Kila kitu kina gharama yake, lakini sio kila gharama inaonekana.

Mwaka jana, madaktari walinipima na kuniambia kuwa nina bakteria wanaoitwa H.pylori wanaosababisha vidonda vya tumbo. Bakteria hawa walikuwa wanakula kuta za utumbo na kusababisha vidonda.

Mara nyingi ndio sababu kubwa sana ya watu kupata vidonda vya tumbo au hata kansa ya tumbo. Kabla ya siku hii, sikuwahi kusikia neno H.pylori kwenye maisha yangu.

Maumivu niliyokuwa nayapata kabla ya kwenda kwa daktari yalikuwa makubwa sana. Sikuwa na kipingamizi chochote cha kuhusu ushauri wa daktari. Nilikuwa tayari kufuata maelekezo yote ya matibabu nitakayopewa.

Ingawa nilikuwa tayari kufuata maelekezo yote, sikutegemea kuona kiasi cha vidonge na dawa nilizokuwa natakiwa kunywa kutibu bakteria watoke. Watu wa duka la madawa walinipa kifurushi chenye dawa mchanganyiko na kuanza kuniandikia maelezo ya namna ya kutumia. Nikahesabu kwa haraka kulikuwa na zaidi ya vidonge arobaini.

Haikuishia hapo tu, akaniongezea vidonge vingine ishirini na sita vya maumivu. Kisha akaniongezea vidonge vingine thelathini vya kuzuia kuta za tumbo zisidhurike zaidi na vyakula na vinywaji. Kisha nikatajiwa vyakula na vinywaji vya kuacha kutumia na vipi vya kuanza kutumia.

Nikiwa bado na mshtuko, daktari akasema kuwa ile ilikuwa ni dozi ya kwanza. Ikiisha itabidi nirudi hospitali kupima tena, na kama hali itakuwa haijabadilika basi nitapewa dozi ya pili kama ile.

Baada ya wiki sita, hali yangu ilikuwa mbaya zaidi kushinda mara ya kwanza. Maana yake ile dozi haikunisaidia kabisa. Nikarudi hospitali kwa vipimo zaidi na dozi ya pili. Daktari akaniambia ni kawaida kwa wale bakteria kuzoea dawa na kushindwa kutoka kwa dozi ya kwanza. Alikuwa na imani kuwa dozi ya pili itawaondoa kabisa na nitapona.

Miezi miwili ikapita, na dozi ya pili nayo ikaisha, hali yangu haikubadilika. Ikanibidi nirudi tena hospitali kufuata ushauri wa daktari. Daktari akasema mara nyingi dozi ya pili huwa inatibu, ila kuna baadhi ya watu inahitajika na dozi ya tatu kutatua tatizo kabisa. Akasema mimi ni miongoni mwa wale wachache watakaohitaji dozi ya tatu.

Akanipatia maelekezo ya kwenda duka la dawa na kuchukua dozi ya tatu, akanipa na aina nyingine ya dawa za kutuliza maumivu. Nikarudi nyumbani na kuanza kutumia dawa zile. Hali yangu haikubadilika sana kwa miezi mitatu.

Kuna siku usiku sana, maumivu ya tumbo yalirudi kwa kasi kubwa sana. Nilikuwa siwezi kusimama wala kulala. Kila dawa ya maumivu niliyokuwa nayo ndani haikusaidia kutuliza maumivu siku nzima. Uvumilivu ukanishinda, ikanibidi aubuhi niende duka la dawa la karibu nitafute dawa nyingine ya maumivu.

Nesi wa duka la dawa akaniuliza nataka dawa ya maumivu kwa ajili ya nini, nikamuelezea historia yangu ya maumivu, bakteria wa H.pylori and dozi zote nilizotumia. Akaniangalia kwa huruma sana, kisha akasema, “unalipia gharama kubwa sana kushinda unayoiona kwa kunywa hizo dawa”

Mwanzoni nilifikiria ana maanisha kuwa bei niliyokuwa nalipia ya dawa za mara ya kwanza kwenye duka la dawa la mwanzo ilikuwa ni kubwa. Nikafikiria kuwa niliibiwa sana kama walinifanyia hivyo kwa dozi zote tatu.

