Chuo kikuu cha dar es salaam kuna taasisi nyingi sana zinaongozwa na wanafunzi. Wakati mimi nipo chuo, miongoni mwa taasisi kubwa mbili zilikuwa ni AIESEC na DUFA, ambayo ilikuwa ni taasisi ya wanafunzi wa maswala ya fedha.
Mwaka wangu wa pili nikiwa chuo nilipata uzoefu kwenye hizi taasisi. Nilipata ujuzi wa namna mambo yalivyokuwa yanaendeshwa. Pia nilipata ujuzi wa namna ya kusimamia watu na matamasha.
Nikiwa katibu mkuu wa taasisi ya wanafunzi maswala ya fedha (DUFA), ilikuwa ni kawaida kuchukua lawama pale mambo yasipoenda vizuri na pia kuchukua sifa mambo yakienda vizuri. Ilikuwa ni nafasi ya uongozi yenye uwazi sana kiutendaji.
Tukio kubwa sana la taasisi ilikuwa ni kuandaa kongamano la shule za biashara za vyuo vikuu Afrika Mashariki. Tukio lilikuwa linahusisha wanafunzi wa vyuo vikuu vya biashara kutoka Kenya, Uganda, Rwanda na wenyeji Tanzania.
Lilikuwa ni tukio la siku mbili, siku ya kwanza ilikuwa kwenye ukumbi wa kihistoria wa Nkrumah pale chuo kikuu cha Dar es Salaam na siku ya pili ilikuwa ni kutembelea mbuga za wanyama au sehemu ya utalii na mapumziko.
Kuandaa kongamano hili ilikuwa inachukua miezi kadhaa na timu ya watu wengi sana. Ilikuwa linaanza na vikao vya kuweka mipango. Kuandaa bajeti na kuizungusha kwa wadhamini wa makampuni na mashirika tofauti tofauti kuomba msaada wao.
Mara nyingi tulikuwa tunaomba misaada ya kudhamini kutoka kwa makampuni na mashirika zaidi ya mia, mwisho wa siku tulikuwa tunapata mdhamini mmoja au wawili. Na hiyo pia ilikuwa haikidhi bajeti nzima ya kongamano kwa siku mbili.
Kabla sijawa kiongozi sikuwa najua nguvu na kazi iliyokuwa inahitajika kufanikisha kongamano hilo. Nilihudhuria la kwanza kama mgeni na nikaona ni rahisi sana kuandaa. Mwaka uliofuata mimi ndio nilikuwa Katibu Mkuu na shughuli niliiona.
Tulikuwa tunazunguka kwenye ofisi za makampuni na mashirika asubuhi na mchana wakati wanafunzi wengine wakiwa darasani wanasoma au hosteli wamepumzika. Tulikuwa tukirudi hosteli tunaendelea na majukumu ya kufuatilia majibu kwa simu au barua pepe kutoka kwenye makampuni tuliyoomba.
Miezi ikapita na hakuna matunda yeyote yaliyokuwa yanaonekana kwa kazi yetu kubwa tuliyofanya. Timu ikaanza kukata tamaa na kuhisi kuwa tunaweza kushindwa kufanya kongamano lile kwa mwaka husika. Ilifanyika kazi kubwa sana lakini hakuna mafanikio yalikuja.
Tukafunga chuo kwa ajili ya likizo fupi, na tulikuwa na wiki tatu mbele tukirudi ili ifike siku ya tukio. Tulikuwa tumeshawaalika wageni kutoka Kenya, Uganda na Rwanda. Lakini hatukuwa na fedha za kufanya kongamano lile.
Tukakubaliana kuwa tukirudi kutoka likizo tutakaa kikao na kutafakari namna bora ya kutafuta njia mbadala wa tatizo letu. Mimi nikasafiri kwenda Arusha kutembelea familia yangu. Nilikuwa mnyonge sana kwasababu ni mara ya kwanza baada ya miaka mingi kuna uwezekano kongamano kubwa zaidi lisifanyike. Na mimi ndio nikiwa Katibu Mkuu wa kuliandaa.
Ilikuwa ngumu kukaa nyumbani nilipofika Arusha, nikawa nazunguka sehemu mbalimbali kupunguza mawazo. Kuna siku nikaamua kwenda mjini, nikapanda daladala na kushuka sehemu inaitwa Clock Tower. Nikaona kuna kibao kimeandika kuwa ofisi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zipo karibu.
Nikapita karibu na geti la ofisi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, ni sehemu moja nzuri na kubwa sana. Nilivutiwa sana na mazingira yale. Nikapita karibu na geti na kusalimia walinzi na kuendelea na safari yangu.
Hatua kadhaa mbele, wazo likanijia, sisi tunandaa kongamano kwa ajili ya wanafunzi wa maswala ya biashara wa Afrika Mashariki, na wao ni ofisi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, nikijaribu kuongea nao hawawezi kutusaidia?
Ingawa nilikuwa likizo na mapumzikoni nikaona ni fursa kujaribu kuomba udhamini kwao pia. Nikarudi pale getini na kujitambulisha vizuri na kuelezea shida yangu. Wakaniambia niingie ndani kwenye geti la pili kuna mapokezi.
Kumbukumbu mbaya ya watu wa mapokezi ikanijia. Kwenye kuzunguka kuomba udhamini kwenye maofisi ya makampuni na mashirika mara nyingi watu wa mapokezi ndio walikuwa wanatukwamisha.
