Nilipoanzisha kampuni yangu ya Emakatt, mazingira ya biashara changa za teknolojia yalikuwa yanaanza kuchangamka sana. Na nchini kwetu ilikuwa bado ni nadra sana kwa watu wengi kujihusisha hivyo ilikuwa rahisi sana kujuana. Ilikuwa kawaida kujiona kama sisi ni mashujaa na watu wenye uwezo mkubwa sana kwenye mazingira hayo.
Ilikuwa haijalishi ndoto na malengo ambayo mtu alikuwa nayo. Kitu cha maana ilikuwa ni kuwa mjanja na kuonekana umejipata. Na hiyo ilikuwa ndio dalili kuu ya kuwa mtu alikuwa anaelekea kwenye malengo yake.
Lengo la kampuni ilikuwa ni kuruhusu watu wengi zaidi kuanza kutumia mashine za kufua kwenye maisha yao. Nilitengeneza programu kwenye simu iliyowaruhusu watu kuweka oda ya kufuata nguo zao chafu kwa pikipiki na kuzipeleka sehemu zifuliwe na mashine. Baada ya hapo nguo hizo ilikuwa zinarudishwa kwa mteja.
Wazo letu lilikuwa kubwa na zuri sana, lakini ili kuwa sawa na wengine ilitakiwa pia kuwa na tisheti nzuri na za kuvutia za wafanyakazi zinazoendana na muonekano wa kampuni mpya ya teknolojia kama ambavyo marekani walikuwa wanafanya.
Tulitengeneza tisheti nzuri sana na kadi za biashara za kuvutia. Zilikuwa nzuri kiasi ambacho marafiki na wateja wengi wakawa wanaomba tisheti. Na tukawa tunazigawa kwa furaha sana. Hii ilitufanya tujione kuwa tunafanikiwa sana.
Miezi ikapita na utaratibu huu tukaendelea nao, lakini tukaanza kuona changamoto. Mauzo ya watu kuleta nguo ili zifuliwe yakapungua sana. Kuna muda tulikuwa tunagawa tisheti nyingi kushinda idadi ya nguo zilizokuwa zinakuja kwa ajili ya kufuliwa.
Na hizi tisheti tulikuwa tunatumia gharama nyingi sana kutengeneza na tuliishia kuzigawa bure kwa marafiki, wateja na waanzilishi wengine wa kampuni tuliokuwa tunafahamiana nao. Tulikuwa tunajitetea kuwa tunafanya vile kama njia ya matangazo na mauzo.
Hali ilivyozidi kuwa mbaya ikabidi tuwe na kikao cha dharura kutafakari nini cha kufanya. Kwanza ikabidi tujikumbushe vitu vita vya muhimu kwenye biashara yetu:
Cha kwanza, ilikuwa ni idadi ya watu waliopakua programu yetu kwenye simu.
Pili, idadi ya watu waliotumia programu hiyo kuweka oda ya nguo zao kufuatwa na kufuliwa.
Tatu, ni idadi ya watu waliotumia tena programu kuweka oda siku zilizofuata.
Katika malengo kumi ya kwanza ambayo tuliainisha hamna hata moja ambalo lilikuwa kuwa na tisheti nzuri na bora sana kwa ajili ya kugawa kwa marafiki, wateja na watu wengine. Ingawa kiuhalisia hicho ndio kitu tulichofanya kwa ubora na vizuri kushinda vyote vilivyokuwa kwenye kumi bora.
Mwisho wa kikao tukakubaliana kuwa kufanya kitu ambacho sio cha muhimu kwa umaridadi na ubora hakukubadilisha kikawa cha ubora na kuifanya biashara yetu ipige hatua. Ilitulazimu turudi kwenye misingi ya kutambua nini kilikuwa cha umuhimu na kukipa kipaumbele.
Tukaacha kutengeneza tisheti kwa ajili ya watu wengine na kutumia zile fedha kwenye matangazo yenye ufanisi wa kuweza kuwafikia wateja. Na hapo ndio tukaanza kuona utofauti kwenye mauzo.
Kile kipindi kilinipa funzo kubwa sana ambalo linatumika kwenye kila nyanja ya maisha, kuchukua kitu ambacho hakina umuhimu na kukifanya kwa umaridadi, umakini na ubora sana hakutakifanya kitu hicho kuwa muhimu mwisho wa siku.
Nilikuwa na marafiki, ndugu na mahusiano na watu wengi sana ambao wakuwa na umuhimu kwenye maisha yangu, lakini nilikuwa naweka jitihada, nguvu na kuwekeza muda na rasilimali kuhakikisha tunaendelea kuwa karibu.
Lakini haikuwahi kubadilisha na kuwafanya watu hao kuwa wa umuhimu. Nikaacha, nikaanza kuweka jitihada kwa watu wa umuhimu tu.
Nilikuwa nakubali kufanya miradi au mawazo ya aina tofuati tofauti ambayo hayakuwa na umuhimu kwenye maisha yangu. Ila nilikuwa najitoa na kuifanya kama vile maisha yangu yalikuwa yanategemea ile miradi na yale mawazo.
Mwisho wa siku haikufanya ile miradi na yale mawazo kuwa ya umuhimu. Nikaacha na kuweka nguvu kwenye miradi na mawazo yenye umuhimu tu.
Kwenye mitandano ya jamii nilikuwa nafuatilia kila mtu na kila kitu nikiwa na imani kuwa kuna umuhimu nitapata. Nikajifunza kuwa sio kweli, kuna waongo, waigizaji, presha na vingi sana kutoka kwenye mitandao ambavyo havikuwa vya umuhimu kwangu. Nikachagua watu wa muhimu na vitu vya muhimu vya kufuatilia.
Kila nyanja ya maisha ina vitu vya umuhimu na ambavyo sio muhimu. Kila binadamu ana hivyo vitu vyote. Kuna vitu ni vya muhimu kwa rafiki zako na ndugu zako lakini sio muhimu kwako. Ukivifanya vitu hivyo kwa ufasaha na umaridadi mkubwa sana havitakuja kuwa vya muhimu bado mwisho wa siku.
Ni jukumu lako kuchukua muda na kutafakari vitu gani ambavyo unavifanya kwa ufasaha na umaridadi mkubwa sana lakini sio vya muhimu kwenye maisha yako. Inaweza kuwa kung’ang’ania urafiki au mahusiano yasiyoenda popote au kufanya kazi au biashara ambayo haina faida au kufuatilia vitu kwenye mitandao ya jamii ambavyo havina mantiki kwenye maisha yako.
Viache hivyo vitu na tumia muda kutafakari ni vitu gani vya umuhimu kwako na maisha yako. Kisha wekeza nguvu, akili, muda na rasiliimali nyingine nyingi unazoweza kuzipata kwenye hilo jambo.
Kila ukirudia kufanya vitu ambavyo sio vya muhimu kumbuka kuwa hata uvifanye kwa umakini vitu hivyo vhavitaweza kuwa vya muhimu kamwe. Huu ni muda wa kuacha vitu visivyo vya muhimu kuanza kufanya vitu vya muhimu.
Usipofanya hivyo maisha yatatafuta njia ya kuvifanya vitu vya muhimu vipotee au viharibike mpaka utakapokubali kubadilika.
#iThinkSo
Kama kuna kitu umejifunza mtumie mtu wako mmoja wa karibu naye ajifunze.
Uwe na furaha.
Uwe na afya.
Uwe huru kutoka kwenye matatizo.
Uwe na amani.
Rogers Katuma
Financial Artist, Senior Adventurer, Occasional Storyteller, Amateur Golfer, Baby Pianist, and Rookie Chessman.
