Nilianza kusoma darasa la kwanza kwenye shule ya msingi ambayo ilikuwa imeanzishwa mwaka mmoja nyuma. Darasa letu lilikuwa ndio la pili kujiunga na shule, hivyo tulikuwa tunapewa uangalizi wa utofauti sana.
Darasani tulikuwa watu ishirini na sita, watatu wakiwa ni wasichana na wengine wote walikuwa wavulana. Miaka kadhaa mbele waliongezeka wasichana wawili na wavulana wawili.
Tulikuwa tunajuana kwa ukaribu sana na kujua kila mtu anakaa wapi. Na hiki kilikuwa ni kipindi ambacho hamna mitandao ya jamii wala ramani za Google. Ilikuwa ni utamaduni kutembeleana au kufanya vitu kwa pamoja baada ya shule. Na kwa kuwa tulikuwa na wasichana wachache ilikuwa ni faida kwa yeyote aliyekuwa anajua wanawake wanakaa wapi.
Nakumbuka siku ya mwisho ya mtihani wa darasa la saba tulikuwa na furaha sana. Tulifikiria kuwa ule ni mwisho mzuri sana baada ya miaka saba ya urafiki na matukio mengi. Tulianza kama watu baki na kumaliza kama marafiki au ndugu. Wengine walimaliza wakiwa wapenzi pia.
Baada ya mtihani wa mwisho baadhi yetu tulitoka na kwenda kutafuta vibanda vya kupigia picha. Tulikuwa kumi na mbili kati ya thelathini na moja tuliomaliza. Tulitembea kilomita kadhaa kupata mpiga picha. Alitupiga picha huku akitabasamu na kusema tumekuwa na mwisho mzuri na wenye mafanikio.
Nikiitazama picha ile leo, inaonekana kama ulikuwa mwisho mzuri. Lakini nikifikiria kwa undani sio sahihi. Ile ndio ilikuwa mara ya mwisho kuwasiliana na asilimia tisini ya watu niliokaa nao kwa miaka saba. Ilikuwa ni kipindi ambacho tulikuwa hatuna simu wala mitandao ya jamii.
Miaka ishirini mbele sasa, naongea na watu wawili tu katika lile kundi la watu thelathini na moja niliosoma nao shule ya msingi. Wengine nasikia wameoa au kuolewa na wana watoto. Wengine hawajawahi kuwa kwenye mahusiano ya muda mrefu.
Kuna wengine wana kazi, wengine hawana kazi za kudumu. Wengine wafanya biashara, wengine wamepata matatizo ya akili, na wengine hakuna anayejua walipo. Kuna mmoja alifariki peke yake kilomita zaidi ya elfu moja mbali na nyumbani. Ule haukuwa mwisho mzuri.
Nilijiunga na shule ya sekondari ya Pugu, ambayo ilikuwa ni shule pekee ya serikali ya bweni kwa wavulana mkoa wa Dar es Salaam. Mazingira ya shule hii yalikuwa ni tofauti kabisa na shule ya msingi ya St Joseph niliyotoka.
Kwanza mazingira ya bweni ya wavulana tupu ni ya upekee sana. Pia shule ilikuwa ina wanafunzi wengi sana na ilikuwa ngumu kufahamiana au kufahamika. Kipindi mimi nasoma darasa letu lilikuwa na mikondo mitano, A mpaka E, na kila mkondo ulikuwa na wanafunzi sio chini ya sitini.
Shule hii tulikuwa kuna changamoto nyingi kushinda raha. Maji yalikuwa ya shida, vyoo vilikuwa vya zamani na vichafu muda mwingi. Walimu wazuri walikuwepo lakini ilikuwa nadra sana kuwaona darasani. Chakula kilikuwa sio kizuri wala kuvutia.
Ilivyofika wakati wa kumaliza kidato cha nne nina imani kila mtu aliona kuwa ule ulikuwa ni mwisho bora zaidi kwenye maisha yake. Miaka mingi mbele nikitafakari sioni kama ulikuwa mwisho bora.