Walikuwa wanapokea barua zetu na maombi yetu na kukaa nayo tu. Au walikuwa wanatukatalia na kuturudisha bila kutupa nafasi ya kuonana na viongozi husika. Na pia ilikuwa ni kipengele sana wakati wa kufuatilia kwa simu au barua pepe. Akili ikaniambia safari yangu inaenda kuishia kwa mtu wa mapokezi wa pale ofisini.
Mbaya zaidi hii siku ya leo sikuwa na barua wala fomu za kuomba udhamini za hata kumuachia mtu wa mapokezi. Nikajipa moyo na kusema kuwa sina cha kupoteza, nipo likizo na ile ni fursa ya kutalii ofisi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Pale mapokezi nikamkuta dada mmoja mcheshi sana, asili yake ilikuwa ni Rwanda. Alikuwa mrefu, ana nywele ndefu na mrembo haswa. “Habari, naitwa Rogers, Katibu Mkuu wa taasisi ya wanafunzi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwenye maswala ya fedha,” nikajitambulisha.
Alinisikiliza kwa umakini na usikivu sana, nikamuelezea kilichonileta. Akaniambia atanirudia baada ya dakika kadhaa. Na ndani ya dakika thelathini nilikuwa ghorofani kwenye ofisi za watu waliokuwa wanahusika na mambo ya vijana kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Ndani ya nusu saa nyingine walikuwa wamekubali kutudhamini dola elfu saba kuandaa kongamano letu. Walikubali bila kuona barua wala fomu yeyote ya udhamini. Walinipa barua pepe yao na kusema jioni nikitulia niwatumie hivyo vitu.
Miezi mingi sana tulitumia kuzunguka na barua na fomu za kuomba udhamini kwenye maofisi zaidi ya mia bila kupata mafanikio yeyote. Leo hii tulipata dola elfu saba kwenye ofisi ambayo nilienda nikiwa likizo na sina barua wala fomu.
Lile tukio ilikuwa ni miongoni mwa sehemu ya maisha ambayo ina funzo kubwa sana, “ sio kila mafanikio yanakuja kwa kufanya kazi kwa bidii, na sio kila kushindwa au kufeli kunakuja kwa kuwa mvivu”
Timu kubwa iliyokuwa imejiandaa kuhangaika asubuhi na mchana kuzunguka maofisini kuomba udhamini haikufanikiwa. Mtu mmoja aliyekuwa likizo akiwa hana maandalizi yeyote akafanikiwa.
Ni kweli kuwa kufanya kazi kwa bidii huongeza asilimia za kufanikiwa kwenye jambo husika, lakini haimanishi kuwa ni uhakika utafanikiwa. Sio kila mtu aliyefanikiwa alifanya kazi kwa bidii, mateso na muda mrefu sana. Kuna wengine mafanikio yalikuja kwa haraka na namna ya tofauti na wengi.
Na sio kila mtu ambaye hajafanikiwa ina maanisha hafanyi jitihada za kutosha. Kuna watu wanafanya kazi masaa zaidi ya kumi na sita kwa siku. Siku saba za wiki, kuanzia mwanzo wa mwaka mpaka mwisho. Kwa miaka mingi sana. Na bado hawajafanikiwa. Hawa sio wavivu wala wazembe.
Nakumbuka wakati sisi tunafanya kongamano letu mwaka ule kwa fedha tulizozipata kutoka ofisi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, taasisi nyingine nyingi sana zilihairisha au kukatisha ratiba zao kwa kukosa fedha na udhamini. Haikumaanisha walikuwa wavivu.
Kwenye maisha kuna watu wanafanya kazi kwa bidii sana maofisni lakini miaka inaenda na kurudi bila wao kupandishwa cheo wala kuongezwa mishahara. Ila kuna watu wamefika tu kazini na kupata cheo na mishahara kuongezeka.
Kuna watu wanafanya biashara kwa nguvu kubwa sana na kujitolea kwa miaka mingi bila kupata nafasi ya kupata mitaji ya kukuza biashara au kupata wateja wa maana. Ila kuna wengine wanaanza tu biashara na kupata mitaji mingi na wateja wa kutosha.
Kuna watu wanahangaika kanisani, misikitini na wengine kwa waganga kupata mahusiano na bado wanashida. Ila kuna wengine wana mahusiano mpaka yanawashinda. Kuna wengine wanatafuta mtu mmjoja tu wa kuoa, wakati wengine wanaoa wake wanne na bado fursa zinawajia.
Kuna baadhi ya vitu kwenye maisha ni siri, na siri moja wapo ni ya mafanikio na kutafuta. Ukiona umefanikiwa kwenye kitu usijisifie tu kwa kuwa ulifanya kazi kwa bidii. Kama haujafanikiwa na unafanya kazi kwa bidii pia usikate tamaa ukahisi una mkosi.
Na pia ukiona mtu hajafanikiwa kwenye kitu haimaanishi haweki nguvu ya kutosha au ana uvivu sana kwenye maisha yake. Ni ulimwengu ndio unaojua kwanini muda fulani kitu kinakuja na muda mwingine hakiji.
Hauwezi kubadilisha lini kitu kije au kiende kwa nani. Unachoweza kufanya ni kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuongeza uvumilivu pale mambo yanapokuwa magumu.
#iThinkSo
Uwe na furaha.
Uwe na afya.
Uwe huru kutoka kwenye mateso.
Upate amani.
Kama kuna kitu umejifunza, mtumie mtu mmoja wa karibu yako na yeye ajifunze.
Rogers Katuma
Chieftain, Mphami Estate.
