Mara ya kwanza kupewa nafasi ya kuendesha gari ilikuwa na mjomba wangu, ambaye alikuwa ni dereva wa magari makubwa ya mizigo. Jioni moja alijitolea kunifundisha. Hiyo siku alirudi na daladala ndogo ambayo aliazima kwa rafiki yake kazini.
Ilikuwa ni gari ya zamani na ilikuwa ni ya kubadilisha gia kwa mkono. Alinifundisha kwa masaa mawili na tukamaliza. Ilikuwa ni wakati bora sana kwenye maisha yangu ambao ulitengeneza ndoto yangu ya kuja kuwa na gari yangu na kuendesha kila mara na kila sehemu.
Sikupata nafasi nyingine yeyote ya kufundishwa tena na nikasahau kila kitu nilichofundishwa. Kitu pekee kilichobaki kilikuwa ni harufu ya petroli, sauti za gia zikiwa zinabadilika na sauti za matairi wakati napita kwenye mashimo.
Miaka mitano ilipita mpaka nilipopata nafasi nyingine ya kuendesha gari. Mara ya kwanza ilikuwa ni rafiki yangu ambaye tulikuwa naye chuo mwaka mmoja. Yeye alifanikiwa kununua gari yake kwa kuagiza kutoka Japan.
Akawa ndio kioo changu cha kumuigiza, ndoto yangu ikawa karibu zaidi maana alinieleza mbinu zote alizotumia kufanikisha ndoto yake akiwa chuo. Siku moja alinichukua na kunipeleka kwenye barabara zenye ukimya na kuniachia niendeshe.
Gari yake ilikuwa sio ya kuingiza gia kwa mkono, ilikuwa inaingia moja kwa moja maana ilikuwa ni automatic. Hakunipa muda mrefu sana wa kuendesha, lakini alitumia muda mwingi sana kunielezea namna ya kuagiza gari Japan na gharama zake.
Hii iliniongezea hamasa ya kutaka kuwa na gari yangu mwenyewe kabla ya kumaliza chuo. Nilianza kuwaambia watu wengi zaidi na kutafuta njia mbali mbali za kunisaidia kujifunza gari kabla yangu haijafika.
Miezi kadhaa ikapita, ikaja siku yangu ya kuzaliwa, rafiki yangu Jacqueline, alikuwa na gari, akatengeneza mpango vila mimi kujua. Akaniambia twende tukale chakula cha mchana nje ya chuo kusheherekea siku yangu ya kuzaliwa. Tukatoka chuo taratibu na kupiga stori, mara nikajikuta anaingiza gari kwenye viwanja vya wazi vya Tanganyika Packers, maeneo ya Kawe.
Akazima gari, akachomoa funguo na kutoka nje ya gari na kuzunguka upande wangu, kisha akasema, “haya kijana mwenye siku yake ya kuzaliwa, shika funguo,” huku akinikabidhi funguo za gari.
“Ingiza funguo, zungusha kuelekea kulia, kanyaga breki, weka gia kwenye alama ya “D” na taratibu achia breki gari itaanza kwenda mbele” alianza kunipa maelekezo ambayo mtu anayejifunza gari mara ya kwanza anayahitaji.
Siku hii ndio nilifurahia zaidi kujifunza kuendesha gari, na niliendesha kwa muda mrefu zaidi kiasi ambacho kilinipa imani kubwa zaidi ya kuja kuweza kuendesha gari. Pia nadhani kufundishwa na sauti ya kike kulichangia, hauwezi jua.
Kwenye kuendesha gari shida haipo kwenye kuwasha gari au kujua breki ipo wapi na kukanyaga mafuta. Bali kujiamini kufanya yote hayo wakati unakadiria nafasi yako barabarani, kupishana na magari mengine, pikipiki na watembea kwa miguu. Na hivyo vyote kuvifanya wakati unafuata sheria.
Pamoja na yale mafunzo mazuri, gari yangu ilipofika nilikuwa nimesahau kila kitu nilchofundishwa. Dereva aliyeniletea gari alilisimamisha kwenye sehemu ya kuegeshea karibu na kitu cha mafuta pale Sinza, akaondoka.
Mwanzoni nilijihisi kuwa nitaweza kuendesha mwenyewe kwasababu nilipata mafunzo mwaka uliopita, lakini nilipoingia kwenye gari kila kitu kilikuwa kipya kwangu. Nilitumia zaidi ya masaa matatu nikihangaika kushusha breki ya mkono, sikukumbuka kufundishwa kuhusu hicho.
Mlinzi wa kile kituo cha mafuta aliona nimekaa muda mrefu akaja kuniuliza kama kila kitu kipo sawa. Nikamwambia najaribu kukanyaga breki, na kuweka gia kwenye D lakini gari haiendi. Akaniambia ni kwasababu breki ya mkono ilikuwa juu, alinisaidia kuishusha na kuniacha.
Bado nikawa sijui namna ya kuwasha taa, kutoa waipa, na vitu vingine vingi. Simu yangu ilikuwa imeisha chaji, ningetumia kuingia kwenye mitandao na kutafuta. Nikaamua kutoka vile vile bila taa na waipa zikiwa zimewashwa mpaka chuo cha ardhi.
Njiani nilipigiwa honi nyingi sana kwa kutembea vile lakini sikujali. Uzuri ilikuwa imeshafika saa sita usiku barabara haikuwa na magari mengi wala foleni, vinginevyo nisingefanikiwa. Nilikuwa na nafasi kubwa ya kukutwa hospitali au polisi na sio chuoni.