Kwenye shule ambayo ilikuwa na wanafunzi zaidi ya elfu moja mia tano kuanzia kidato cha kwanza mpaka sita ninaongea na watu sio zaidi ya watatu. Kuna wengi ninaowajua ambao wamefariki, na idadi ni kubwa zaidi kwa nisiowajua. Kuna watu wapo jela, kuna wengine wana matatizo ya akili na wengi sana hawana kazi. Huo sio mwisho mzuri.
Chuo kikuu cha Dar es Salaam haikuwa tofauti. Tuliingia kwa maelfu na tulimaliza kwa mamia. Siku ya mahafali ilikuwa ni kama mwisho bora zaidi kwenye maisha yetu. Kuna watu walipata kazi, kuna watu hawakufanikiwa. Kuna watu walianzisha biashara na wengine hatujui walipo. Kuna rafiki zetu walipoteza maisha. Huo sio mwisho mzuri.
Na hata nilipoanza kazi mzunguko uliendelea. Tulianza tukiwa watu kumi na tano mwaka wetu, tukapewa mafunzo kwa pamoja ofisini kwa mwaka mzima. Miaka kumi na mbili mbele siwezi kusema ulikuwa mwisho mzuri. Wachache sana bado wapo kwenye ofisi ile. Baadhi walibadilisha waajiri, wengine walijiajiri na mmoja wetu alifariki. Huo sio mwisho mzuri.
Nikiangalia safari yangu ya maisha ni rahisi kuona kuwa kitu ambacho kilikuwa kinaonekana ni mwisho mzuri wakati kinatokea kinaishia kuwa sio mwisho mzuri. Kila mwisho kuna mambo mengine mengi yanafuata ambayo hutoa taswira tofauti.
Hii haimanishi kuwa hamna kitu kizuri kinaweza kutokea kwenye maisha. Safari nzuri ya maisha ipo, lakini mwisho mzuri haupo. Ni ngumu kuchagua mwisho uwe vipi kwenye maisha lakini tumepewa uwezo wa kuchagua safari iwe namna gani.
Nikikumbuka kuamka asubuhi na kuwapitia rafiki zangu kwenda shule, kuchelewa kurudi nyumbani sababu ya kucheza barabarani wakati nipo shule ya msingi ile ilikuwa safari nzuri. Upole na upendo wa masista wa St Joseph, ucheshi na vituko vya mwalimu Ponera ambaye muda mwingi alikuwa amelewa ni kumbukumbu bora sana ya maisha yangu ya shule ya msingi. Safari ya elimu ya msingi ilikuwa bora.
Maisha yangu ya sekondari ya Pugu yamejaa kumbukumbu nyingi sana pia. Kwenda kwenye mechi na shule mbalimbali, mchakamchaka siku za wikiendi asubuhi na kuingia disco na warembo wa shule ya sekondari ya wasichana ya Jangwani. Safari za kutoroka shule ili kwenda tuisheni mchikichini, Kariakoo ilikuwa ni hekaheka zenye ukumbusho. Safari ya elimu ya sekondari ilikuwa bora.
Chuo kikuu maisha yalikuwa ya utofauti sana. Drama na wanawake warembo na wenye historia tofauti tofauti, mashindano ya mpira wa miguu kutoka idara tofauti tofauti ilikuwa ni furaha sana. Mabusu na mapenzi kwenye hosteli za wanaweka hauwezi kusahau hivyo vitu. Safari ya elimu ya chuo kikuu ilikuwa bora.
Maisha ya kuanza kazi ya kwanza, mafunzo mwezi mzima na kupokea mshahara ni kumbukumbu kubwa sana. Kutengeneza mazingira ya kupata hela ofisini kwa ajili ya safari, kufanya kazi nje ya masaa ya muda na kuhangaika na siasa za maofisini ni kumbukumbu ya milele. Safari ya kuajiriwa ilikuwa bora.
