Usiamini sifa zako unazoweka kwenye mitandao ya jamii

Cheo kipi kizuri zaidi? Muanzilishi au Mkurugenzi? Nilikuwa nafikiria kitu gani cha kujaza kwenye wasifu wangu wa mtandao wa jamii wa LinkedIn. Kama ambavyo kila mtu hufanya, anaenda kwenye mitandao ya jamii hususani LinkedIn kutangaza sifa zake za kazi au biashara.

Nilikuwa nimetoka kufanya kazi kama mkaguzi kwenye kampuni ya kimataifa, PwC Tanzania. Nilifanya mafunzo ya kikazi kwenye kampuni nyingine ya kimataifa ya KPMG Tanzania. Nimesoma chuo kikuu cha Dar es Salaam. Nilikuwa muanzilisha wa kampuni ya teknolojia na mkurugenzi wake mkuu.

Hizi zilikuwa sifa nyingi sana kwenye mitandao ya jamii, hususani LinkedIn. Na mtu yeyote akiangalia kwa mbali kwenye maisha yangu alikuwa anaona kuwa nimejipata na kila kitu kinaenda vizuri kwenye maisha yangu.

Vilevile nilikuwa nahisi kuwa kila mtu ninayemuona kwenye mitandao ya jamii amejipata pia. Sifa zake anazoweka kwenye mitandao ni za kweli. Kila sehemu nikiangalia nilikuwa naona watu wote maarufu, wana kazi nzuri za kuvutia, wanamaisha ya kuhamasisha. Siku moja nikapata uhalisia wa maisha ambao ulibadilisha mtazamo mwingi sana.

“Hello Rogers, mimi ni mzoefu na mjuzi wa mambo ya masoko na mauzo. Nina uzoefu wa miaka minne, sasa hivi natafuta kazi.” Huu ulikuwa mwanzo wa ujumbe niliopokea kwenye mtandao wa LinkedIn.

Nikaenda moja kwa moja kwenye wasifu wake kuangalia sifa zake. Aliandika; Mtaalamu wa masoko, mauzo na matangazo. Amejiajiri kwa muda wa miaka kumi na muanzilishi wa kampuni ya MarketZone.

Nilimuonea huruma baada ya kusoma wasifu wake, alichoandika kwenye ujumbe kuja kwangu ni tofauti na sifa alizoweka kwenye mtandao wa jamii. Hii ilinikumbusha miaka kadhaa nyuma ambapo nilipokea ujumbe kwenye mtandao wa LinkedIn, kutoka kwa baba yangu alipojiunga.

Nikaenda kuangalia wasifu wake, aliandika “Nina uzoefu wa miaka 29 kwenye maswala ya benki. Nimefanya kazi benki ya NBC kwa miaka 21, nikianzia chini kabisa mpaka kuwa kwenye ngazi ya uongozi. Miaka nane imepita tangu nianze kufanya kazi na benki ya kimataifa ya Barclays. Ndoto yangu ni kuanzisha kampuni yangu na kusaidia jamii yangu.”

Kabla ya hapa nilikuwa sijawahi kujua kuwa ndoto ya baba ilikuwa ni kuanzisha kampuni. Nilijua anafanya kazi ya ndoto yake. Nadhani angekuwa kwenye presha zetu sisi vijana angeweka muanzilishi au mkurugenzi wa kampuni yake ya ndoto aliyotaka kuanzisha.

Baba yangu alifariki bila kufanikisha ndoto yake. Baada ya mazishi nikaja kugundua kuwa alikuwa ameanza utaratibu wa kusajili kampuni yake na alikuwa ametafuta jina, EMAKAT.

Miaka ikapita, na mimi nikajikuta nipo kwenye mtandao wa LinkedIn nikifikiria kuandika sifa gani nzuri. Mwanzilishi au mkurugenzi wa kampuni. Na jina la kampuni yangu ilikuwa ni EMAKAT, kuendeleza ndoto ya baba.

Jioni hii ikanifanya nifikirie kwa undani sana kuhusu presha niliyokuwa najipa ya kuamini kila kitu ninachoweka kwenye mitandao ya jamii. Yule jamaa aliyetuma ujumbe kuomba kazi, wasifu wa baba, na uhalisia wangu vyote vilikuwa vinaendana.