Nikaamua kuwa nitaanza kufanya mazoezi ya kuendesha gari kila jioni nikitoka kazini. Ili iniongezee kujiamini na kupata uzoefu. Nilikuwa naenda kulichukua gari chuo kikuu cha Ardhi na kuendesha kwenye barabara za chuo kikuu cha Dar es salaam. Nikimaliza nilikuwa narudisha gari chuo cha Ardhi ambapo ni karibu na nilipokuwa nakaa.
Nilifanya hivi kwa wiki tatu kabla ya mafuta kukaribia kuisha. Hii ikanilazimu kupeleka gari kwenye kituo cha mafuta. Hapo ndio kipimo kikuu cha uzoefu kilikuja, kwasababu barabara ya mlimani city ambapo kulikuwa na kituo cha mafuta kulikuwa na gari nyingi sana.
Nilifanikiwa kuifikisha gari kwenye kituo cha mafuta na kuirudisha tena chuo kikuu cha ardhi bila ajali na majanga. Hapo ndio imani yangu kuwa nimeweza kuendesha gari ilikuja. Nikaendelea kupata uzoefu zaidi na kusafiri na gari mpaka mikoani.
Miezi ikapita na nikawa mkongwe barabarani. Sina shida kuendesha huku nikicheza muziki au kupiga stori na watu. Sikuwa na hofu ya kupishana na magari makubwa wala kusumbuana na pikipiki.
Miaka ikapita na ile raha ya kuendesha ikaanza kupotea. Kadri nilivyokuwa nazidi kupata uzoefu na uwezo kwenye kuendesha gari ndivyo nilivyokuwa nachoka sana kuendesha gari. Sikuwa na hamasa ya kuendesha kama kipindi ambacho mjomba alikuwa ananifundisha, au rafiki yangu na gari yake ya Japan au siku yangu ya kuzaliwa na gari ya Jacqueline.
Kuendesha gari ilikuwa ni kama kukamilisha ratiba ya kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine. Nikabadilisha magari, barabara na mazingira lakini furaha ya kuendesha gari ilibakia kunichosha.
Nikaanza kujifunza kuendesha gari na trela, kuendesha pikipiki na hata kurudi kwenye gari za kuingiza gia kwa mkono. Lakini utaratibu ukawa ule ule, kadri nilivyokuwa bora zaidi kwenye kuendesha kupata uzoefu, ndivyo nilivyozidi kuchoka kuendesha.
Nilipofikiria kwa undani nikagundua mafanikio ndio yapo hivyo, ukianza kufanikiwa na kuviweza vitu huwa vinaanza kuchosha. Vitu vipya huwa na hamasa na furaha ya kuanza na kujifunza. Vitu vyenye uzoefu na imara huwa vinachosha.
Biashara changa huwa na mbwembwe na hamasa nyingi sana kwa sababu zinaanza, ndoto nyingi na vitu vingi vya kubadilisha na kufanya. Biashara kubwa huwa hazina hivyo vitu. Zinakuwa na utaratibu na sheria ya namna ya kufanya vitu. Zinakuwa na njia na mbinu za kupata wateja wanojirudia.
Mahusiano au ndoa zinazoanza huwa na mambo mengi sana. Wapenzi wapya huwa wana hamu ya kujuana zaidi, kuwa na hamasa ya kutoka na kufanya vitu vingi kwa pamoja. Penzi la muda mrefu na lenye mafanikio huwa linachosha. Wapenzi wanajuana tayari, wanajua mabaya na mazuri ya mwingine. Wanafanya vitu vilevile vinavyojirudia kwasababu wamegundua vinawafaa wao.
Watu wa mazoezi waliofanikiwa na kuwa fiti wanafanya mazoezi ya aina yale yale ambayo huwa yanachosha. Pia huwa wanakula vyakula vya aina ileile. Watu amabo sio wa mazoezi ndio wanakuwa na hamasa ya kufanya mazoezi mengi na ya aina tofauti. Pia ndio watu ambao hutafuta aina zote za vyakula.
Jiulize hapo kwenye maisha yako, kitu unachofanya kinakupa hamasa ya kukifanya kila siku? Je umeweza kutengeneza misingi na ratiba ya kujirudia rudia kwa sababu umegundua inafanya kazi? Au ndio upo kwenye mlolongo wa kubadili kila siku?
Ukiona kila siku unaanza kitu kipya, ratiba mpya, una mpenzi mpya au mahusiano mapya ina maanisha bado haupo kwenye hatua ya mafanikio. Mafanikio ya kweli ni kama kuendesha gari ambayo umeizoea kwa miaka mingi. Utaratibu unakuwa ule ule, kadri unavyokuwa dereva mzuri ndivyo inavyochosha zaidi
Ukitaka kufanikiwa inabidi ufanye kitu kwa muda mrefu ili uwe na uwezo na uzoefu wa kutosha kuanza kukufanya uchoke.
Fanya mazoezi yale yale kwa miaka mingi na utapata mwili unaoutaka.
Fanya biashara ya lengo lako kwa muda mrefu na itajenga misingi ya mafanikio.
Jenga mahusiano na mpenzi wako kwa mufa mrefu kiasi ambacho utakuwa unajua mazuri yake, mabaya yake na sio kutaka kutoka ili mjuane.
Fanya ajira yako kwa unyenyekevu na umakini kiasi inakuwa inachosha kurudia, hapo ndio utakuwa bora.
Mafanikio yakija utajua tu, utakuwa unafanya vitu vinavyochosha.
#iThinkSo
Uwe na furaha.
Uwe na afya.
Uwe huru kutoka kwenye mateso.
Upate amani.
Kama kuna kitu umejifunza mtumie mtu mmoja unayemjali naye ajifunze.
Rogers Katuma
Financial Artist, Senior Adventurer, Occasional Storyteller, Amateur Golfer, Baby Pianist, and Rookie Chessman.
