Bibi yangu mzaa baba alifariki miaka michache iliyopita akiwa na miaka mia moja na tatu. Mwaka mmoja kabla ya kifo chake alikuwa amepata mshituko na kupooza upande wake wa kushoto. Hivyo alikuwa hawezi kutembea, muda wote yupo ndani.
Wiki moja kabla ya kupata mshtuko na kupooza alitoka kushinda kesi mahakamani. Kesi ilikuwa inahusu viwanja ambavyo alikuwa anamiliki Kigamboni. Kuna mzee mmoja alienda mahakamani na kusema baadhi ya viwanja ni vyake na sio vya bibi.
Historia ya bibi na yule mzee ni ya kufuraisha sana. Wao wawili ndio walikuwa miongoni mwa watu wakwanza kuhamia maeneo yale ya Kigamboni, miaka ya sabini. Maeneo hayo yalikuwa ni mapori kabisa. Walianza kulima na kuweka makazi, huku taratibu wakiwauzia watu.
Yale maeneo yalivyoanza kuwa mji na watu kuongezeka biashara yao kubwa ilikuwa ni kuuza kwa watu. Nakumbuka wakati nipo chuo kikuu bibi alinishawishi na mimi ninunue kiwanja kwake pia, akimshirikisha mtoto wake wa mwisho anishawishi. Nikanunua.
Kwahiyo ilipofika kipindi ambacho wakapelekana mahakamani sababu ya viwanja walikuwa na migogoro mingi sana ya maeneo mengi sana. Maana wakati wanaanza kulikuwa hakuna njia nyepesi ya kupima viwanja wala kuweka alama na mipaka.
Bibi alikuwa na ushahidi mwingi sana alipofika mahakamani, na akafanikiwa kushinda ile kesi. Yule mzee akakubali kushindwa, lakini akasema kitu ambacho mpaka leo ni fumbo. Alimwambia bibi, “Umeshinda kiwanja, lakini utapoteza kitu cha thamani zaidi.”
Na kilichofuata ni kuwa wiki moja baada ya bibi kushinda ile kesi akapata mshtuko na kupooza upande wote wa kushoto. Zile safari za mahakamani ndio zilikuwa safari zake za mwisho, baada ya kupoza alikuwa anashinda ndani tu.
Aliugua kwa mwaka mzima kabla ya umauti kumfika. Nakumbuka kila nikiwa naenda kumtembelea alikuwa na huzuni sana. Hakupenda kuzungumzia kuhusu viwanja, mashamba wala ile kesi aliyoshinda. Alikuwa amebaki na mashamba na viwanja vingi bado lakini hakuwa na furaha navyo.
Kuna baadhi ya watoto wake walikuwa wanamuonyesha wazi kabisa kuwa wanasubiri afariki ili wachukue mali zake. Na ubaya ni watoto wake hao hao ambao ilibidi wapeane zamu ya kumuuguza na kumtunza.
Walikuwa wanamsaidia chakula, kumbadilisha nguo, kumpeleka chooni, kumuogesha na baadhi ya siku kumtoa nje apunge upepo na kumrudisha ndani. Na walikuwa wanamsema, wanamdharau na kumkejeli sana.
Hakuna aliyekuja na wazo la kuuza baadhi ya viwanja au shamba ili zipatikane hela za kumtunza bibi vizuri. Mali zake hazikuwa na msaada mkubwa kwake kwa kipindi hiki. Hiyo nayo iliongeza huzuni aliyokuwa nayo.
Tarehe ishirini na nane ya mwezi wa nane miaka kadhaa nyuma akaaga dunia akiwa usingizini. Kitu cha kwanza kilichonijia kichwani nilipopewa taarifa ya kifo chake ni kauli ya yule mzee, “Umeshinda kiwanja, lakini utapoteza kitu cha thamani zaidi.”
