Kinachoonekana cha ajabu au kijinga kwako ni cha kawaida na kueleweka kwa wengine.

Nina mdogo wangu mmoja ambaye anapenda sana michezo ya kukimbiza magari na kutelezesha matairi ya gari kwenye lami. Hutumia muda mwingi na fedha nyingi sana kwenye gari lake. Huwa anaangalia kila aina ya video yenye kuonyesha watu wakifanya kama yeye pia. Mwanzoni nilikuwa naona ni kitu cha ajabu sana. 

Nina rafiki mmoja ambaye anapenda sana pikipiki kubwa. Haumwambii kitu chochote kuhusu pikipiki kwenye maisha yake. Mwili huwa unamsisimka akisikia mlio wa pikipiki kubwa inapita, hata kama ni mbali kiasi gani. 

Nilikuwa na jirani mmoja ambaye ni mvuvi. Amefanya kazi ya kuvua baharini kwa miaka zaidi ya thelathini. Huwa anachukua mtumbwi wake mdogo na kwenda nao katikati ya bahari huko ili kuvua. Kuna muda hutumia ndoano na kuna muda anatega nyavu. Na uvuvi wake ni usiku sana.

Mimi nilikuwa naona ile ni kazi ya ajabu sana kwa yote ninayoyajua na nisiyoyajua kuhusu bahari. Lakini yeye anasema anamshangaa zaidi mdogo wake ambaye yeye huwa anazama chini kabisa baharini bila mtungi wa gesi wakati wa kuvua. Kwake yeye, mdogo wake huwa hamuelewi. 

Kwangu mimi, hao wote watatu wanafanya vitu vya kushangaza na ajabu sana. Kuna muda pia nilikuwa nahisi ni vitu vya kijinga. Sikuwahi kuona sababu ya mtu kupenda kutelezesha gari na tairi kwenye lami mpaka moshi unatoka. 

Sikuwahi kufikiria kufanya kazi ya kuvua samaki baharini, usiku wa manane. Sikuwahi kufikiria kwanini mtu apende kuendesha pikipiki kubwa zenye mwendo kasi na hatari zaidi. 

Inawezekana wewe ni kama mimi pia, kitu kimoja au viwili kati ya nilivyokuwa naviona vya ajabu na wewe unaviona ni vya ajabu pia. Na kuna vitu vingi zaidi huko nje bado unaviona vya ajabu. 

Nakumbuka na mimi nilivyokuwa nawasimulia kuhusu namna nilivyoruka kutoka kwenye ndege angani wote watatu waliniona mimi wa ajabu sana. Mdogo wangu mpenda magari, rafiki yangu mpenda pikipiki na jirani mvuvi wote walisema mimi nilifanya kitu cha hatari na kushangaza kushinda vyakwao. Mimi nilijaribu mchezo wa kuruka kutoka kwenye ndege angani.

Kuruka kwenye ndege ni mchezo ambao unahusisha mtu kupanda kwenye ndege ambayo inapaa mpaka angani. Ukifika juu, unaruka kutoka kwenye ndege huku ukiwa na mwamvuli wa kurukia ambao utaufungua zikiwa zimebaki hatua chache kufika ardhini. 

Mimi nilienda kufanya hivyo Zanzibar miaka kadhaa nyuma. Tulipaa angani kwa urefu wa futi elfu kumi na saba ambazo ni karibu na urefu wa mlima Kilimanjaro ambao ni mlima mrefu zaidi duniani kwa milima iliyosimama huru. 

Ndege tuliyotumia ni ndogo sana, hii ilikuwa inawasaidia wao kupunguza gharama. Kwenye ile ndege kulikuwa hakuna mlango wa kutenganisha ndani na nje. Ukiingia kwenye ndege sehemu ya kurukia inakuwa wazi kuanzia ndege inaanza kupaa mpaka urefu wa tayari kuruka. 

Muda ukifika unaruka kutoka kwenye ndege ukitanguliza kichwa chini, mikono imebana kifuani na miguu imenyoka kama mshale. Unaruka hivyo kwa sekunde kadhaa, kwa wale wanaojifunza. Kwa wazoefu huruka hivi kwa dakika nyingi zaidi. 

Baada ya sekunde au dakika kadhaa unafungua mwamvuli na kuanza kuvuta kamba zake ili kuongoza upande na spidi ya kushukia. Unatumia muda huu kuangalia mandhari nzuri kabisa ya dunia ukiwa mbali sana angani. 

Kwenye mchezo huu kuna vitu vingi sana ambavyo vinaweza kwenda kombo. Na kila kitu ambacho kinaweza kwenda kombo kina nafasi kubwa sana ya kusababisha kifo. 

Inawezekana kwa kusoma tu hii umeshapatia picha na kusema hilo ni jambo la ajabu sana mtu kuamua kufanya. Au inawezekana ukawa mkali zaidi na kusema ni jambo la kijinga, ni haki yako. 

Nakumbuka na mimi nilipofika chini salama na mwamvuli na kumuuliza mwalimu wetu yeye huwa anafanya hivyo mara ngapi kwa wiki, akasema biashara ikiwa nzuri huwa anaruka mara nne kwa siku. Kwangu mimi pia nikafikiria kuwa hili ni jambo la ajabu sana. 

Aliona mshtuko wangu, akaniambia mpenzi wake naye anafanya kazi hii yupo Urusi. Yeye amesharuka mara mia tatu arobaini ndani ya miaka michache tu. Kitu ambacho na yeye alisema ni cha ajabu sana. 

Funzo kubwa sana kwenye maisha ni kutambua kuwa mtazamo wako kuhusu kitu fulani sio mtazamo wa watu wote. Vitu ambavyo wewe unaona vya ajabu sana au vya kijinga sana kuna wengine wanaona ni kawaida tu. 

Jukumu lako kwenye maisha ni kutafuta maana ya jambo lako na kulifanya. 

Kama wazo lako la biashara linaonekana la ajabu au la kijinga sana kwa watu na wewe unaona inawezekana, usikate tamaa, endelea kulifanya wazo lako liwe uhalisia. 

Kama malengo yako kazini yanaonekana ni ya ajabu au ya kushangaza kwa watu lakini wewe unaamini ndio ndoto yako, usijali, endelea kusimamia ndoto yako. 

Kama mahusiano yako yanaonekana hayaeleweki au ya kushangaza kwa watu lakini wewe na mwenzako mnaona mnaelekea nchi ya ahadi, usikate tamaa, endelea kupalilia huba. 

Ndoto yeyote uliyokuwa nayo kwenye maisha, hata kama ni ya kushangaza na mpaka watoto wanaweza kusema ni ya kijinga, usiiache. Kushangazwa au kuona ujinga ni mtazamo wa mtu au watu lakini sio uhalisia. 

Usiruhusu mtu akutengenezee maana ya kitu kipi ni cha kawaida, kipi cha kushangaza au kipi cha kijinga. 

Watu wanachokiona cha kijinga na kushangaza haimaniishi ni cha kijinga na kushangaza kwako. 

#iThinkSo

Uwe na furaha

Uwe na afya

Uwe huru kutoka kwenye mateso

Uwe na amani. 

Kama kuna kitu umejifunza kwa kusoma hii mtumie mtu mmoja unayemjali na yeye ajifunze. 

Rogers Katuma

Chieftain and Financial Artist

Mphami Estate.


Discover more from iThinkSoo

Subscribe to get the latest posts sent to your email.