Nikajiuliza kama nimeshawahi kuweka kwenye mitandao kuhusu changamoto niliyokuwa napitia kulipa mishahara ya wafanyakazi kwenye kampuni yangu? Hapana sijawahi.

Nikajiuliza kama nimeshawahi kuweka kwenye mitandao kuhusu changamoto nilizokuwa napitia kwenye kutafuta mtaji wa biashara na mara ngapi nilikuwa nakataliwa. Hapana sijawahi.

Nikajiuliza kama nimeshawahi kuweka kwenye mitandao hofu na uoga niliokuwa nao wa biashara yangu kufeli? Hapana, sijawahi.

Vitu nilivyokuwa naweka kwenye mitandao vilikuwa vile vinavyofanya nionekane vizuri na nafanikiwa. Nikiwa mazingira mazuri na nikiwa nakutana na watu wengine wenye sifa kama zangu au walionizidi.

Hii ikanifanya niwe naamini zaidi kwenye wasifu wangu kwenye mitandao ya jamii. Ilinifanya nitumie nguvu nyingi kujenga sifa zangu kwenye mitandao ya jamii kushinda kwenye maisha halisi.

Kwenye uhalisia biashara ilikuwa na changamoto, wateja ilikuwa ngumu kuwapata. Wateja waliopatikana walikuwa hawalipi kwa muda au hawalipi kabisa. Kutafuta mtaji kuendesha biashara ilikuwa ni changamoto kubwa sana.

Ilifika wakati ikawa ni rahisi nikiamka kukimbilia kwenye mitandao ya jamii kushinda kwenda ofisini kwenye biashara yangu. Hii ni miaka zaidi ya nane nyuma ambapo mitandao ya jamii haikuwa mikubwa kama sasa hivi. Sasa hivi hali ni mbaya zaidi kwa watu wengi zaidi.

Wengi wanaweka sifa za malengo na ndoto zao kwenye mitandao ya jamii lakini havina uhalisia kwenye maisha yao. Wanachuja maisha yao kwa jicho la kila kitu kionekane bora, na taratibu wanaanza kuamini hivyo wakati uhalisia sio.

Ni kawaida kuona watu wakiweka kwenye mitandao ya kijamii kuwa wana mahusiano mazuri, ya kuvutia na wanapendana sana. Lakini uhalisia ni mchungu kwao. Maumivu na drama ndo maisha yao ya kweli.

Ni kawaida watu kuweka kwenye mitandao kuwa wana marafiki wengi sana, maarufu sana na wana uwezo sana. Na wataweka picha na video kuonyesha kuwa wanafurahia maisha sana. Lakini uhalisia hawa watu wakipata shida wanakuwa peke yao.

Ni kawaida watu kuweka vyeo na sifa kubwa sana kuhusu kazi zao na biashara zao kwenye mitandao ya jamii. Lakini uhalisia wanahangaika kutafuta kazi, kubadilisha kazi au kufanya biashara tofauti na wanayo ionyesha

Ukimaliza kuzunguka kwenye mitandao ya kijamii na kuamini wasifu na sifa zako unazoweka mwenyewe uhalisia huwa unarudi. Intaneti ikikata au simu ikiisha chaji unabakiwa na maisha yako halisi. Kama hauna amani na furaha kipindi hiki basi una kazi ya ziada ya kufanya.

Kama hauhitaji kwenda mazingira fulani kupiga picha au kukutana na watu fulani ili kuonyesha kwenye mitandao ya jamii basi uhalisia wako ni mzuri.

Kama ukiamka hauna amani kufanya kitu kwenye maisha yako halisi na ni bora uende kwenye mitandao basi una kazi ya kufanya.

Sifa na wasifu unaoweka kwenye mitandao isikufanye uamini ndo uhalisia wako.

#iThinkSo

Uwe na furaha.

Uwe na afya.

Uwe huru kutoka kwenye matatizo.

Upate amani.

Kama kuna kitu umejifunza mtumie mtu wako mmoja wa karibu na yeye ajifunze

Rogers Katuma

Financial Artist, Senior Adventurer, Occasional Storyteller, Amateur Golfer, Baby Pianist, and Rookie Chessman.


Discover more from iThinkSoo

Subscribe to get the latest posts sent to your email.