Wakati naendelea kufikiria maumivu ya kuibiwa kama alivyosema, akaniambia, “mimi nilikuwa na vidonda vya tumbo pia, gharama niliyolipia kwa kunywa dawa ilikuwa kubwa kushinda nisingetumia”

Hapo ndio nikaelewa kuwa alikuwa hamaanishi bei ya dawa madukani, alikuwa ana maanisha gharama au hasara za kunywa zile dozi zote tatu na bado bakteria wa H.pylori walikuwa hawajaondoka. Aliniona namna nilivyokodoa macho nikisubiria maelezo zaidi ya historia yake, akatabasama, akakohoa kidogo kulainisha sauti na kunipa mkasa wake.

“Na mimi nilikuwa na vidonda vya tumbo,” alianza kusimulia huku akivuta kiti na kukaa. “Mimi vidonda vyangu vilikuwa vikitibuka ilikuwa ni maumivu makubwa sijawahi kuyasikia kwenye maisha yangu. Mara nyingi nilikuwa napoteza fahamu.”

Ikanifanya mimi nijione natania na maumivu yangu, sijawahi kupoteza fahamu kwa maumivu. Umakini ukaniongezeka zaidi kusikiliza stori yake. “Mimi nilikuwa kama wewe, nilitumia dozi ya kwanza mpaka ya tatu bila kupona. Nikabadilisha hospitali na madaktari zaidi ya watano na sikupata nafuu.”

Nikaanza kupata hofu kuwa na mimi naelekea kuwa kama yeye, maana sioni nafuu na nipo dozi ya tatu. Na hapo bado nilikuwa sijabadilisha madaktari na hospitali. “Hali yangu ikawa mbaya zaidi baada ya kuanza kupata na madhara ya kunywa dozi nyingi sana za vidonda vya tumbo,” akaendelea kusimulia.

“Nikaanza kukosa usingizi, kuzimia kukaongezeka, ngozi ikaanza kutoka vipele na kuwasha, nikawa natoka jasho sana na kupata shida kupumua na vingine vingi sana. Daktari wakawa waniambia hizo ni madhara yanayofuata kwa kutumia dozi nyingi kushinda uwezo wa mwili kuvumilia.”

Hapo ndio aligundua kuwa gharama ya kutumia zile dawa ni kubwa kushinda pesa alizokuwa analipa hospitali na maduka ya madawa. Lakini alikuwa hana suluhisho jingine hivyo ilibidi aendelee.

Maisha yake yalibadilika miaka kama minne nyuma, ni ambapo alipoteza tena fahamu akiwa mazingira ya karibu na kijijini kwao. Familia yake ikampeleka hospitali na kumpa huduma ya kwanza. Akakutana na nesi mmoja mzee sana, ambaye ushauri wake ulibadilisha maisha yake.

“Shida ya tumbo lako ni aina ya maisha uliyonayo. Tumia muda mwingi kuhakikisha unakula matunda, mboga za majani na vyakula vyenye asili ya mbegu. Pumzika kwa wakati na jizuie sana kunywa dawa kila ukisikia maumivu. Sio suluhisho la haraka sana, lakini baada ya muda mrefu itakusaidia sana”, yule nesi mzee alimwambia.

Kwakuwa alishajaribisha aina mbali mbali za dawa na haikuwa na msaada, akamsikiliza yule nesi mzee. Akafuata ushauri wake kama ambavyo watu wanafuata miongozo ya dini. Akaacha kutumia zile dawa nyingi kila akisikia maumivu na kubadilisha vyakula na vinywaji.

Baada ya miezi kadhaa, maumivu yakaanza kuwa ya kawaida, akaacha kupoteza fahamu na hakuwahi kurudi tena hospitali kwa ajili ya vidonda vya tumbo. Muda huu ananisimulia hii stori ilikuwa imepita miaka minne. Akaniambia kama na mimi nimetumia mpaka dozi ya tatu na sijapona, basi ni muda wa kusikiliza ushauri wa yule nesi mzee.

