Leo ni siku ya mwisho ya mwaka 2025. Sitengenezi malengo mapya ya mwaka unaofuata. Ninarudia kukagua na kupitia nini nilifanya mwaka huu. Na miongoni mwa vitu nilivyopitia ni vitu niliyopoteza, kuharibu au kuvunja. Vipo vingi sana.
Nikiwa katikati ya kupitia nikakumbuka miaka mingi sana imepita na nimefanya kitu hiki sana. Kumbukumbu zikaanza kuja kuhusu vitu vyangu ambavyo vilikuwa bora na muhimu sana kwenye maisha yangu wakati navipata, na sasa havipo na mimi kwasababu moja ama nyingine.
Baiskeli yangu ya kwanza kumiliki ipo juu kabisa kwenye orodha ya vitu muhimu kuwa navyo maishani. Ilikuwa nyekundu, saizi ya kati na ilikuwa ya kuingiza gia, ambazo zilikuwa sita. Baiskeli hii ilikuwa ni zawadi kutoka kwa mama yangu baada ya kuwa na ufaulu mzuri sana wa darasa la saba.
Nilikuwa naendesha baiskeli hii kila siku kwenda kila sehemu. Sasa hivi sikumbuki nini kilitokea kwenye hii baiskeli mpaka ikaondoka maishani mwangu. Miaka mingi imepita na hapo katikati nimeshamiliki baiskeli nyingine tofauti kama saba. Baiskeli ni kitu rahisi kukibadilisha.
Kitu cha pili kwenye orodha yangu ilikuwa ni kifaa kidogo cha Sony kwa ajili ya kusikilizia muziki. Na kulikuwa na nyimbo moja ya msanii anaitwa T-Pain, inaitwa 5 O’clock in the morning. Nilikuwa naisikiliza nyimbo hii moja kwa kurudia rudia kwa masaa kila siku. Nakumbuka siku moja wakati nimeenda kumtembelea bibi yangu Songea nilimuazima kifaa hiki ndugu yangu mmoja, akapotea nacho.
Nilikubali kuachwa na basi la kunirudisha Dar es Salaam ila nimpate yeye. Nilimtafuta kila sehemu, nikaja kumpata baada ya siku ya nne. Sikuwa tayari kumuachia yeye wala mtu yeyote duniani. Miaka ikapita na sijui kilienda wapi kifaa kile. Nikabadili vifaa vingi vya kusikilizia muziki, mpaka sasa miziki yote inakuwa kwenye simu. Ni rahisi kubadilisha vifaa vya kusikilizia muziki.
Gari yangu ya kwanza ilikuwa ni miongoni mwa ndoto yangu ya muda mrefu sana. Ni kawaida ukiwa mtoto kutaka kuwa na gari ukiwa mkubwa. Nilivyofika chuo ndoto yangu ikageuka na kuwa lengo. “Nataka kuwa na gari yangu aina ya Toyota celica, nyekundu kabla ya mahafali yangu ya chuo kikuu mwaka wa tatu.”
Ndoto yangu ikatimia, na ilikuwa nzuri kama nilivyokuwa napatia picha. Nilisafiri na lile gari sehemu nyingi sana Tanzania. Ilinipeleka kwenye mbuga za wanyama Ruaha, Iringa, kwenye mapango ya Amboni Tanga na kwenye barabara tambarare za kuelekea Dodoma. Miaka ikapita nikaliuza lile gari. Nikabadilisha gari mbalimbali na hata kubadilisha ndoto na malengo kuhusu gari. Ni rahisi kubadilisha gari.
Wakati nipo mtoto nilikuwa nasikia sana msemo kuwa “ardhi ni mali.” Nikasema siku moja na mimi nitakuja kumiliki ardhi. Nilipofika chuo nikafanikiwa kupata fedha ya kununua kiwanja changu cha kwanza. Bibi yangu aliyekuwa mwenyeji wa Kigamboni, Dar es Salaam aliniuzia kiwanja. Miaka ikapita na kiwanja kikaongezeka thamani.
Sikufanya chochote kwenye kile kiwanja kwasababu sikuwa na mpango wa haraka. Kama ambavyo vitu hutokea, na kiwanja changu kikakutwa na tukio. Bibi yangu alipofariki nikaja kuambiwa kuwa kuna ndugu wa karibu alikiuza kile kiwanja changu kwa mtu mwingine kabka bibi hajafariki. Ni rahisi kubadilisha kiwanja.