Kwa hivi vyote nimejifunza kitu kubwa sana kwenye maisha. Maisha yetu ni safari, tupo njiani tukikusanya uzoefu, kumbukumbu, historia, stori zenye maumivu, mshangao na furaha. Mahafali kwa wanafunzi, kupandishwa kazi kwa wafanyakazi, faida kwa wafanyabiashara au hatua tofauti tofauti kwenye familia.
Ile safari ya kutafuta cheti na kufanikiwa kwenda kwenye mahafali, ile safari ya kufanya kazi ili upandishwe cheo, ile safari ya kuanza biashara ili upate faida ndio vitu vya umuhimu kwenye maisha.
Chochote unachofanya sasa hivi usifikirie sana mwisho wake utakuwaje, tumia muda mwingi kufikiria namna ya kufurahia safari sasa hivi.
Kama unasoma, usifikirie sana kuhusu mitihani, vyeti na mahafali. Fikiria kuhusu muda na kumbukumbu unazotengeneza na wanafunzi wenzako. Ratiba na maisha unayoishi ukiwa kama mwanafunzi. Vitu unavyojifunza na namna vitakusaidia kwenye maisha.
Kama unafanya kazi usifikirie sana kuhusu kupandishwa cheo au mshahara. Tengeneza mazingira ya kufurahia kazi unayoifanya, na watu unaofanya nao maana hao ndio watakupa kumbukumbu za furaha miaka mingi zaidi mbeleni. Ujuzi unaotengeneza sasa hivi ambao unajenga msingi wa kuajiriwa sehemu nyingine au kujiajiri mbeleni.
Kama unafanya biashara usiwaze sana kuhusu faida utakayoipata au bidhaa mpya utakayoileta. Fikiria kuhusu siku kwa siku na matatizo unayoyatatua, watu unaokutana nao na kumbukumbu unazotengeneza.
Maisha ni safari, na furaha ya kweli ipo katikati ya unapoanza safari na mwisho. Mwisho wa safari sio malengo ya safari. Kumbukumbu, historia, furaha, huzuni na kila kitu kinatokea katikati ya safari.
Achana na mawazo na matangazo ambayo dunia imetufanya tuamini kuwa kuna kitu kinaitwa mwisho mzuri. Ukianza kuamini kuwa kuna mwisho mzuri utakuja kuumia sana ukikutana na na ukweli kuwa ule mwisho sio mzuri.
Utapata cheti na kufanya mahafali ya shule ya msingi au sekondari na bado usipate chuo ulichokuwa unataka. Kama upo chuo, unaweza kumaliza na kupata cheti na bado ukakosa kazi. Huo sio mwisho mzuri ambao uliahidiwa.
Unaweza kudhani kuwa ukiwa kwenye mahusiano basi mwisho mzuri ni kuwa kwenye ndoa na kufurahia mpaka mwisho wa dunia. Utafadhaika sana ukija kuingia kwenye ndoa na kugundua migogoro, changamoto na maumivu ni sehemu ya ndoa.
Kumbuka kuwa hakuna mtu atatoka kwenye hii dunia akiwa hai. Na huo ndio mwisho mkubwa kuliko yote wa maisha ya binadamu. Na kiuhalisia sio mwisho bora wa kuufikiria kwa watu wengi.
Ila kitu kizuri ni kuwa una uwezo wa kuwekeza mawazo na akili zako wa safari ya aina gani unataka kuwa nayo kwenye maisha haya mafupi. Mwisho sio mzuri kwakuwa utakufa tu, lakini safari ya maisha unaweza kuifanya vizuri.
Kumbukua, kuna safari nzuri kwenye maisha lakini hakuna mwisho mzuri.
#iThinkSo
Uwe na furaha
Uwe na afya
Uwe huru kutoka kwenye mateso
Uwe na amani.
Kama kuna kitu umejifunza mtumie mtu wako wa karibu na yeye ajifunze.
Rogers Katuma
Chieftain and Financial Artist
Mphami Estate
