Utotoni sikuwahi kujiona nikiwa kiongozi kwenye ngazi yeyote ile. Na mara nyingi nilijitahidi kuepuka mazingira ya kuongoza au yaliyonihitaji kuwa mbele za watu. Sehemu pekee nilikuwa tayari kuwa mbele za watu ni wakati wa kucheza mpira wa miguu. Hali hiyo ilibadilika wakati najiunga sekondari ya Pugu Dar es Salaam.
Rafiki yangu mmoja aligombea uongozi nafasi ya uraisi kwenye serikali ya wanafunzi, akashinda. Akanichagua mimi kuwa naibu waziri wa afya kwenye serikali yake. Nafasi ile ilikuwa na faida nyingi sana wakati wa mchana na jioni.
Nilikuwa naruhusiwa kuwahi kutoka darasani kwenda kukagua na kuonja chakula. Nilikuwa napewa ruhusa na msamaha kwa kutokwenda darasani au kuchelewa. Nilikuwa naruhusiwa kuchukua maji ya bure jikoni kwa matumizi yangu binafsi.
Ikifika usiku sasa ndio shughuli ilikuwa ngumu kwenye ile nafasi ya uongozi. Majukumu ya waziri wa afya yalikuwa kuamshwa usiku wa manane kuwapeleka wanafunzi waliokuwa wanaumwa au waliokuwa wanajisikia tu kuumwa.
Mimi ndio nilikuwa mtu wa kwanza kuamshwa. Halafu nitoke kwenda kumuamsha mwalimu wa zamu, halafu kumuamsha dereva na nesi wa shule. Baada ya hapo kumpeleka mgonjwa hospitali ya serikali maeneo ya Gongolamboto.
Pia ilikuwa ni wajibu wangu kuhakikisha mgonjwa ana nguo za kubadilisha ikiwa atalazwa. Kufanya mpango wa kuhakikisha chakula na vinywaji vinapatikana kwa mgonjwa aliyelazwa na vitu vingine vingi sana.
Kuna siku ilikuwa ni kitu cha kawaida kuwa na wagonjwa mpaka watano kwenye mida tofauti. Nilitumia muda mwingi sana kuwajali na kuhangaikia wanafunzi wenzangu. Shule ilikuwa na wanafunzi zaidi ya eflu moja wakati mimi kiongozi, hivyo kupata kesi tano za wagonjwa tuliona ni kawaida.
Kwenye kutimiza majukumu yangu ya kuhudumia wanafunzi zaidi ya elfu moja, usiku wa manane nilikuwa naona kama napambana na dunia nzima. Nilikuwa nahisi nipo peke yangu kwa sababu mimi ndio nikuwa mtu wa kwanza kuamshwa usiku. Na mimi ndio nilikuwa mtu wa mwisho kurudi kulala.
Shule ilikuwa na wanafunzi wengi sana, ilikuwa ngumu pia watu wengi kujuana. Mimi sikuwa najulikana sana shuleni kwa sababu nafasi yangu ya uongozi ilikuwa ni kuonja chakula mchana na kuhangaika na wagonjwa usiku.
Na kuna watu wengi sana ambao walinisahau kabisa siku ya pili baada ya kushinda nao usiku kucha kwa daktari au baada ya kulazwa. Wakipona na kurudi kwenye maisha yao ya kila siku huwa walikuwa hawakumbuki uwepo wangu.
Nakumbuka siku moja kulikuwa na mechi ya madarasa kwenye timu za mpira wa miguu, kapteni wa darasa wakati anapanga namba akasema hanikumbuki kabisa. Wakati mimi nakumbuka wiki kadhaa nyuma nilikesha naye hospitali wakati anasumbuliwa na tumbo la kuhara.
Kibaya sio kwamba alikuwa hanikumbuki kama mchezaji mwenzake tu, bali hata kuwa mimi ni naibu waziri wa afya ambaye nilimuhangaikia kwenda hospitali alipozidiwa. Hiki kitu kiliniumiza sana na kuhisi kweli napambana na dunia ambayo haijali.