Kila mtu ana historia ya mpenzi wake wa kwanza. Mimi wa kwangu alikuwa mzuri sana, na alinikubali kipindi ambacho sikuwa na kujiamini sana kuhusu vitu vingi kwenye maisha. Na hii ilikuwa sekondari. Ilikuwa mara ya kwanza kuelewa watu walivyokuwa wanasema “mapenzi matamu, ukipendwa unaweza ishi bila chakula.”
Penzi letu lilikuwa la mbali, mimi nilikuwa shule ya bweni yeye yupo nyumbani, zaidi ya kilomita elfu moja mbali. Uvumilivu ukamshinda akatoka na mtu mwingine. Furaha aliyonipa ndani miezi sita ya ucbumba na maumivu aliyonipa siku tulipotengana bado yapo.
Natamani kusema miaka ilipita na nikaweza kumbadilisha kwa kuwa na mpenzi mwingine lakini mahusiano hayapo hivyo.Baiskeli, kifaa cha kusikilizia muziki, gari, ardhi na vitu vyote unavyoweza kuvimiliki una uwezo wa kuvitafuta tena au kuvibadilisha.
Mahuasiano ni miongoni mwa vitu vitatu ambavyo hatuvimiliki na hatuwezi kuvibadilisha, vingine ni afya na muda.
Kila binadamu anakupa kitu tofauti kwenye maisha yako. Furaha au huzuni anayokupa ni tofauti na ambayo atakupa mtu mwingine. Kila unayekutana naye duniani ni mtu wa pekee, nafasi yake anaweza kuchukua mtu mwingine lakini alivyokufanya ujisikie hakuna mwingine anaweza kurudia. Miaka ikapita na kila mwanamke aliyekuja kwenye maisha yangu alikuwa na utofauti wake.
Hiyo sio tu kwa mpenzi, ipo kwa wazazi, ndugu, jamaa, marafiki na hata watu baki. Vitu vizuri na vibaya wanavyokuja navyo ni wao tu wana uwezo wa kuja nao. Na kila mtu atakuja kivyake.
Nina marafiki ambao walinisaliti, lakini siwezi kuomba marafiki wengine kwasababu vitu nilivyojifunza kwenye usaliti ule vilikuwa ni muhimu na ilibidi wao tu wafanye vile ili nijifunze. Kuna maadui au washindani ninao ambao wananifanya niwe bora kwa namna fulani kwasababu tu ya namna wao walivyo.
Nina wadogo zangu ambao kuna siku nataka wapotee dunia kwa namna wanavyokera na kuna siku nakuwa tayari kupotea duniani kwa ajili yao. Kila mmoja wao ni wa utofauti na hakuna njia ya kuwabadilisha.
Hakuna anayemiliki muda. Uwe unataka au hautaki, muda utaendelea kwenda. Utakachochagua kufanya sasa hivi una uwezo wa kufanya mambo fulani yatokee na mengine yasitokee, lakini muda wenyewe utaenda tu. Na muda ukishaenda, hata ufanye nini hauwezi kuurudisha.
Muda unaenda kwa spidi yake yenyewe. Haijalishi una furaha kiasi gani kwa yanayokuja kiasi unatamani muda uje haraka au una huzuni kiasi gani unatamani muda uende haraka. Hauwezi kusogeza mbele muda wa sasa na hauwezi kuuleta muda wa mbele uje nyuma. Hauwezi kuurudisha muda uliopotea urudi sasa. Haumiliki muda lakini una uwezo wa kuchagua nini cha kufanya kwenye muda uliopewa.
Huwa nakumbuka furaha na maisha mazuri niliyoishi nikiwa chuo. Ulikuwa muda huru sana na sikuwa na mawazo mengi kuhusu maisha, michezo ilikuwa mingi, nilikuwa napewa fedha za matumizi na kulikuwa na marafiki wengi sana, hasa wale wakike. Siwezi kurudisha muda ule, hata nikienda chuo tena kusoma sitakutana na watu walewale, mazingira yale yale na urafiki wa aina ileile.
Na kitu cha mwisho ni afya, hii ni asili na ni bailojia. Nina uwezo wa kuchagua kitu cha kula, cha kunywa, mazoezi ya kufanya na kuupumzisha mwili lakini siwezi kuupangia mwili namna ya kuzeeka, kipi cha kuumwa au siku na namna ya kufa.
