Tulikuwa tumeshachelewa kutoka hotelini, kitu cha mwisho ambacho hatukutaka kututokea ni kuchelewa kwenye treni ya mwendo kasi. Sehemu moja kubwa sana ya safari yetu ya utalii nchini Dubai ilikuwa ni kwenda kuangalia sinema mpya ya Avengers kwenye ukumbi maarufu sana ndani ya Dubai Mall.
Siku ya kwenda kuangalia sinema tulihisi tumetoka kwa wakati hotelini kwenda ukumbini. Wakati tunatoa ramani zetu za utalii wa jiji la Dubai kuona treni za mwendo kasi zipo wapi tukagundua tuna kama dakika ishirini hivi kuwahi kabla ya sinema haijaanza.
Utaratibu wa kupata kadi na tiketi za treni ya mwendo kasi ulikuwa rahisi sana. Lakini dakika chache ndani ya treni tukagundua kuna kitu hakipo sawa. Kuna sehemu ramani ilikuwa inaonyesha kuwa tunatakiwa kukata upande wa kushoto, lakini hapa ilikuwa inaenda upande wa kulia.
Changamoto ni kuwa treni hii ilikuwa inaendeshwa kiuweledi mkubwa sana. Ukikosea sehemu ya kushuka au treni uliyopanda inabidi usubiri mpaka kituo kingine na kupanda treni nyingine. Tukasubiri mpaka kituo kilichofuata, tukauliza na kupata msaada. Dakika kumi na tano nyingine zikapotea hapo.
Ramani yetu ya utalii ilionyesha kuwa pale tulipo mpaka Duabi mall ni dakika tatu. Ina maanisha tutabakiwa na dakika kama mbili kutoka getini mpaka kuupata ukumbi wa sinema. Tulivyoshuka tu kwenye treni tukaanza kukimbia kuwahi ukumbini. Hapo ndo kila kitu kikaenda kombo.
Wakati huo Dubai Mall ndo ilikuwa mall kubwa zaidi kushinda zote duniani. Kuna milango mingi ya kuingilia na kutokea, kuna maduka, kumbi nyingi na sehemu nyingi sana. Kwa mtalii kujua sehemu husika ulipo na njia sahihi ya kupita kufika unapotaka kwenda ni changamoto sana.
Tukafuata njia ya kwanza kwenye ramani na baada ya dakika tano tukajikuta tumerudi pale pale tulipoanzia. Tukatafuta njia nyingine tukaenda kutokea kwenye hoteli na sio ukumbi wa sinema. Baada ya dakika kumi nyingine za kuhangaika na ramani tukampata mlinzi akatusaidia kutuelekeza.
Tulipofika kwenye ukumbi wa sinema wakasema imeshaanza kama dakika ishirini zilizopita. Tukaanza kuharakisha kununua bisi na juisi. Tukaanza kuharakisha kuingia ukumbini. Kulikuwa na giza kubwa sana, ikawa changamoto kupata siti zetu. Ikabidi kuwasha tochi za simu kutafuta, kitendo kilichowakera watu wengi mle ukumbini.
Mpaka tunafanikiwa kukaa kwenye siti karibu dakika thelathini zilikuwa zimeisha. Tumekaa tu, tukagundua kuwa tumesahau miwani ya 3D ya kuangalizia muvi pale kaunta wakati tunanunua bisi na vinywaji. Ikabidi mimi nirudi tena na kuifuata, muda mwingine ukapotea pale.
Ile sinema ilikuwa ni ya masaa karibu matatu, lakini zile dakika thelathini za mwanzo tulizokosa ndio zilibeba msingi mzima wa stori. Tuliangalia ile muvi mle na tulikuwa hatuelewi. Tulivyorudi Tanzania baada ya wiki ikabidi kutafuta ukumbi mwingine wa sinema kuiangalia ile muvi kuanzia mwanzo tena.
Kile kitu kiliniumiza sana, nikajiapia kuwa nitajitahidi kupangilia vizuri ratiba zangu na maisha yangu nisipitie ile changamoto tena. Hususani kwenye vitu vya muhimu. Ile hali ya kuharakisha kitu, kukimbia na kuhisi kuchelewa ni mbaya sana. Na hiyo ndio dalili kuu ya kuchelewa.
Kwenye kitu chochote ninachofanya nikiona naanza kuharakisha najua nimeshachelewa. Mipangilio mizuri na ratiba sahihi haitakiwi kufanywa kwa kuharakishwa. Na mambo mengi ya kuharakisha hayanaga matokeo mazuri kwenye maisha.
Ningejipanga vizuri kule Dubai ningetoka mapema ili kuwa na muda wa kufidia changamoto za treni ya mwendo kasi, kuzunguka Dubai mall mabayo ni kubwa na sikuizoea, kutafuta siti kwenye ukumbi wa sinema na kuhakikisha sijasahau miwani wala tiketi.
Sasa hivi napangilia vitu vyangu vikubwa au vidogo kuhakikisha siwi kwenye haraka. Kama naenda kukutana na mtu, huwa natoka mapema kuwa na muda wa kutosha nikikutana na foleni au chombo cha usafiri kikikutana na hitilafu.
Kwenye malengo na ndoto yangu huwa naweka muda na bajeti mara mbili au tatu ya kawaida kujiandaa ikiwa nitakutana na changamoto ambazo siwezi kuzipangilia au kuzitegemea. Hii imenipunguzia presha kubwa sana na kuniondolea changamoto ya kufanya vitu kwa haraka.
Najua na wewe umeshapitia vitu vingi sana ambavyo ulijikuta unaharakisha. Ukikaa chini na kutafakari utagundua kuwa mara zote ulizokuwa unaharakisha vitu haikuwa na mwisho mzuri kwako au haukuwa na amani.
Na dalili ya kwanza ya kuchelewa ni kujikuta una haraka.
Ukiwa na haraka ya kukimbiza gari kufika sehemu maana yake umechelewa, haukupangilia muda wako vizuri
Ukiwa na haraka ya kukamilisha malengo au ndoto zako mpaka unaanza kuchukua njia za mkato maana yake unahisi umechelewa, na hii hutokana na kutokuwa na njia nzuri ya kujiandaa na changamoto na vizuizi wakati wa kupanga.
Panga ratiba zako na maisha yako vizuri usiwe na haraka. Ukiona una haraka ujue tayari umeshachelewa.
#iThinkSo
Uwe na furaha
Uwe na afya
Uwe huru kutoka kwenye matatizo
Uwe na amani
Kama kuna kitu umejifunza, mtumie mtu mmoja unayemjali.
Rogers Katuma
Financial Artist, Senior Adventurer, Occasional Storyteller, and Amateur Golfer
