwa na tabia ya kunituma vitu bila kunielezea. Nitaambiwa nikate vitunguu, au nyanya au kukuna nazi basi. Wataendelea kuweka nyanya au nazi bila kusema kitu.Baada ya kuona naanza kupenda mapishi wakaanza kunielezea.

Nikaanza kujua mapishi ya aina mbalimbali. Nikajifunza kuhusu viungo na namna ya kuvitumia kwa kila aina ya mapishi. Kuna kitu kimoja kilikuwa juu ya vitu vyote kila mara, chumvi. Mara ya kwanza nilimsikia bibi akimsema dada yangu kuhusu chumvi, alimwambia “ Haijalishi chakula chako kizuri kiasi gani, chumvi ikizidi au isipokuwepo inaharibu kila kitu”

Sikuwahi kumsikia mama akimsema mtu kuhusu chumvi lakini kuna siku aliwahi kusema “wapishi wazuri wanajua sana kuhusu chumvi.” Nikaanza kufuatilia kwa umakini sana kila muda wa kuweka chumvi kwenye chakula.

Kwa miaka mingi sana bado nilikuwa sielewi vigezo vyao vya chumvi. Kuna siku mama alikuwa anaweka kijiko kidogo cha chumvi na haongezi tena. Na chakula kikitoka kinakuwa kizuri sana. Kuna siku alikuwa anaweka kidogo, anaonja mchuzi, anaongeza tena, anaonja tena na chakula kikitoka kinakuwa kizuri kabisa.

Mara zote nilikiwa nawauliza vigezo vyao vya chumvi na sikuwa naelewa majibu yao. Kuna siku mama akaniweka chini na kunieleza vizuri filosofia ya chumvi kwa uzoefu wake. Akasema, “hamna kiwango sahihi cha chumvi kwenye chakula, kiwango unachopendelea wewe kinaweza kuwa kingi au kidogo kwa wengine. Mbinu sahihi ni kuweka kiwango cha kutosha kuleta ladha na kuweka chumvi nyingine mezani. Hauwezi kumridhisha kila mtu.”

Nikaanza kufanyia mazoezi elimu ile na ikafanya kazi. Na mimi nikawa najua kiwango cha kuweka kwa kuangalia maji ya mboga au wali. Kuna muda naonja mara mbili na kuna muda sina haja ya kuonja mpaka chakula kiive.

Miaka mingi ikapita na nikagundua kwenye maisha pia elimu ile inatumika. Watu waliofanikiwa kujenga maisha yao kwa namna yeyote ile wanatumia mawazo ya wapishi bora. Wanajua kiwango sahihi cha chumvi pia. Na wanajua kuwa hamna kiwango kimoja kwa ajili ya kila mtu.

Wanapofanya maamuzi wanatambua kuwa sio kila mtu atapenda maamuzi yao na sio kila mtu atachukizwa. Lakini wapo tayari kufanya maamuzi hayo na kuishi nayo. Wakipokea ushauri mzuri sawa, wakipokea lawama ni sawa pia, ni kama kuweka chumvi ya ziada mezani na kutoa pole kwa atakayesema chumvi imezidi kwenye chakula.

Wakati unajenga maisha yako ni upo kwenye safari ya kujipika, na kiwango sahihi cha chumvi ya maisha yako ni muhimu. Hauwezi kumridhisha kila mtu na hauwezi kumkwaza kila mtu. Jitambue wewe, tambua malengo na ishi maisha yako.

Kuna watu watakuja kukusaidia na kukupeleka mbele, hawa ndo wale wataonja chakula chako na kusema chumvi haitoshi, watachukua chumvi mezani na kuongeza kwenye chakula chako ili wakifurahie. Halafu kuna wale ambao watakupinga na kukulaumu, hawa ni wale watakaosema chumvi imezidi na hawataki kula.

Ukiwa mpishi, haujui mlaji wako atakuwa wa aina gani, na mpishi mzuri haogopi kupika sababu ya lawama ya chumvi. Wewe ni mpishi mzuri wa maisha yako, usihofu kuhusu watu wengine.

#iThinkSo

Uwe na furaha.

Uwe na afya.

Uwe huru kutoka kwenye matatizo

Uwe na amani

Kama kuna kitu umejifunza, mtumie mtu mmoja unayemjali.

Rogers Katuma

Financial Artist, Senior Adventurer, Occasional Storyteller, and Amateur Golfer


Discover more from iThinkSoo

Subscribe to get the latest posts sent to your email.