Nilipewa mwili wangu na wazazi nilipozaliwa, na nitauacha siku nikifa. Hapo katikati ya kuzaliwa na kufa ninachoweza kufanya ni kuutunza mwili wangu kwa kadri ninavyoweza kuepusha magonjwa au madhara yanayoweza kuzuilika.
Baada ya kupitia mwaka 2025 na kuona vitu vyote nilivyopoteza au kuharibu ambavyo nilikuwa namiliki ikanibidi nitafakari kwa undani sana kuhusu vitu ambavyo sivimiliki na sina uwezo wa kuvibadilisha au kuvitafuta tena.
Baiskeli, kifaa cha kusikilizia muziki, gari, ardhi ni vitu ambavyo naweza kuvitafuta tena mwaka wowote nikiamua. Mahusiano na watu ninaowajali na kuwapenda yakishaharibika au mtu akifariki hakuna namna ya kuyabadilisha. Muda ukishapita ndo umepita. Afya ikiwa mbovu hamna kitu kingine chochote kinachoweza kwenda kwenye maisha.
Ikanifanya nifikirie ni namna gani mwaka unaofuata nichague kuweka nguvu kwenye hivi vitu. Najua na wewe una furaha ya mwaka mpya, na ni kawaida ya watu wengi kuweka malengo mapya ya mwaka mpya.
Naomba kwa huu mwaka mpya ufikirie yafuatayo:
Kwanza, acha kutumia muda na nguvu nyingi sana kutafuta vitu ambavyo unaweza kuvibadilisha au kuvitafuta tena ukiamua, hizo baiskeli, magari na mashamba ukiamua kutafuta utapata tu. Hususani kama kufanya hivyo unapoteza afya, muda na mahusiano.
Pili wekeza nguvu zako kwenye mahusiano yenye maana kwako. Kama una familia ambayo inakujali, kukupenda na kukuthamini basi weka juhudi kuwajali na kuwathamini. Usiishi ukijidanganya kuwa huyo mzazi wako, kaka yako au dada yako au rafiki yako atakuwepo milele.
Usimfanye yeye awe ndo wa kwanza kukutafuta kila siku, wa kwanza kukujulia hali, wa kwanza kukutembelea. Kuna siku atachoka na kuacha. Kuna siku hatakuwepo duniani kuendelea kufanya hayo. Unaweza kujidanganya kuwa atakuja mtu mwingine kwenye maisha yako, uhalisia ni kuwa kila mtu mwingine atakuja na vitu vingine.
Tatu, wekeza nguvu kwenye afya yako. Ukiumwa hauwezi kwenda kazini, hauwezi kufanya biashara, hauwezi kuwa bora kwa watu wako wa karibu. Utaishia kuwa mzigo kwao. Angalia vitu unavyokula na kunywa. Jitahidi kupumzisha mwili ukichoka. Fanya mazoezi. Pia jitahidi kujali afya yako ya akili. Msongo wa mawazo na huzuni hudhoofisha mwili pia.
Kitu cha mwisho na muhimu zaidi ya vyote ni kukubaliana na uhalisia kuwa una muda mchache sana hapa duniani. Ulizaliwa, utakufa. Haujui itakuwa lini na kwa njia gani. Tumepoteza wengi mwaka 2025 na tutapoteza wengi zaidi mwaka unaofuata.
Kila sekunde, dakika na siku ya kuwa hai ni zawadi na bahati. Usipoteze muda kwa vitu visivyo na maana. Usihairishe kufuata ndoto zako na malengo yako kwa kujindanganya kuwa bado una muda mwingi sana.
Kumbuka, vitu vyote unavyovimiliki unaweza kuvibadilisha au kuvitafuta tena. Vitu ambavyo hauvimiliki ni mahusiano yako, afya yako na muda wako. Hauwezi kubadilisha wala kuvitafuta tena vikiondoka.
Heri ya mwaka mpya kwako na unao wapenda.
#iThinkSo
Uwe na furaha.
Uwe na afya.
Uwe huru kutoka kwenye mateso.
Uwe na amani.
Kama kuna kitu umejifunza mtumie mtu mmoja unayemjali na yeye ajifunze.
Rogers Katuma
Financial Artist, Senior Adventurer, Occasional Storyteller, Amateur Golfer, Baby Pianist, and Rookie Chessman.