Akaniambia gharama ninayolipia ni kubwa sana kushinda bei ya dawa. Nikakumbuka kuwa ni kweli wiki chache nyuma na mimi nilianza kusikia mapigo ya moyo kwenda kasi sana bila sababu, kuanza kupata shida ya kupumua na hata muda mwingine kuhisi ninataka kuanguka.

Nikapata jibu kuwa zile dawa nilizokuwa nakunywa zilikuwa na madhara mengi sana kwenye mwili bila kujua. Sikuwa tu nalipia fedha, nilikuwa nalipia gharama nyingine zaidi ya bei ya dawa. Nikamshukuru yule nesi wa pale duka la dawa kwa kuwa mkweli na msaada kwangu, nikamwambia basi haina haja ya kuniuzia dawa tena.

Nikafuata ushauri wake, nikaanza kuongeza umakini wa vyakula nilivyokuwa nakula. Nikaanza kujizuia kuchukua dawa za maumivu kila tumbo likiuma. Haikuwa rahisi na haraka, lakini mwaka sasa umepita tangu nimepitia changamoto yeyote ya tumbo. Ina maanisha ilifanya kazi.

Kwenye maisha kila kitu kina gharama. Kuna zile ambazo haraka haraka zinaonekana na nyingine hazionekani kwa urahisi au mwanzoni. Ni jukumu letu kukaa chini na kutafakari kila aina ya gharama utakayolipia kwenye kila kitu unachokifanya.

Mahusiano au ndoa ni mazuri na yana faida sana, lakini gharama za kuwa kwenye mahusiano au ndoa hazionekani kwa haraka. Ukikaa na mtu aliyeamua kutoka kwenye mahusiano au ndoa atakuwa na majibu mazuri sana.

Kuanzisha biashara kuna faida nyingi sana, na wengi hudhania kuwa ukiwa na mtaji tu unaweza kuanza na kuifanya kwa raha. Uhalisia ni kuwa kuna vingi vinaendelea kwenye ujasiriamali na biashara zaidi ya tunavyoviona.

Kufanikiwa kazini na kupata promosheni ni kuzuri sana, wengine tunahisi kuwa tukifanya kazi kwa bidii tu inatosha. Wengi wanaofanikiwa hulipia gharama kubwa zaidi ya tunavyodhani. Mahusiano, afya zao za mwili na akili huwa sehemu ya gharama hizo.

Kuwa na mali, fedha, umaarufu au uongozi inaonekana ni raha sana na gharama yake ni ndogo tu. Uhalisia ni tofauti sana. Watu wenye mali, fedha, umaarufu na uongozi wanalipia gharama nyingi sana ambazo hazionekani kwa urahisi. Hofu ya kupoteza mali, fedha, umaarufu na uongozi huwa kwao kila siku.

Kutokuwa na imani na watu wa karibu yao. Kutojua watu wapya wanaokuja kwao kama wana nia njema au mbaya. Muda wote kuwa kwenye nafasi ya kuombwa vitu, msaada, ushauri na sapoti wakati hakuna atakayewachukulia kwa umakini wao wakiomba, wataonekana wanatania.

Funzo kubwa kwenye maisha yako ni kutumia muda wa ziada kukagua gharama halisi unayolipia kwa kila lengo na kitu unachotaka kukifanya. Watu wengi huishia kujuta baada ya kugundua malengo na ndoto walizokuwa nazo yamekuja kwa gharama kubwa kushinda walivyotegemea.

Ni sawa na mimi kufanikiwa kupunguza maumivu ya tumbo kwa vidonge vingi wakati nikijiletea tatizo la shida ya kupumua, kukosa usingizi na kuelekea kuanza kupoteza fahamu.

Uwe na furaha.

Uwe na afya.

Uwe huru kutoka kwenye mateso.

Upate amani.

#iThinkSo

Kama kuna kitu umejifunza, mtumie mtu wako wa karibu unayemjali na kumthamini naye ajifunze

Rogers Katuma

Financial Artist, Senior Adventurer, Occasional Storyteller, and Amateur Golfer


Discover more from iThinkSoo

Subscribe to get the latest posts sent to your email.