Nilipoanza chuo kikuu niliweka lengo la kuwa na gari langu nikifika mwaka wa tatu. Ilikuwa ni ndoto yangu kununua Toyota Celica nyekundu au Altezza ya bluu. Nilifanikiwa kununua Toyota Celica nyekundu mwezi mmoja kabla ya mahafali ya chuo, ilikuwa ni kitu kikubwa sana maishani mwangu.
Mara ya kwanza kumiliki kitu au kupitia kitu fulani huwa ina uwezo wa kubadilisha maisha yako. Gari ya kwanza ilikuwa ni miongoni mwa vitu vilivyobadilisha maisha yangu. Hata sasa hivi kuandika tu kuhusu ile gari tabasamu limekuja.
Inanikumbusha safari ya kwanza niliyochukua na gari yangu. Nililichukulia gari langu kama nipo kwenye mahusiano ya kwanza na mwanamke niliyempenda sana.
Miezi michache baada ya kupata gari yangu nilifunga safari kumtembelea baba yangu aliyekuwa anaishi Arusha. Nilipanga safari hii ili kufurahia safari ndefu bila kusumbuliwa na foleni za jijini Dar es Salaam. Kuendesha gari ya ndoto yako kwa kilomita mia saba unahisi kuwa peponi.
Nilipofika nyumbani kwa baba nikamkuta kijana mmoja ambaye nilikuwa simfahamu. Alikuwa analiangalia gari tangu nimefika mpaka naingia ndani. Wakati wote tupo ndani tunasalimiana yeye akaamua kubaki nje.
Nikakumbuka mbali sana, kipindi ambacho na mimi nilikuwa nakaa nje barabarani kushangaa magari ya watu na kutengeneneza ndoto yangu. Nikaamua kuisogeza ndoto yake karibu zaidi. Nikatengeneza mazingira ya yeye kuwa karibu zaidi na gari.
Nikaliweka gari kwenye kona huku likiangalia mbele ili wakati wa kutoka iwe rahisi. Pia ilikuwa ni sehemu ya karibu na bomba la maji kwa ajili ya kuweka mpira wa kuoshea gari. Nikamwambia yule kijana aoeshe gari na kumuachia funguo.
Machozi ya furaha yalikaribia kumtoka wakati anapokea funguo. Nilijua ile ilikuwa fursa nzuri kwake kuliangalia vizuri gari na kutengeneza ndoto yake ya gari atakalolitaka mbeleni. Nikaingia ndani na kuendelea na stori.
Dakika kadhaa zikapita tukasikia mlio mkubwa sana nje, tukashtuka na kuangaliana. Wote tukakimbia na kutoka nje, mimi nikiwa nimeanza kupata hofu ya kitu ninachoenda kukutana nacho ni kuhusu gari.
Kitu cha kwanza kilichoonekana ni moshi mdogo ukitoka nyuma ya gari. Pili nikamuona yule kijana akiwa ndani ya gari ameshikilia usukani. Haikuhitaji bingwa wa hesabu kujua kilichotokea. Kijana alijaribu kuendesha gari, akarudi nyuma na kugonga ukuta.
Kichwani nikajisemea “hapa sasa ndio nimekaribishwa nyumbani na gari limekaribishwa pia.” Nilikuwa na mswali mengi sana kwa yule kijana lakini hekima iliniongoza kuhakikisha kuwa yupo salama. Hakuwa anajibu kitu chochote.
Kwa kuwa hakuumia sehemu yeyote ya nje ya mwili tukawa na amani. Mimi nilitambua kuwa atakuwa ameathirika kisaikolojia kwa kosa alilofanya. Kujaribu kuendesha gari ya mgeni usiyemjua, unayemuona mara ya kwanza na kuigonga gari yake ukutani, sio taswira nzuri kwa mtu yeyote atakayesimuliwa.
Maswali yangu yalikuwa bado kichwani;
Najua hamu ya kutaka kuendesha ilikuzidi, lakini kwanini uliweka gia ya kurudi nyuma wakati gari lipo ukutani tayari?
Kwanini uchague kurudi nyuma wakati mbele kupo wazi na kulikuwa na nafasi ya kutosha mpaka kufika getini?
Kwanini uliamua kuwasha gari na kutaka kuendesha kwanza?
Unaweza kuendesha gari?
Kwakuwa hakuwa na uwezo wa kujibu na kujielezea nikabaki na maswali yangu kichwani. Nikaanza kujiuliza mwenyewe na kutafuta majibu. Nikajiweka kwenye nafasi yake na kumuelewa. Nikamwambia nimemsamehe, ashuke na kuendelea kuosha gari. Na nikamwambia nikitulia nitamfundisha kuendesha gari.
Wakati narudi ndani maswali yote yalipata majibu kichwani kwangu isipokuwa swali moja; Kwanini uchague kurudi nyuma wakati mbele kupo wazi na kulikuwa na nafasi ya kutosha mpaka kufika getini? Kujipa amani ya moyo nikasema alikuwa hajui anachofanya.
Lakini likanijia wazo, kuwa hata mimi mara kwa mara narudi nyuma kwenye maisha yangu na kukumbuka kitu kilichotokea na kukileta sasa, na bado kitaniumiza. Nitakumbuka kitu mama au baba alifanya miaka mingi nyuma na bado kujisikia vibaya.
Nikakukumbuka kuwa sio peke yangu, ni hulka ya binadamu wengi sana kurudi nyuma kwenye maisha yao na kuchukua kitu kitakacho waumiza sasa hivi. Kukumbuka vitu ambavyo vitakupa huzuni, hofu na mawazo mengi mabaya.
Kiuhalisia ni sawa na kwenda kutafuta vitu vya zamani ili vije kututesa huku mbeleni. Tuna maisha mengi sana mbele yetu, kuna nafasi kubwa sana ya kuangalia mbele lakini tunachagua kurudi nyuma kama kijana alivyoendesha gari.
Tunarudi utotoni na kukumbuka mateso tuliyopitia na kujihisi unyonge sasa hivi. Tunakumbuka marafiki au ndugu waliotutesa na kutudharau zamani na kuhisi tunadharaulika hata sasa hivi. Hii ni sawa na kujikwaa kwa kitu ambacho tumekipita na kukivuka.
Hii hutufanya kuharibu maisha yetu ya sasa kwa hofu, huzuni au mawazo kwa kutumia kitu kilichotokea zamani sana. Tukitulia na kufikiria tunagundua tunachofanya hakina maana. Kwa yule kijana tumekubali alikuwa hajui analofanya ndio maana akaweka gia ya kurudi nyuma wakati gari imeshafika ukutani.
Je mimi na wewe?
Tunarudi nyuma kwenye maisha yetu kutafuta kitu ambacho kitatupa simanzi, huzuni, hofu na mawazo sasa hivi au mbeleni.
Siamini kama hatujui tunachofanya kwenye maisha.
Tuache kujikwaa kwenye vitu ambavyo tumevipita na kuruka nyuma
#iThinkSo
Uwe na furaha.
Uwe na afya.
Uwe huru kutoka kwenye matatizo.
Uwe na amani.
Kama kuna kitu umejifunza mtumie mtu mmoja unayemjali na yeye ajifunze
Rogers Katuma
Financial Artist, Senior Adventurer, Occasional Storyteller, Amateur Golfer, Baby Pianist, and Rookie Chessman.