Siku moja nakumbuka wakati tupo hospitalini tukimsubiri mgonjwa aliyelazwa, nilianzisha mazungumzo na mwalimu wa zamu niliyekuja naye. Huyu alikuwa ni miongoni mwa walimu wakongwe zaidi pale shuleni.
Ameshafanya safari za kuwaleta wanafunzi hospitali zaidi ya mamia na ameshiriki kusuluhisha matatizo ya wanafunzi kwa maelfu. Nilipomwambia kuhusu machungu yangu ya watu kutojali au kutokunikumbuka baada ya kuhangaika nao usiku alitabasamu tu.
Baada ya sekunde kadhaa za ukimya akasema “Mimi nakutana na wanafunzi wengi sana ambao niliwasaidia kuhamia shuleni hapa, niliwatatulia matatizo yao na wazazi wao au niliwasaidia kufaulu, na huwa hata kunisalimia hawataki. Wengi wao hunikwepa kabisa”
Tabasamu lake likapotea, akaangalia chini na kisha kusema kitu ambacho kilikuwa na funzo kubwa sana, “kuna wanafunzi wangu ambao sasa hivi ni viongozi wakubwa sana, wafanyabiashara maarufu na wengine wapo kwenye nafasi kubwa sana, lakini hakuna aliyewahi kuja kushukuru wala hata kuzungumza sehemu mchango wangu kwao. Lakini nawaelewa, ni hulka ya binadamu kujifikiria wenyewe sana kiasi kushindwa kutambua uwepo au mchango wa wengine.”
Ile ikanipa moyo pia kuwa ninachofanya kina faida kwa watu hata kama nahisi nipo peke yangu na watu hawaoni au kushukuru. Wakati mimi nawahi kutoka darasani na kukosa vipindi kwenda kuonja na kukagua chakula wao watakuja wakati wa kula wakiwa na njaa sana, ni ngumu kutambua mchango wangu.
Wakati mimi nahangaika na walimu wa zamu, manesi na dereva kuwapeleka hospitali wao wanahangaika na maumivu mengi sana usiku kukumbuka kuhusu uwepo wangu au kuwa tupo timu moja tunacheza mpira darasani.
Kupitia ile ikanifundisha kujizuia kuweka matarajio kutoka kwa watu nikiwa nafanya kitu. Ilinifundisha kutosubiria watu washukuru, wakupe ushauri, wakupe maoni kama unataka kufanya kitu. Pia iliniondolea hofu ya kuogopa watu watasemaje au wananionaje kwa kitu ninachofanya.
Watu wanakuwa na mambo yao mengi sana wanapitia kutulia na kuangalia nini mimi nafanya au nawafanyia. Hii ikanipa hamasa pia ya kutokuogopa kuanza jambo au kuendeleza jambo kwa kuwaza watu watanionaje au watanifikiriaje. Najua hawana muda wa kuwaza wala kufikiria kwasababu wana yao wanahangaika nayo.
Kufanya jambo lako ukiwa unahisi dunia nzima inakuangalia na kukutazama sio uhalisia. Muda mwingi dunia haitambui hata uwepo wako. Ukijaribu jambo na likafeli hakuna anayejali wala kujishughulisha na wewe. Dunia itajali uwepo wako pale utakapofanikiwa au kuwa mtu fulani mwenye nafasi na maana kwao.
Kama kuna kitu unafanya, fanya kwa uzuri na ubora haijalishi watu wanaona au hawaoni. Fanya kwa nguvu zote, kwa muda mrefu kwa sababu hakuna anayejali ukiwa unajitafuta. Watu watajali ukifanikiwa.
Hakuna mtu mwenye muda na wewe ukiwa haujafanikiwa. Dunia haitambui uwepo wako. Hakuna vita ya dunia na wewe. Kwenye maisha yako vita ni ya wewe wa sasa apambane kumjenga wewe anayekuja.
#iThinkSo
Uwe na furaha.
Uwe na afya.
Uwer huru kutoka kwenye mateso.
Uwe na amani.
Kama kuna kitu umejifunza mtumie mtu mmoja unayemjali na yeye ajifunze kitu.
Rogers Katuma
Financial Artist, Senior Adventurer, Occasional Storyteller, Amateur Golfer, Baby Pianist, and Rookie Chessman.