Bibi alishinda ile kesi lakini alipoteza furaha, alipoteza afya na mwisho alipoteza maisha yake. Ni kawaida kwa binadamu kujiuliza maswali mengi sana;
Je yule mzee alihusika kwa lolote kumfanya bibi kupooza mwili upande wa kushoto?
Je yule mzee alihusika kwenye kifo chake?
Je ilikuwa ni uzee wa bibi kuwa na miaka mia na tatu?
Nadhani mpaka mwisho wa dunia hatutakuwa na majibu. Tuliendelea na mazishi na nikiwa kama mjukuu mpendwa wa bibi nikateuliwa kusoma wosia wa marehemu. Nilijitahidi kuelezea maisha yake kwa njia nzuri na kusema vitu ambavyo yeye angevisema.
Miezi kadhaa ilipita baada ya kifo na mazishi ya bibi, kuna mtu akafungua kesi kuhusu kiwanja kule Kigamboni. Hiki kiwanja kilikuwa ni kile ambacho bibi alinishawishi mimi ninue kutoka kwake, na mwanae wa mwisho akiwa shahidi.
Huyu mzee akasema kuwa aliuziwa kile kiwanja na bibi kabla hajafariki na alikuwa na mikataba, ushahidi wa malipo na taarifa kutoka serikali za mitaa. Hii ilinishtua sana, lakini nikakumbuka ugomvi wa bibi na yule jirani yake.
Nikasema sitaki kupitia alichopitia bibi, hivyo sitajishughulisha na kushindana mahakamani au serikali za mtaa kuhusu kile kiwanja. Mama yangu akasema nakuwa myonge sana, akasema yeye atafuatilia.
Mama alihangaika sana, alitafuta mashahidi wa serikali za mtaa na kuuliza ndugu wote wa bibi kama wanajua kuhusu bibi kuuza kile kiwanja tena. Hakupata ufumbuzi na nikaona inaanza kumuongezea huzuni.
Nikamsimulia mama mkasa wa bibi na yule jirani yake kabla ya kupooza. Nikamwambia aachane na kile kiwanja. Kwa shingo upande alikubali, na bado aliniona nakubali kinyonge sana.
Mimi sikuchukulia ile kama unyonge, niliona hekima na funzo kwenye maisha na kifo cha bibi yangu. Kwamba, bibi yule kuna muda alikuwa ni miongoni mwa watu wachache sana Kigamboni wenye kumiliki maeneo mengi sana.
Kwenye lile eneo ambao yeye alihamia kwa takwimu ni karibu watu watano kati ya kila kumi walinunua kiwanja au shamba kutoka kwake. Lakini mali zote zile bado alipoteza furaha na amani yake kwa kugombea viwanja vingine na kupooza na hizo mali kushindwa kutumika kumsaidia wakati anazihitaji zaidi.
Hiyo imenifanya niwe makini sana kwenye vitu ninavyotafuta, haijalishi ni vizuri kiasi gani huwa ninajiuliza furaha na amani nitakayopoteza kwa kumiliki hivyo vitu. Au natakiwa kupoteza furaha, amani, na afya kiasi gani ili kumiliki kitu?
Inanipa amani angalau kuwa bibi aliishi kufika miaka mia na tatu, mimi ndio kwanza nipo kwenye miaka thelathini. Nina safari ndefu ya maisha an vitu vya kupitia.
Wakati nasoma wosia wa bibi, niliongezea maneno ambayo najua angekuwa hai angeyasema, “Siri ya maisha mazuri na marefu ni kutafuta furaha na amani bila kumiliki kitu.”
Furaha ya kweli isiambatane na mali, ije yenyewe.
Kwasababu, nini thamani ya mali kama hauna furaha na amani nayo?
#iThinkSo
Uwe na furaha.
Uwe na afya.
Uwe na amani.
Uwe huru kutoka kwenye mateso.
Kama kuna kitu umejifunza mtumie mtu mmoja unayemjali na yeye ajifunze.
Rogers “Ronn Dinero” Katuma
Chieftain and Financial Artist
Mphami Estate
