Les Brown, mwandishi wa vitabu, mzungumzaji na mfanyabiashara wa Marekani aliwahi kusema, “Mafanikio sio kitu unachokipata, mafanikio ni mtu unayekuwa.” Haupati mafanikio, unakuwa mtu mwenye mafanikio. Watu wengi hawajaweza kujua utofauti, na ndio sababu ya kushindwa kupanda kwenye ngazi ya mafanikio.
Baada ya muda, vitu vizuri huja kwetu sote, lakini vinakuja haraka sana kwa wale ambao hufanya kazi kwa bidii. Habari mbaya ni kwamba hatuna muda mwingi duniani kupata vitu vyote vizuri vinavyotakiwa kuja. Hivyo kuongeza jitihada ni njia sahihi ya kuongeza mafanikio. Kufanya kazi kwa bidii ni tabia, tabia ambayo hubadilisha wasiofanikiwa kuwa waliofanikiwa.
Kupandishwa cheo kazini mtu inabidi awe na ujuzi zaidi, uzoefu zaidi na thamani zaidi. Hapo watapata mshahara wa juu zaidi, faida nyingine juu ya mshahara, umaarufu na heshima kazini. Inamuhitaji huyo mtu kuwa zaidi ili kupata zaidi.
Kwa mwanasiasa kupata kura, kuheshimika, kupata mamlaka na wafuasi inamuhitaji kuwa mtu mwenye uwezo mzuri wa kuongea mbele za watu, kuwa na maono yake, kuwasiliana vizuri na watu wa makundi mbalimbali, kuwa na muonekano mzuri na kuaminika. Inabidi awe zaidi ya alivyo ili kupata zaidi ya alichonacho.
Kuwa mtu wa ziada ni kazi ngumu, inahitaji uvumilivu, kufanya kazi kwa bidii kwa muda mrefu bila matunda na kutokuwa na moyo wa kukata tamaa.
Mfano mzuri na maarufu ni wa mianzi yenye asili ya China. Ina shikilia rekodi ya kuwa miongoni mwa mianzi mirefu zaidi duniani. Lakini upandaji wake ni wa utofauti na una funzo kubwa sana. Mkulima akipanda mianzi hii, huwa inachukua miaka sita kwa mbegu kuchepua kutoka ardhini.
Hii ina maanisha ndani ya miaka sita, mkulima anamwagilia mbegu ya mianzi na haoni chochote. Mwaka wa sita ndio mbegu huchepua na kuonekana ardhini. Lakini maaajabu yake ni kwamba ndani ya wiki sita, mti huu hukuwa haraka sana na kukaribia urefu ambao hufanya mianzi hiyo kuwa mirefu zaidi duniani.
Watu wengi hatuna uvumilivu wa kumwagilia mbegu kwa miaka sita bila kuona kitu chochote kikitokea ardhini. Tungekata tamaa na kuacha kumwagilia, na kwenda kulima kitu kingine au kutafuta kitu kingine kabisa cha kufanya.
Na hata kama ungekuwa na moyo wa kuendelea, ungepata lawama, kukatishwa tamaa na kuchekwa na ndugu, jamaa, marafiki na hata watu baki tu.
Watu waliofanikiwa kwenye maisha walijifunza kuwa hauwezi kuiruka hii hatua ya mianzi. Pengine walifundishwa na mtu, walijifunza baada ya kujaribu na kushindwa sana au iliwekwa tu ndani yao. Walitambua kuwa ili ufanikiwe inabidi ufanye kwa bidii, kwa muda mrefu bila matunda kuonekana. Inabidi uwe wa ziada ili kupata ziada.
Watu wanaofanikiwa ni wale ambao wamekubali kupanda mbegu kwa miaka sita wakiwa hawaoni matunda, wanachekwa, wanakatishwa tamaa na kubezwa na ndugu, jamaa na marafiki wanaowapenda. Ile ndoto yao ya kupanda mianzi mirefu zaidi duniani inawapa hamasa ya kutokukata tamaa.
Watu wanofanikiwa wamejifunza kuwa ni rahisi kutamani na kutaka mafanikio kama vile mianzi inavyokuwa kutoka kuchipua mpaka kuwa mirefu zaidi duniani ndani ya wiki sita. Lakini wamekubali na kuelewa kuwa zile wiki sita zinakuja kwasababu kuna kazi iliyokuwa inafanyika kwa miaka sita bila kuonekana.
Kitu chochote unachotaka kufanikisha kwenye maisha kinafuta mlolongo huo huo. Kuna muda utahitajika kufanya kazi kwa bidii na kwa muda mrefu bila kuona mafanikio. Kipindi hiki utadharauliwa, utachekwa, utakatishwa tamaa na kutaka kuacha. Hiki ndio kipindi chako cha miaka sita ya kupanda mianzi.
Kama ndoto yako ni kucheza mpira, kuna kipindi utakuwa unafanya mazoezi mara tatu kwa siku, upo fiti na bado haupati namba hata timu ya mtaani. Utaenda kwenye timu na bado utakuwa unaanzia nje. Unaweza kuanza kucheza na bado haulipwi mshahara. Itachukua muda kuwa miongoni mwa wachezaji bora na kulipwa kama mchezaji bora.
Kama ndoto yako ni kufanikiwa kazini hatua ni hiyo hiyo. Utachukua muda sana kupata kazi. Ukipata kazi pia itachukua muda wewe kupewa kazi za maana na mshahara wa maana. Itachukua muda na bidii kubwa sana kabla haujaanza kuaminiwa. Miaka mingi itapita kabla ya kuwa mfanyakazi bora, mwenye mshahara na mafao mengi kazini.
Kama ndoto yako ni biashara, utaratibu ni huo huo. Utaanza na biashara ambayo mteja ni wewe na muuzaji ni wewe. Utapitia kipindi kigumu cha kutokuwa na wateja na watu kutoamini biashara yako. Itachukua muda kupata wateja wa uhakika na wakujirudia. Itachukua muda kufikia hatua mabenki yanakutafuta wewe wakupe mikopo nafuu. Itachukua muda biashara yako iweze kukufanya uishi maisha ya ndoto yako.
Chagua eneo ambalo ndoto yako ipo, chagua kuanza na kukubali kuwekeza miaka yako sita kama ambavyo mkulima wa mianzi anakubali kufanya. Kipindi hiki utafanya zaidi, utakuwa zaidi, utafanikiwa na kupata zaidi.
Kitu chako kinaweza kuchukua mwaka, miaka au maisha yako yote, lakini kitakuwa.
Kupata zaidi, inabidi uwe wa ziada.
#iThinkSo
Uwe na furaha.
Uwe na afya.
Uwe huru kutoka kwenye matatizo
Uwe na amani
Kama kuna kitu umejifunza mtumie mtu wako mmoja wa karibu na yeye ajifunze.
Rogers Katuma
Financial Artist, Senior Adventurer, Occasional Storyteller, Amateur Golfer, Baby Pianist, and Rookie Chessman.
