Wiki iliyopita nilisimulia kuhusu stori ya bibi yangu. Alifariki miaka michache nyuma akiwa na miaka mia moja na tatu, miaka nadra sana kwa watu kuishi kwa kizazi hiki. Miezi kadhaa kabla ya kifo chake, bibi alikuwa amepooza mwili wote upande wa kushoto.
Alikuwa hawezi kutembea wala kufanya shughuli za kila siku za kujitunza. Alikuwa anategemea watoto wake wakike na wakiume kumtunza. Alikuwa anahitaji mtu wa kuja kumuandaa asubuhi baada ya kuamka, kumpa chai na kumvalisha nguo mpya.
Pia alikuwa anahitaji mtu mwingine wa kuja mchana kumsaidia kwenye maswala ya choo, kumsafisha na kumuandalia chakula cha mchana.
Jioni alikuwa anahitajika mtu mwingine wa kuja kumuandalia chakula cha usiku, kumtandikia kitanda na kumuwekea mazingira mazuri ili alale. Ratiba hii ilikuwa inajirudia kila siku, tangu siku aliyopooza mpaka umauti ulipomfika.
Hii ratiba na haya mahitaji ya kumtunza bibi yalikuwa yanamgusa kila mtu kwa njia yake. Ilikuwa ngumu kumpeleka na kumuacha hospitali hivyo ilibidi aendelee kubaki nyumbani.
Ilikuwa ni kawaida sana kukuta watoto wake wakibishana au kugombana kwa sababu kuna mtu hakufanya majukumu yake vizuri.
Kuna siku ilikuwa kawaidia kuona watoto wake wakimkemea na kumlaumu bibi kwa kitu alichosema au alichofanya ambacho kilipelekea wao kupata shida ya kumtunza. Na kadri siku zilivyokuwa zinaenda ndio hasira na changamoto zao zilikuwa zinaongezeka.
Na hiyo ilikuwa ni sehemu moja ya changamoto, ambayo ni uhitaji wa muda na mtu wa kumtunza bibi kwakuwa alikuwa amepooza na hawezi kutoka nje kuendelea na majukumu yake ya kila siku.
Changamoto nyingine ilikuwa ni maswala ya fedha. Gharama nyingi sana zilikuwa zinahitajika kwa ajili ya kumtunza bibi. Mavazi, gharama za madaktari kuja kumuona nyumbani, chakula na vinywaji pia.
Ilikuwa ni kawaida kwa watoto wake kuomba msaada kwa ndugu na jamaa. Na ilikuwa kawaida sana kwa sisi wajukuu kupokea simu na meseji asubuhi sana au usiku wa manane kuambiwa kuhusu upungufu wa kitu au mahitaji mapya.
Na karibu watoto wote wa bibi walikuwa hawana kazi zenye mikataba wala biashara ambazo zinaweza kujiendesha zenyewe. Walikuwa wanahitajika watoke ili na wao wakajipatie kipato chao na cha familia zao. Hiyo iliongeza changamoto kwasababu ilibidi wapeane zamu.
Maisha ya kila mtu ambaye alikuwa karibu na bibi yalipata madhara. Mimi sikuwa kwenye jukumu la kumuuguza pale nyumbani lakini zile simu za uhitaji na changamoto zake zilikuwa ni kitu cha kuamka na kulala nacho.
Na haya yote ni mimi naelezea kwa mtazamo wangu, hatukupata nafasi ya kuongea na bibi kujua na yeye anajisikiaje kupitia hali ile. Kuwa ndani siku nzima, kila wiki, kila mwezi. Kutokuwa na uwezo wa kujihudumia. Kuhitaji msaada kwenye kila kitu. Najua ni hali ngumu sana mtu yeyote anaweza kupitia.
Ni rahisi kusema kwasababu yeye aliishi miaka zaidi ya mia tayari basi ilikuwa ni kitu kinachoeleweka. Vipi kuhusu mimi na wewe?
Likitokea tukio lolote la kiafya ambalo likafanya uhitaji msaada wa watu na kukuzuia wewe kufanya shughuli zako za kila siku itakuwaje?
Kama umeajiriwa, kuna sera za mwajiri za kuhusu siku unazoruhusiwa kupewa ruhusa ya kuuguza mgonjwa au kujiuguza. Ukiumwa kwa muda mrefu mwajiri anahaki ya kusimamisha mkataba wako wa kazi.
Kama umejiajiri najua ni asilimia nyingi sana kuwa biashara yako inahitaji uwepo wako wa kila siku ili iendelee. Vitu vingi vinaenda kwasababu wewe upo na una pambana. Ukiumwa kwa muda mrefu vitu vyote hivyo navyo vitasimama.
Na hiyo ni sehemu moja ya changamoto, vipi kuhusu fedha?
Una akiba kiasi gani ndani?
Una akiba ya kuweza kupambana na ugonjwa wa aina gani?
Akiba yako inaweza kuhimili kwa muda gani ukipitia changamoto?
Na hiyo ni kuhusu wewe tu, vipi kuhusu watu wako wa muhimu wanaokutegemea pia?
Watu wengi tunachangamoto za kifedha wakati ambao hatuna changamoto za kiafya za kutuweka ndani kwa wiki au miezi mfululizo.
Umewahi kufikikiria itakuwaje matatizo ya afya yakaongezeka kwenye hali yako ya kifedha unayopitia?
Iwe unapenda au haupendi, ni muhimu kufikiria kwa undani kuhusu fedha na afya yako.
Ni muhimu kuishi maisha ambayo yanaweka kipaumbele kwenye afya yako ili kuzuia magonjwa ambayo yanazuilika na kupunguza nafasi kwa magonjwa mengine.
Ni muhimu zaidi kujenga maisha yako ya kifedha na uchumi ili kuwa kwenye nafasi nzuri ya kupambana na changamoto za kiafya za kwako na watu wako wa karibu pale itakapohitajika.
Changamoto za kifedha na afya sio za swala la kama litatokea au halitatokea. Ni swala la kuwa litatokea lini na ukiwa kwenye nafasi gani.
Ni bora kujiandaa.
#iThinkSo
Uwe na furaha.
Uwe na afya.
Uwe huru kutoka kwenye mateso.
Uwe na amani.
Kama kuna kitu umejifunza mtumie mtu wako wa karibu naye ajifunze.
Rogers “Ronn Dinero” Katuma
Chieftain, Financial Artist and Storyteller
Mphami Estate
